1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Uganda ichunguze ukandamizaji wa wanaharakati

Bruce Amani
11 Februari 2022

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limeihimiza serikali ya Uganda kuchunguza haraka ripoti kuwa maafisa wa kijeshi walimtesa mwandishi wa tashtiti aliyekimbilia uhamishoni

https://p.dw.com/p/46s7V
Uganda Autor Kakwenza Rukirabashaija
Picha: ABUBAKER LUBOWA/REUTERS

Mtafiti wa HRW nchini Uganda Oryem Nyeko amesema ni jambo lisilovumilika kwamba vikosi vya usalama Uganda bado vinawatesa na kuwatendea unyama wafungwa. Anasema badala ya kuwashitaki wakosoaji wao kwa sababu ya ujumbe wanaoandika kwenye mitandao ya kijamii, serikali ya Uganda inapaswa kuwa inachunguza kisa hiki na tuhuma nyingine nyingi nzito za mateso yanayofanywa na vyombo vya usalama katika miaka ya karibuni.

Mnamo Desemba 28, 2021 maafisa wa kijeshi walimkamata Rukirabashaija nyumbani kwake Kampala na kumpelekwa eneo lisilojulikana. Alishikiliwa kwa siku 14 bila kuwasiliana na familia wala mawakili. Alishitakiwa kwa kumkosoa Rais Yoweri Museveni na mwanawe Muhoozi Kainerugaba. Aliikimbia nchi Februari 9, kwenda kutibiwa majeraha aliyopata kwa kuteswa kizuizini.

Soma pia: Mkosoaji wa rais Museveni aitoroka Uganda

Rukirabashaija aliliambia shirika la Human Rights Watch kuwa maafisa wa jeshi walimpiga, wakamlazimisha kucheza densi kwa masaa mengi, wakaunyofoa mwili wake kwa kutumia koleo, na kumchoma sindano yenye vitu visiovyojulikana. Maafisa walimhoji kuhusu uhusiano wake na wanafanyakazi wa Umoja wa Ulaya, balozi za Marekani na Uingereza, na kitabu chake cha Banana Republic, ambacho kinaelezea matukio yake ya kukamatwa huko nyuma na kuzuiliwa na jeshi mwezi Aprili na Septemba 2020. Anasema maafisa walimlazimu kurekodi ujumbe wa video wa kumuomba radhi Museveni na Kainerugaba.

Uganda Kultur l Aktivistin und Schriftstellerin Dr. Stella Nyanzi in Kampala vor Gericht
Mwanaharakati Stella Nyanzi aliwahi kukakamatwa na serikaliPicha: picture alliance/AP Photo/R. Kabuubi

Maafisa wa Uganda mara kwa mara hutumia Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta ili kubinya uhuru wa kujieleza mitandaoni, hasa kama maudhui yanawagusa maafisa waandamizi wa serikali.

Mamlaka nchini humo ziliwalenga wanaharakati wengine wanaomkosoa rais na wale walio karibu nae chini ya sheria hiyo. Mnamo Agosti 2019, mahakama ilimkuta na hatia msomi na mwanaharakati Stella Nyanzi, na kumhukumu kifungo cha miezi 18 jela kwa shairi alilochapisha kwenye Facebook, mwaka wa 2018 akimkosoa Rais Museveni. Jaji wa mahakama kuu alifanya uamuzi Februari 2020 kuwa haki ya Nyanzi ya kupitia utaratibu unaofaa ilikiukwa wakati wa kesi yake na akakibatilisha kifungo chake.

Mnamo Februari 5, 2021, maafisa wa polisi waliovalia nguo za kiraia walimkamata Michael Muhima, mwanafunzi wa sheria, nyumbani kwake Kampala kuhusiana na ujumbe wa Twitter uliomkejeli msemaji wa polisi, Fred Enanga. Mamlaka kisha zikamshtaki Muhima kwa kile walichokiita "mawasiliano ya kukera.” Muhima alifungwa jela na akazuiwa kuwasiliana na familia na mawakili wake kwa siku tano kabla ya kuwachiwa kwa dhamana.

Sheria ya Uganda na vyombo vya kimataifa vinazuia ukamataji wa kiholela, kuzuiliwa watu kinyume cha sheria na mateso.

HRW imesema kukamatwa kwa Rukirabashaija ni tukio la karibuni tu katika matukio yanayoongezeka Uganda ya ukandamizaji dhidi ya maoni yanayoonekana kuikosoa serikali. Nyeko anasema serikali inapaswa kukomesha matukio hayo na kushughulikia hoja zinazoibuliwa na wakosoaji badala ya kuwatesa.

Chanzo: HRW