1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Senegal wanatarajia nini kutoka kwa Faye?

Lilian Mtono
27 Machi 2024

Akiwa na umri wa miaka 44, Bassirou Diomaye Faye atakuwa rais wa tano wa Senegal na mdogo zaidi baada ya mgombea huyo wa upinzani kumshinda mgombea wa chama tawala. Ni yepi matarajio ya Wasenegal kutokana na urais wake?

https://p.dw.com/p/4eAG5
Rais mpya wa Senegal Bassirou Diomaye Faye
Rais mpya wa Senegal Bassirou Diomaye Faye anatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumiPicha: Luc Gnago/REUTERS

Bassirou Diomaye Faye amemshinda mgombea wa chama tawala alieteuliwa na rais anaeondoka madarakani Macky Sall. Pamoja na mshauri wake Ousmane Sonko, Faye ni sehemu ya kizazi kinachoinukia cha wanasiasa wa Afrika na anajitanabahisha kama mtu wa mabadiliko na anaejitenga na yaliopita.  

Faye anasema msingi hasa wa mradi wake wa kisiasa ni kuzifanyia marekebisho taasisi za Jamhuri na kurejesha serikali yenye msingi wake katika utawala wa sheria ambavyo anadai vilipuuzwa na Macky Sall, rais anaemaliza muda wake alieiongoza Senegal kwa mihula miwili.

Faye anasema anataka kupambana dhidi ya kile alichokiita mamlaka yaliopitiliza ya taasisi ya urais, ambayo amesema yamesababisha mhimili wa urais kuidhibiti kikamilifu mihimili ya bunge na mahakama na hivyo kupelekea kutumia vibaya sheria kuwakandamiza wapinzani na kuwafunga jela.

Mkuu huyo ajae wa nchi ameahidi kupunguza mamlaka ya rais, akitarajia kuanzisha sheria ya kumuondoa madarakani rais, wadhifa wa makamu wa rais, kupiga marufuku ulimbikizaji wa mamlaka ya kisiasa, kupambana na rushwa na kuanzisha hatua mbadala kwa kifungo cha gerezani.

Soma pia: Sonko azungumza na wafuasi wake baada ya kuachiliwa huru

Baadhi ya viongozi waliopo na wastaafu wa Jumuiya ya ECOWAS katika mkutano uliofanyika mjini Abuja
Senegal chini ya utawala mpya inaangazia pia kuimarisha ushirikiano wake na Jumuiya ya Maendeleo kwa mataifa ya Magharibi, ECOWAS.Picha: Kola Sulaimon/AFP

Rais huyo mpya ameapa kurejea uhuru wa taifa, neno ambalo alitumia si chini ya mara 18 katika ilani yake ya uchaguzi, ambayo ni pamoja na dhamira ya kujadili upya mikataba ya madini na hidrokaboni ambayo inatazamiwa kuanza kutekelezwa mwaka huu.

Faye aahidi kuipitia upya mikataba ya uvuvi na mataifa ya kigeni

Faye pia anataka kutathmini upya mikataba ya uvuvi na mataifa ya kigeni, wakati ambapo rasilimali za samaki ambazo zinasaidia karibu familia 600,000 za Senegal zinapungua, zinaporwa - wanasema, na meli za Ulaya na Asia. Zaidi ya hayo, ilani yake inasisitiza haja ya kuendeleza sekta ya msingi ili kuhakikisha usalama wa chakula na kuelekea katika kujitosheleza, hasa chakula kikuu cha mchele.

Faye pia ameahidi mageuzi ya kifedha, yaumkini hata kuanzishwa kwa sarafu mpya iitwayo Senegal, badala ya faranga ya CFA, ambayo ni sarafu ya kikanda iliyoanzisha kabla ya uhuru miaka 65 iliyopita kutoka kwa mkoloni wa zamani Ufaransa na ambayo inahusishwa na sarafu ya euro.

Kiongozi huyo ajaye anataka kusawazisha ushirika wa kimataifa na kupanga upya uhusiano na Ufaransa, ambayo ndiyo mshirika mkuu wa kibiashara wa Senegal. Mshirika wake Sonko, alikuwa pia ameashiria enzi ya kusawazisha uhusiano wa Dakar na ulimwengu. Mchambuzi wa kisiasa kutoka taasisi ya ushauri ya Wathi, Babacar Ndiaye, anasema wanachotaka viongozi hao vijana ni sera ya manufaa kwa wote, ya uzalendo wa kiuchumi.

Soma pia:Senegal inajiandaa kuwa mzalishaji wa mafuta baadae mwaka huu.

Akidai kuwa Mwana Afrika, Faye anataka kuimarisha uwepo wa kidiplomasia wa Senegal kote Afrika na kukuza ushirikiano wa kikanda ndani ya ECOWAS huku akiimarisha jukumu la bunge na mahakama ya haki ya Senegal.

Wapiga kura wa Senegal walimuunga mkono Faye katika duru ya kwanza wakimuona kama mtu atakaendokana na hali ya msukosuko ya hivi karibuni nchini humo na kuleta mabadiliko. Lakini hakutakuwa na muda wa kustarehe, alionya Ndiaye, ambaye alisema watu watataka kuona matokeo haraka.