1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Intaneti ilivyochangamka na Kombe la Dunia

Bruce Amani
16 Julai 2018

Mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vya habari vinazungumzia kitu kimoja tu. Kombe la Dunia la 2018. Salamu za pongezi zinaendelea kutolewa baada ya fainali ya kukata na shoka uwanjani Luzhniki

https://p.dw.com/p/31X39
WM Finale Frankreich Pogba  Pokal
Picha: Getty Images/AFP/F. Fife

Tangu asubuhi, kinachozungumzwa tu ni Kombe la Dunia, Kombe la Dunia na Kombe la Dunia Zaidi

Gazeti maarufu la michezo la L'Equipe limeandika kichwa cha "Furaha ya milele”

Waziri wa michezo Laura Flessel alisema kwenye redio ya Europe 1 kuwa ushindi huo unawaruhusu vijana wa Ufaransa kama wale wa mitaa maskini ambayo wachezaji wengi wa timu ya taifa walikulia, kuendelea kuamini katika ndoto zao.

Na lakini sio vyombo vya habari vya Ufaransa tu vilivyoimiminia sifa kedekede timu yao. Hata nchini Croatia, vijana wao wamesifiwa kwa kuwa mashujaa baada ya taifa hilo dogo kuweka historia ya kucheza kwa mara yake ya kwanza fainali ya Kombe la Dunia.

"Ahsanteni, mashujaa! – mlitupa kila kitu!” kilisema kichwa cha gazeti la Sportske Novosti.

Nalo Gazeti la Vatreni likasema nyie ndo wakubwa, fahari yetu, majina yenu milele yataandikwa kwenye dhahabu!

Gazeti la Vecernji List likasema Croatia inawapongeza, nyie ni dhahabu yetu!

Na kama tu itakavyokuwa mjini Paris, zaidi ya mashabiki 100,000 wa nchi hiyo wanaikaribisha timu yao nyumbani leo katika mji mkuu Zagreb.

Russland WM 2018 Frankreich gegen Kroatien
Modric na Mbappe wachezaji boraPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Ujumbe wa mitandao ya kijamii

Intaneti pia ilijaa kila aina ya ujumbe kwa washindi na walioshindwa na hasa mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook. Na sio wachezaji wa zamani tu waliotoa salamu zao za pongezi, bali hata wanasiasa.

Rais wa Ufaransa aliandika neno moja tu kwenye Twitter akiiambia timu ya taifa: Merci kumaanisha ahsante.

Rais Donald Trump wa Marekani aliandika. Hongera kwa Ufaransa, ambao walicheza kandanda safi, kwa kushinda Kombe la Dunia 2018. Pia, Hongera kwa Rais Putin na Urusi kwa kuandaa kinyang'ayiro kizuri kabisa cha Kombe la Dunia. Mojawapo ya matamasha bora Zaidi!

Toni kroos anayechezea Ujerumani na Real Madrid aliandika: hongera Ufaransa na Raphael Varane. Mnastahili kuwa warithi wetu wa Kombe la Dunia la FIFA. Tembea kwa fahari Luka Modric na Mateo Kovac, mlifanya kazi nzuri sana na timu ya Croatia. Hao bila shaka ni wachezaji wenzake wa Real Madrid

Halafu beki wa Ujerumani na Bayern Munich Jerome Boateng akaandika, hongereni Ufaransa na ndugu zangu Corentin Toliso na Paul Pogba. Mnastahili taji hilo. Kisha akamtia moyo Mario Mandzukic akimwambia kuwa hayo ni mafanikio makubwa.

Naam kwa ujumbe huo ndipo nafika mwisho wa michezo kwa sasa, umekuwa na mi Bruce Amani kwaheri kwa sasa

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA/Reuters
Mhariri: Josephat Charo