1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran: FIFA iipige marufuku Israel kufuatia mapigano Gaza

Amina Mjahid
10 Februari 2024

Shirikisho la soka la Iran limesema limeiomba bodi ya shirikisho la soka duniani FIFA kulisimamisha shirikisho la soka la Israel kufuatia vita vinavyoendeshwa na nchi hiyo katika ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4cFbA
Mehdi Taj
Rais wa shirikisho la soka la Iran Mehdi Taj Picha: Ffiri/Zuma/IMAGO

Katika taarifa iliyowekwa katika tovuti ya shirikisho la Iran, Jamhuri hiyo ya kiislamu iliiomba FIFA kulipiga marufuku shirikisho la Israel kushiriki shughuli zote za kandanda, na kuitaka pia FIFA na wanachama wake kuja na mikakati ya kuizuwia Israel kuendelea na uhalifu wake, na kutoa pia msaada wa chakula, maji na dawa kwa wapalestina. 

Mapigano ya Gaza yalianza Oktoba saba, baada ya wanamgambo wa Hamas kushambulia Kusini mwa Israel na kusababisha mauaji ya waisrael 1,160.

UN yahofia usalama wa raia walioko Rafah

Israel nayo ikajibu kwa mashambulizi ya angani na ardhini ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 27,000  wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Hayo ikiwa ni kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas. Israel imeapa kulitokomeza kabisa kundi hilo.