1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chadema: Maandamano yatafanyika kama yalivyopagwa

George Njogopa 17 Januari 2024

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema kimesisitiza kuwa maandamano yake ya kuishinikiza serikali iondoe bungeni miswaada inayohusu vyama vya siasa na uchaguzi yatafanyika kama ilivyopangwa Januari 24

https://p.dw.com/p/4bNCT
Tansania Daressalam | Wafuasi wa chama cha chadema
Chdema yatangaza kuendelea na maandamano yake Januari 24Picha: Eric Boniphace/DW

Hatua ya chama hicho kutoa tamko hilo inafuatia kauli ya hivi karibuni ya mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila aliyesema wanajeshi wapatao 500 watafanya usafi siku hiyo ambayo chama hicho kilishapanga kufanya maandamano.

Katika mkutano na waandishi habari, katibu mkuu wa Chadema John Mnyika, amesema chama hicho kimeshaandaa barua zilizotumwa kwa makamanda wa polisi kuelezea sehemu ambako maandamano hayo ya amani yatapitia.

Baadhi ya maeneo yaliyotajwa na mwanasiasa huyo ni pamoja na yatakayoanzia pembezoni mwa mji na mengine kutokea eneo la buguruni kupitia maeneo ya katikati ya mji.

Kilele cha maandamano hayo kwa mujibu wa Mnyika ni katika ofisi za Umoja wa Mataifa ambako ujumbe maalumu utasomwa.

Mbali ya ajenda ya kisiasa maandamano hayo pia yanakusudia kutoa ujumbe unaoitaka serikali kuandaa mpango maalumu wa dharura kwa ajili ya kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha.

Chama hicho kimesisitiza kuwa maandamano ni haki ya kikatiba hivyo chama cha Chadema kitachukua hatua  zote kuyafanikisha

Baadhi ya vyama vya upinzani vyataka maandamano ya Chadema yadhibitiwe

Tansania Daressalam | Wafuasi wa Chadema
Chama kikuu cha upinzani Tanzania Chadema chasema maandamano ya kuishinikiza serikali iondoe bungeni miswaada inayohusu vyama vya siasa na uchaguzi yatafanyika kama ilivyopangwa.Picha: Eric Boniphace/DW

Wakati chama hicho kikiitisha maandamano hayo, kwa upande mwingine umoja wa vyama vya upinzani umejitokeza hadharani kuyakosoa ukitaka yadhibitiwe na vyombo vya dola.

Kwa kutoa hoja mbalimbali, umoja huo umekilaumu chama cha Chadema kwa mkakati wake wa kutaka kujibainisha kama chama pekee chenye ushawishi katika siasa za nchi.

Mmoja wa viongozi wa chama hicho aliyeongoza mkutano na waandishi wa habari Abdul Mluya alisema haoni umuhimu wa maandamano hayo wakati milango ya maridhiano ingali iko wazi.

Baadhi ya vyama vya upinzani vimekuwa vikikosoa baadhi ya vipengele katika miswaada yote mitatu iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni, ikiwamo muswaada unaoangazia vyama vya siasa pamoja na uchaguzi.

Tume huru ya uchaguzi ni miongoni mwa maeneo yanayotupiwa macho na vyama hivyo. Baadaye mwaka huu Tanzania itaendesha uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofuatiwa na uchaguzi mkuu mwaka ujao wa 2025.

Mwandishi: George Njogopa