1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yazipa Ukraine na Moldova hadhi ya wagombea kujiunga

John Juma
24 Juni 2022

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamezipa Ukraine na Moldova 'hadhi ya kuwa wagombea' kujiunga na umoja huo.

https://p.dw.com/p/4DA6D
EU-Gipfel in Brüssel
Picha: Geert Vanden Wijngaert/AP Photo/picture alliance

Uamuzi huo ulifikiwa baada ya majadiliano baina ya viongozi wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wa kilele mjini Brussels jana Alhamisi. 

Kupewa hadhi ya kugombea uanachama wa Umoja wa Ulaya ni ishara thabiti ya mshikamano wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya dhidi ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Umuzi huo wa viongozi wa Umoja wa Ulaya ni hatua ya kwanza miongoni mwa nyingine nyingi kwa Ukraine na Moldova kujiunga na umoja huo. Hatua hiyo imejiri mnamo wakati Marekani imesema inaipa Ukraine misaada zaidi ya mifumo ya kisasa ya roketi.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliupongeza uamuzi huo akisema ni wa kipekee na kihistoria. Hii ni licha ya mataifa hayo wanachama wa zamani wa muungano wa Soviet, kuwa na safari ndefu kabla yajiunge rasmi na kunufaikia faida za kuwa mwanachama ikiwemo soko la pamoja.

"Tumepokea hadhi ya ugombea. Huu ni ushindi wetu. Tumesubiri kwa siku 120 n miaka 30. Tutamshinda adui na tupumzike. Au labda tutaijenga Ukraine upya ndipo tupumzike. Au tushinde, tuijenge nchi upya, tuingie Umoja wa Ulaya kisha tupumzike. Au labda hatutapumzika," amesema Zelensky.

Macron: Hii ni ishara kali kwa Urusi

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron asema anafikiri hatua ya EU kuzipa Ukraine na Moldova hadhi ya ugombea ni ujumbe mkali kwa Urusi.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron asema anafikiri hatua ya EU kuzipa Ukraine na Moldova hadhi ya ugombea ni ujumbe mkali kwa Urusi.Picha: Olivier Matthys/AP Photo/picture alliance

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron naye amesema uamuzi huo wa viongozi wa Umoja wa Ulaya ni "ishara kali” kwa Urusi kwamba nchi za Ulaya zitaunga mkono matarajio ya Ukraine.

"Nafikiri huu ni ujumbe mkali. Tangu siku ya kwanza ya mgogoro huu , Ulaya imekuwa ikichukua hatua za kihistoria, kwa haraka na mshikamano. Kuanzia vikwazo, kisha uchumi, msaada mkubwa wa kijeshi na kifedha na sasa ishara hii ya kisiasa," amesema Macron.

Rais wa Urusi Vladimir Putin alitangaza Ukraine kuwa sehemu ya eneo la Urusi na alisisitiza kwamba alichukua hatua kufuatia majaribio ya kutaka nchi hiyo kujiunga na Jumuiya ya kujihami ya NATO, ambao ni muungano wa kijeshi unaokuja na dhamana ya kiusalama.

Majaribio ya hivi karibuni ya nchi za Magharibi kuimarisha uungwaji mkono kwa Ukraine yanajiri mnamo wakati Urusi imefunga miji muhimu eneo linalozozaniwa mashariki mwa Ukraine, hivyo kuibua wasiwasi wa kimataifa kuhusu vikwazo dhidi ya mauzo ya gesi na nafaka.

Ukraine na Moldova zilituma maombi ya kutaka kujiunga na umoja huo, wiki chache tu baada ya Urusi kuivamia Ukraine.

Tayari Umoja wa Ulaya umeainisha hatua ambazo sharti Ukraine itimize, ikiwemo kuimarisha utawala wa sheria na kupambana na ufisadi.

Mfumo Himars unaweza kufyatua makombora kadhaa kwa usahihi mkubwa

Mfumo kwa jina Himars unaweza kufyatua makombora kadhaa kwa usahihi mkubwa katika masafa marefu.
Mfumo kwa jina Himars unaweza kufyatua makombora kadhaa kwa usahihi mkubwa katika masafa marefu.Picha: Kento Nara/Geisler-Fotopress/picture alliance

Katika tukio jingine, ikulu ya rais White House nchini Marekani imetangaza kwamba inaipa Ukraine silaha zenye thamani ya dola milioni 450 ikiwemo mfumo wa kisasa wa roketi.

Mfumo huo kwa jina Himars unaweza kufyatua makombora kadhaa kwa usahihi mkubwa katika masafa marefu.

Tayari mifumo minne kama hiyo imeshawasilishwa Ukraine. Aidha baadhi ya wanajeshi wa Ukraine wanapewa mafunzo kuhusu namna ya kuitumia mifumo hiyo.

Utawala wa Biden umesema Ukraine imewapa uhakikisho kwamba hawatafyatua makombora ndani ya Urusi.

Mahitaji ya Ukraine yamekuwa yakiongezeka kwa dharura, huku Urusi iliyoshindwa kukamata mji mkuu Kyiv mwanzoni mwa uvamizi huo ulioanza Februari 24, ukisonga mbele sasa maeneo ya mashariki, kukamata mji muhimu kimkakati wa Severodonetsk na Lysychansk.

Udhibiti wa miji hiyo itaipa Urusi udhibiti wa jimbo lote la Luhansk, hivyo kuviwezesha vikosi vyake kusonga ndani zaidi jimbo la Donbas na labda hadi magharibi.

Siku ya Alhamisi, Ukraine ilisema imepoteza udhibiti wa maeneo mawili ambako vikosi vyake vilikuwa vikiilinda miji hiyo miwili na kwamba vikosi vya Urusi sasa vinakaribia kuzingira miji hiyo ya viwanda.

(AFPE)