1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Wasichana waliofukuzwa shule Tanzania wateseka

Grace Kabogo
7 Oktoba 2021

Shirika la kimataifa la haki za binaadamu Human Rights Watch limesema wasichana wanaofukuzwa shule kwa kupata ujauzito Tanzania wanakosa haki yao ya kupata elimu. Wanataka marufuku iondolewe.

https://p.dw.com/p/41NxM
Tansania Mädchenschule Schülerinnen Afrika
Picha: Zuberi Mussa

Kwa mujibu wa Human Rights Watch, tangu mwezi Juni mwaka 2017, Rais John Magufuli na mrithi wake Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alichukua madaraka Machi mwaka 2021, baada ya kifo cha Rais Magufuli, wametekeleza marufuku inayowataka wanafunzi wanaopata mimba au waliojifungua kutorudi shuleni. Mtafiti wa ngazi ya juu wa shirika hilo anayeshughulikia haki za watoto, Elin Martinez anasema wasichana wa Tanzania wanateseka kwa sababu serikali inasisitiza kuhusu sera ambayo inawanyima haki yao ya kupata elimu, inawadhalilisha na inawatenga na kuharibu maisha yao ya baadae.

Sera hiyo haifai

Katika ripoti hiyo iliyotolewa Alhamisi, Martinez anasema serikali inapaswa kuachana mara moja na sera hiyo isiyo ya kibinaadamu na kuwaruhusu wanafunzi wajawazito na waliojifunga kurejea shule, kwani hatua ya serikali ya Tanzania kuwapiga marufuku wasichana wanaopata mimba na waliojifungua kuendelea na masomo imewanyima maelfu ya wasichana haki yao ya kupata elimu.

Mwezi Julai na Agosti, Human Rights Watch iliwahoji wasichana na wanawake 30 wenye umri wa kuanzia miaka 16 hadi 24. Wote hao walifukuzwa shule za msingi na sekondari kati ya mwaka 2013 na 2021 kwa sababu ya kupata ujauzito.

Maafisa wa serikali na walimu ndiyo watekelezaji wa sera hiyo ya serikali, mara nyingi kwa njia ambazo zinawadhalilisha na kuwanyanyapaa wasichana, pamoja na wazazi na walezi wao. Wengi wa hao waliohojiwa walipimwa ujauzito wakiwa shule au kwenye hospitali au zahanati za mkoa, na kisha walifukuzwa shule baada ya muda mfupi.

Lagos Nigeria Frauen freigelassen
Msichana mjamzitoPicha: Reuters TV

Wasichana kadhaa walifukuzwa shule kabla ya kumalizia elimu yao ya chini ya sekondari, hatua muhimu kwa wanafunzi wengi. Baadhi yao hawakufanikiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka uliopita, kwa sababu shule ziliwapima wanafunzi, siku chache kabla ya kufanya mitihani au katikati ya mitihani hiyo.

Mwaka 2020, maafisa wa shule ya mkoa wa Morogoro walimfukuza shule msichana mwenye umri wa miaka 16 katikati ya mihitani yake, ingawa alikuwa amebakiza kufanya mitihani miwili tu ya kidato cha nne. Msichana huyo anasema walimu wake hawakumsikiliza kabisa. Wasichana wengi waliohojiwa hawakuandikishwa kwenye miradi ya kupata mafunzo au vituo mbadala vya elimu. Baadhi yao walijiandikisha katika mafunzo yasio rasmi kama vile ushonaji, na wengine walihudhuria shule isiyo ya kiserikali ambayo inawasaidia wasichana waliofukuzwa shule za umma.

Wanafunzi kurudi shule

Mwaka 2020, serikali ya Tanzania ilitangaza kwamba itawaruhusu wanafunzi waliopata mimba au waliojifungua kujiandikisha katika mpango wa elimu, unyojulikana kama ''njia mbadala wa elimu.'' Mpango huu utagharimu dola milioni 180 kutoka katika mkopo wa dola milioni 500 uliotolewa na Benki ya Dunia kwa ajili ya Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari nchini Tanzania, SEQUIP.

Shirika la Human Rights Watch limesema kuwa Rais Samia anapaswa kutoa agizo la kumalizwa kwa sera ya kuwafukuza shule wasichana wanaopata mimba, na kuiamuru wizara ya elimu, sayansi na teknolojia, kupitisha sera inayolinda haki za wasichana wanaopata mimba shuleni pamoja na waliojifungua, kusoma katika shule za umma.

(HRW https://bit.ly/3BkGW69)