1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bobi Wine azinduwa maandalizi kuelekea uchaguzi wa 2026

Mohammed Khelef
28 Agosti 2023

Umati wa wafuasi wa chama cha upinzani cha NUP nchini Uganda wameandamana kwenye mjini Mbarara wakimshangilia kiongozi wao, Robert Kyagulanyi (Bobi Wine), aliyezinduwa harakati za maandalizi ya uchaguzi wa mwaka 2026.

https://p.dw.com/p/4VfXG
Uganda | Opposition | Bobi Wine
Picha: Nicholas Bamulanzeki/AP Photo/picture alliance

Akiwahutubia watu wa sehemu hiyo, Bobi Wine aliihimiza jamii ya Waankole kuondokana na kasumba kwamba watu wa jamii zingine za Uganda zina uhasama dhidi yao na Yoweri Museveni akiondoka madarakani watalipiza kisasi dhidi yao, akisema hiyo imekuwa mbinu ya Rais Yoweri Museveni kusababisha migawanyiko miongoni kwa raia ili kuendeleza utawala wake.

Adui wa Museveni ni Museveni mwenyewe - Bobi Wine

"Nataka mfahamu kuwa walituvisha hofu. Tumekuwa tukipigana hiyo hofu wakati wote." Alisema mwanamuziki huyo aliyegeuka alama ya siasa za upinzani nchini Uganda.

Soma zaidi: Museveni aadhimisha miaka 37 tangu alipoingia madarakani

Viongozi wa NUP katika eneo hilo waliwataka watu wa jamii nyingine za Uganda wafahamu kuwa watu wa Ankole pia hukumbwa na hali ngumu za maisha licha ya kuwa rais wa sasa anatokea sehemu hiyo, na ndiyo maana nao wanamuunga mkono Bobi Wine alete mageuzi kabambe katika utawala wa Uganda.

"Hamna kazi, hamna dawa hospitalini, barabara zenu zi nzuri na ndivyo hali ilivyo Ankole kama sehemu zingine za nchi. Hatuna kazi, hatuna pesa huu ni wakati wetu sote kujipigania." Alisema mmoja wao.

NUP yaonesha ingali hai

Wafuasi wa chama hicho waliuelezea  mkutano huo kuwa  kielelezo cha kuondoa madai kwamba chama hicho hakina ufuasi magharibi mwa Uganda.

Uganda | Präsident Yoweri Museveni
Rais Yoweri MuseveniPicha: Luke Dray/Getty Images

Hapo awali, palikuwa na mashaka kama mkutano huo ungeruhusiwa kuendelea. Hii ni baada ya kituo cha redio cha Indijitto alichopangiwa kuwasiliana na watu kupitia hewani kuzimwa.

Soma zaidi:Mjadala waibuka kuhusu mageuzi ya katiba nchini Uganda

Aidha, polisi walizingira shule ambako mkutano huo ungefanyika na kuagiza watu wasikusanyike.

Lakini baada ya saa mbili hivi, masharti yalilegezwa na waandazi kuruhusiwa kuendelea na mkutano huo.

Bobi Wine alisisitiza kuwa si mapenzi ya Museveni kukubali mkutano huo kufanyika lakini ni kutokana na shinikizo la watu ndani na nje ya nchi ndipo sasa hana budi kuwaacha waendelee kuwahamasisha wananchi.

Harakati kuelekea 2026

"Hatuko hapa kwa mapenzi ya Museveni. Hakutaka tuwe hapa kuwambia ukweli ndiyo maana redio ilizimwa. Lakini hongereni watu wa Mbarara kwa kutobabaishwa." Alisema.

GMF 2022 | Recording of Arts.21 | Bobi Wine
Mwanamuziki aliyegeukia siasa nchini Uganda, Bobi Wine.Picha: Björn Kietzmann/DW

Viongozi wa chama hicho waliwasifu sana polisi kwa kujidhibiti wenyewe na kuuacha mkutano huo kufanyika kwa amani.

Chama cha NUP kimetangaza kuwa kitaendesha mikutano hiyo kujiimarisha mashinani na kuondoa mashaka miongoni mwa wapiga kura kwamba kimefifia.

Chama hicho kingali kinapinga ushindi wa Rais Museveni mwaka 2021 ulioamuliwa na mahakama ya juu.

Imetayarishwa na Lubega Emmanuel/DW Kampala