1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Uganda lalaani ukandamizaji wakati wa uchaguzi

Admin.WagnerD29 Januari 2021

Spika wa Bunge la Uganda, Rebecca Kadaga ameiagiza kamati ya bunge hilo kuchunguza visa vya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ulioshuhudiwa katika kipindi cha uchaguzi.

https://p.dw.com/p/3oZGU
Uganda Kampala  Rebecca Kadaga Sprecherin Parlament
Picha: DW/Lubega Emmanuel

Spika wa Bunge la Uganda, Rebecca Kadaga ameiagiza kamati ya bunge hilo kuchunguza visa vya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ulioshuhudiwa katika kipindi cha uchaguzi. Aidha bunge hilo limehoji mwendelezo wa kamatakamata ya raia bila wao kufikishwa mahakamani, hali ambayo wanaelezea inazidi kuwaweka jamaa na marafiki katika hofu na mashaka.

Kulingana na wanaharakati wa haki za binadamu zaidi ya watu 500 wamekamatwa na kuhujumiwa na vyombo vya kisheria katika kipindi cha miezi miwili kuelekea uchaguzi mkuu. Hadi sasa takriban watu 60 wameuawa na baadhi hawajulikani waliko.

Hali hii ndiyo imemlazimu Spika wa Bunge la Uganda, Rebecca Kadaga kutaka ufafanuzi kuhusu hali hii ambayo imezitia familia kadhaa katika hofu, wasiwasi na majonzi kuhusu maisha ya watu wao. Akiongoza kikao cha kwanza tangu kufanyika kwa uchaguzi uchaguzi,Spika Kadaga amesema.

''Ningependa kuvihimiza vyombo vya dola kuheshimu utawala wa sheria na walinde haki za binadamu, naiagiza kamati ya bunge ichunguze visa vya ukiukaji wa haki za binadamu na kutoa ripoti katika muda wa mwezi mmoja'' alisema spika Kadaga.

Uganda Festnahme Robert Kyagulanyi aka Bobi Wine
Polisi wa Uganda wakiwa wanamburuta mfuasi mmoja wa mwanasiasa Bobi Wine katika kipindi cha kampeni.Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Kinachoshtusha na kushangaza ni kwamba hata Waziri wa usalama wa nchi, Jenerali Jeje Odong anadai hajui kinachoendelea kuhusu mienendo ya ukiukwaji wa haki za binaadamu na vyombo vya usalama ambavyo anavitumikia.

Baada ya kuulizwa na wanahabari kuhusu kutoweka kwa watu mbalimbali ambayo orodha yao imechapishwa katika vyombo kadhaa vya habari, waziri huyo amesema amemuagiza mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai CIID, Grace Akulo kuchunguza ni akina nani wanatekeleza vitendo vya kuwateka nyara raia katika mazingira yasiyoeleweka. Jenerali Jeje Odong amesema.

Okulo alisema, ''Uchunguzi huu hasa ni kubaini kipi kati ya vyombo vya usalama kinahusika katika visa hivi''

Wakitoa michango yao, wabunge mbalimbali wamemuelezea spika jinsi watu kadhaa wanaowawakilisha walivyo katika mashaka makubwa kuhusu ushiriki wao katika siasa za upinzani. Hii ni kwa sababu wengi wao ndiyo wanalengwa na wanaohusika na kamatakamata kama anavyofafanua zaidi kiranja wa upinzani bungeni Ibrahim Semujju Nga'nda.

''Watu wanalala nje ya nyumba zao baada ya jamaa zao kutekwa nyara. Wakati mwingine watu hao wanavunja nyumba na kuwaburuta waume na watoto wao", alisema.

Waziri Mkuu Dokta Ruhakana Rugunda amekubaliana na spika kwamba serikali inawajibika kuufahamisha umma kuhusu mienendo ya ukiukaji wa haki za binadamu hasa inayofanywa na vyombo vya usalama. Ameunga mkono agizo la spika kwa waziri kutoa taarifa kuhusu hali hiyo katika kipindi cha wiki mbili. Waziri mkuu amesema.

Rugunda alisisitiza ''Ni sawa kabisa kwa viongozi wa kisiasa wapate taarifa kutoka kwa serikali kuhusu hali ilivyo. Serikali inachukulia usalama wa watu wote kuwa suala nyeti."

Huku hayo yakijiri, hatimaye msaidizi wa aliyekuwa mgombea urais wa upinzani Robert Kyagulanyi ajulikanaye kama Selekta Davie amethibitishwa kuwa yuko hai na atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka kutokana na kushiriki maandamano haramu mwaka 2018.

Soma Zaidi:Maoni: Waganda wamemchoka Museveni lakini hawawezi kumuondoa 

Lubega Emmanuel DW Kampala.