1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

India yaadhimisha miaka 66 ya kuwa Jamhuri

26 Januari 2015

India inaadhimisha miaka 66 tangu kuwa Jamhuri katika sherehe inayoohudhuriwa na rais wa Marekani Barack Obama akiwa mgeni wa heshima

https://p.dw.com/p/1EQR4
Gwaride la Kijeshi juu ya ngamia katika siku ya Jamhuri India(26.01.2015)
Gwaride la Kijeshi juu ya ngamia katika siku ya Jamhuri India(26.01.2015)Picha: Reuters/Jim Bourg

India imeonyesha nguvu zake za kijeshi pamoja na utamaduni wake katika sherehe hizo zilizofanyika katika mji mkuu wa taifa hilo New-Delhi.Maelfu ya wananchi walijitokeza licha ya hali ya mawingu na manyunyu ya mvua kuangalia sherehe hizo za masaa mawili ambapo India ilionyesha nguvu zake za kijeshi kuanzia vifaru,helikopta za kijeshi pamoja na gwaride la kijeshi halikadhalika densi ya watoto wa shule.

Sherehe za kila mwaka zimefanyika hasa katika eneo la Rajpath huku sherehe nyingine ndogo zikifanyika kwenye maeneo mbali mbali ya nchi hiyo.India ilitangaza kuwa Jamhuri mnamo mwaka 1950 baada ya kupitisha katiba yake kufuatia kumalizika kwa utawala wa wakoloni Uingereza.

Rais Barack Obama mkewe Michelle Obama na rais Narendra Modi 26.1.2015
Rais Barack Obama mkewe Michelle Obama na rais Narendra Modi 26.1.2015Picha: Getty Images/Saul Loeb

Rais wa Marekani Barack Obama ambaye yuko katika ziara ya siku tatu nchini India ni rais wa kwanza wa Marekani kuwa mgeni ramsi katika sherehe hizo zilizofanyika chini ya usalama wa hali ya juu ambapo maelfu ya askari waliweka ulinzi uliojumuisha kuwakagua watu wote waliokuwa wakiingia kwenye eneo hilo la Rajpath.Hakuna mtu yoyote aliyeruhusiwa kuingia na simu ya mkononi ,Camera,mianvuli au hata kalamu katika sehemu hiypo.Takriban maafisa 50,000 wa usalama wa India walikuwa wakiweka ulinzi kwenye eneo la sherehe huku pia kukiweko walenga shabaha katika majengo marefu yanayozunguka eneo hilo.

Halikadhalika maajaasusi wa wamarekani sio chini ya 500 wako katika eneo hilo kwa mujibu wa kituo cha matangazo cha NDTV.Rais Barack Obama anaandamana katika ziara yake hiyo pamoja na mkewe Michelle.Katika sherehe hizo India imewakumbuka wanajeshi wake waliouwawa wakiwemo wake waliopoteza maisha wakati wa mgogoro kati ya taifa hilo na Pakistana kuhusiana na jimbo la Kashmir linalozozaniwa.

Rais Obama na mwenzake wa India,Pranab Mukherjee na Waziri mkuu Narendra Modi
Rais Obama na mwenzake wa India,Pranab Mukherjee na Waziri mkuu Narendra ModiPicha: picture-alliance/dpa/EPA/H. Tyagi

Shere za Jamhuri nchini India zinakuja baada ya hapo jana Jumapili kufanyika mazungumzo kati ya rais Obama na mwenyeji wake Narendra Modi ambapo walitangaza kufikiwa makubaliano kuhusu mpango wa Nuklia kwa ajili ya matumizi ya kawaida uliotiwa saini mwaka 2008 na ambao ulishindwa kutekelezwa kutokana na wasiwasi uliokuweko kwa makampuni ya Kimarekani uliotokana na sheria ya India kuhusiana na masuala ya ajali za Nyuklia.

Imekubaliwa kwamba paweko makampuni maalum ya Bima yatakayoshughulikia makampuni pindi inatokea ajali katika mitambo ya Nyuklia.Rais Obama amepangiwa kukutana na viongozi wa juu wa upinzani wa chama cha Nationala Congress cha India baadae hii leo pamoja na kufanya mikutano na wakuu wa makampuni wa kibiashara ya Marekani mkutano ambao atahudhuria pamoja na mwenyeji wake.

Rais Obama na Mkewe walipangiwa pia kutembelea eneo maarufu Taj Mahal huko Agra lakini ziara hiyo imefutwa na badala yake Obama na mkewe watakwenda Saudi Arabia Jumanne kutoa pole zao kwa familia ya mfalme Abdulla aliyefariki na kuzikwa Ijumaa iliyopita.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri:Iddi Ssesanga