1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Blinken aitaka ASEAN kuishinikiza Myanmar kukomesha vurugu

Sylvia Mwehozi
14 Julai 2021

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amewatolea wito mawaziri wenzake wa Jumuiya ya nchi za Kusini Mashariki mwa Asia ASEAN, kushinikiza juu ya kukomeshwa kwa vurugu nchini Myanmar

https://p.dw.com/p/3wTSN
Indonesien Präsident Jokowi ermutigt zur Beendigung der Gewalt in Myanmar
Picha: Präsidentenbüro von Indonesien

Katika mkutano na mawaziri wenzake wa mambo ya kigeni kutoka jumuiya ya ASEAN uliofanyika kwa njia ya video, Blinken amewataka viongozi wa Jumuiya hiyo kushinikiza kukomeshwa kwa machafuko, kuitaka Myanmar kurejea katika misingi ya demokrasia na kuachiwa huru kwa wafungwa wote wa kisiasa.

Aidha Blinken, ameitaka jumuiya ya ASEAN kuchukua hatua za haraka za kuutaka "utawala wa Myanmar kuwajibika" katika makubaliano yaliyofikiwa mwezi Aprili baina ya wakuu wa nchi wa jumuiya hiyo na kiongozi wa kijeshi wa Myanmar. Makubalino hayo yaliyokuwa na vipengele vitano, yalitaka kukomeshwa mara moja kwa machafuko na kuanza kwa mazungumzo baina ya pande zinazopingana kupitia usuluhishi wa wajumbe maalumu wa Jumuiya ya ASEAN.

Nchi wanachama wa ASEAN tayari walipendekeza majina ya wajumbe maalumu kutoka Thailand na Indonesia lakini hadi sasa hapajakuwa na maendeleo yoyote. Wawakilishi wawili wa Jumuiya hiyo waliosafri nchini Myanmar mwezi uliopita kwa lengo la kuonana na Suu Kyi na wafungwa wengine waliambulia patupu baada ya maombi yao kukataliwa.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken Picha: Manuel Balce Ceneta/REUTERS

Marekani na Umoja wa Ulaya zimekuwa ndio mpinzani mkubwa wa utawala wa kijeshi uliomuondoa madarakani kiongozi wa kiraia Aung San Suu Kyi mnamo mwezi Februari. Suu Kyi alikamatwa na kuwekwa kizuizini pamoja na viongozi waandamizi wa chama chake cha National League for Democracy, akiwemo rais Win Myint. Kiongozi huyo kwa hivi sasa yuko chini ya kizuizi cha nyumbani wakati akikabiliwa na mashtaka kadhaa ambayo yanaweza kumfanya afungwe kwa zaidi ya muongo mmoja.

Mapema mwezi huu Marekani ilitangaza vikwazo vipya dhidi ya watu 22 ambao wanahusiana na mapinduzi ya kijeshi na mashambulizi yaliyofuata dhidi ya harakati za kutetea demokrasia nchini humo. Wiki iliyopita, Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet alisema kuwa hali ya haki za binadamu nchini Myanmar imebadilika kutoka kuwa mgogoro wa kisiasa hadi "janga pana la haki za binadamu", akiongeza kuwa karibu watu 900 wameuawa na takribani 200,000 wamelazimika kuyakimbia makaazi kutokana na uvamizi wa jeshi.

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP nalo lilikadiria kwamba zaidi ya watu milioni 6 wanahitaji msaada wa haraka wa chakula. Mkutano huo pia umeelezea janga la virusi vya corona, wakati ambapo maambukizi yakizidi kuongezeka, hospitali kufurika sambamba na vyumba vya kuhifadhia maiti huku uchumi katika mataifa ya Asia ukiathirika zaidi.

Vyanzo: Ap/AFP