1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cote d'Ivoire yampa kocha Fae mkataba wa kudumu

Bruce Amani
20 Februari 2024

Emerse Fae ametuzwa kwa kuiongoza Cote d'Ivoire kubeba Kombe la Mataifa ya Afrika - AFCON akiwa kocha wa muda. Chama cha kandanda nchini humo kimemthibitisha kuwa kocha wa kudumu

https://p.dw.com/p/4cb1M
Fae Emerse kocha wa Cote d'Ivoire
Fae aliwaongoza wenyeji Cote d'Ivoire kubeba kombe la AFCON baada ya kocha mkuu kutimuliwaPicha: Sydney Mahlangu/Sports Inc/empics/picture alliance

Cote d’Ivoire walishindwa 1 – 0 na Nigeria katika mechi yao ya pili kabla ya kubamizwa 4 – 0 na Guinea ya Ikweta, ikiwa ni kipigo kizito kabisa kuwahi kuwakuta kwenye ardhi ya nyumbani. Matokeo hayo yakawafanya kuwa wenyeji wa kwanza wa AFCON katika miaka 40 kupoteza mechi mbili za makundi. Kocha Jean-Louis Gasset akafungashiwa virago. Mchezaji wao wa zamani Emerse Fae, akatwikwa mzigo wa kuwa kocha wa muda. 

Cote d’Ivoire wakawapiga mabingwa watetezi Senegal kwa mikwaju ya penalti katika hatua ya 16 za mwisho baada ya kuwasazisha bado katika dakika za jioni za muda wa kawaida.
 
Wakawafunga Mali 2 – 1 katika robo fainali kwa kupata bao la ushindi katika muda wa ziada, baada ya kubaki wachezaji 10 katika kipindi cha kwanza. Kisha wakapata ushindi wa 1 – 0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika nusu fainali. Katika fainali waliwafunga Nigeria 2 - 1.