1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Macron amteua Attal kuwa Waziri Mkuu mpya

Lilian Mtono
9 Januari 2024

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amemteua Gabriel Attal kuwa Waziri Mkuu mpya. Attal anachukua nafasi ya Elisabeth Borne aliyejiuzulu jana Jumatatu sambamba na serikali nzima ya Ufaransa.

https://p.dw.com/p/4b1ph
Ufaransa | Gabriel Attal
Waziri Mkuu wa Ufaransa Gabriel Attal, amechukua nafasi ya Elisabeth Borne aliyejiuzulu sambamba na serikali nzima ya UfaransaPicha: Firas Abdullah/abaca/picture alliance

Attal anakuwa waziri mkuu mwenye umri mdogo kabisa kuwahi kuteuliwa nchini humo. 

Tangazo la uteuzi wa Attal limetolewa na ikulu ya Elysee mchana wa leo na kusema Rais Macron tayari amempa jukumu la kuunda serikali. Waziri Mkuu huyo pamoja na kuandika historia ya kushika wadhifa huu wa ngazi za juu serikalini akiwa na umri mdogo kabisa wa miaka 34, anaadaika pia historia nyingine ya kuwa kiongozi wa serikali aliyeweka wazi kwamba anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Attal anatazamiwa kuleta mabadiliko makubwa ya kimtindo katika ofisi ya waziri mkuu baada ya Elisabeth Borne mwanamke wa pili kuwahi kuiongoza serikali ya Ufaransa, huku pia kukitarajiwa mabadiliko makubwa ya Baraza la mawaziri wiki hii, wakati Macron akisaka sura mpya kwa ajili ya kukabiliana na miaka mitatu ya mwisho ya utawala wake na hasa baada ya maandamano maubwa ya kupinga mageuzi yaliyopingwa vikali ya pensheni, kupoteza wingi wa viti katika uchaguzi wa bunge na sintofahamu juu ya sheria ya uhamiaji.

Attal, alipata umaarufu zaidi kote nchini Ufaransa alipokuwa msemaji wa serikali wakati wa janga la UVIKO-19. Na katika uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni ameonekana kama mmoja ya wanasiasa mashuhuri zaidi nchini humo na mshirika wa karibu mno wa Macron.

Uteuzi wake unafanyika wakati Macron na washirika wake wa mrengo wa kati wakiangazia namna ya kupunguza kasi ya chama cha mrengo wa kulia chini ya mwanasiasa Marine Le Pen kabla ya uchaguzi wa Bunge la Ulaya katika majira ya joto.

Ufaransa | Emmanuel Macron na Gabriel Attal
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri wake mkuu Gabriel Attal, wakati huo akiwa waziri wa elimu, kabla ya gwaride la kijeshi la Siku ya Bastille katika barabara ya Champs-Elysees huko Paris mnamo Julai 14, 2019.Picha: Raphael Lafargue/abaca/picture alliance

Hata hivyo, mtaalamu wa masuala ya katiba Benjamin Morel ameliambia shirika la habari la AFP kwamba uteuzi huo ni ishara ya nguvu na ya kimkakati kuelekea uchaguzi huo, ingawa mwanasayansi wa wa siasa Bruno Cautres akisema hautasaidia chochote na wala hautasuluhisha tatizo kubwa ambalo ni kule mamlaka ya Macron inakoelekea.

Anakumbukwa kwa kuzuia "Abaya" mashuleni

Alipoteuliwa kuwa Waziri wa Elimu mwaka uliopita, hatua ya kwanza aliyochukua ilikuwa ni kuzuia vazi la Kiislamu la Abaya katika shule za serikali na kumwagiwa sifa na wanasiasa wa kihafidhina licha ya asili yake ya kuwa mwanasiasa wa mrengo wa kushoto ambaye baadaye aliungana na vuguvugu la mrengo wa kati la Macron.

Baada ya uteuzi huo, aliwahakikishia wanataaluma katika mkutano na wakuu wa shule za sekondari kwa njia ya mtandao kwamba ataendelea kuwaunga mkono.

Soma pia: Baadhi ya shule zafungwa Ufaransa kutokana na kunguni

"Ninaungana nanyi kwamba shule ndio silaha yenye nguvu zaidi tuliyonayo katika kubadilisha jamii. Na imani hii imeongezeka nguvu kila wakati tangu nilipoteuliwa niwe nanyi, na kwa chochote kinachoweza kutokea, hili nitabaki nalo ili kutimiza dhamira yenu."

Ingawa Macron hataweza kugombea tena katika uchaguzi wa mwaka 2027, mageuzi katika serikali yake yanachukuliwa kuwa ni ya muhimu ili kuepusha mashaka ya taifa hilo hatimaye kuongozwa na Le Pen. Hata hivyo, gazeti la kila siku la Le Figaro la nchini humo limesema mabadiliko kwenye safu ya juu ya uongozi hayatasaidia kubadilisha picha nzima na kuongeza kuwa Atta atakabiliwa na dharura lukuki za kisiasa ikiwa ni pamoja jukumu la kuliunganisha taifa hilo lililomeguka.

Waziri Mkuu mdogo kabla yake alikuwa Laurent Fabius aliyeteuliwa mwaka 1987 na aliyekuwa rais wakati huo Francois Matterand. Alikuwa na miaka 37.