1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bassirou ziarani Mauritania, Gambia

Saumu Mwasimba
19 Aprili 2024

Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal anatarajiwa kuwasili Gambia akitokea Mauritania ikiwa ni ziara yake ya kwanza ya kiserikali nje ya Senegal tangu alipochaguliwa mwishoni mwa mwezi Machi.

https://p.dw.com/p/4ey27
Senegal Bassirou Diomaye Faye
Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal.Picha: Zohra Bensemra/REUTERS

Kwa mujibu wa ripoti katika ziara yake ya Alhamisi (Aprili 18) nchini Mauritania alipangiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Mohammed Ould Ghazouani, kabla ya mkutano ya wajumbe kutoka mataifa hayo mawili ya Magharibi mwa Afrika.

Senegal na Mauritania zinapakana katika eneo la pwani ya pamoja yenye utajiri wa gesi asilia kwenye mradi mkubwa wa nishati unaoendeshwa na kampuni ya nishati ya Uingereza ya BP.

Soma zaidi: Rais mpya wa Senegal kuanza na mageuzi ya kiuchumi

Senegal pia ina makubaliano ya uvuvi na Mauritania na kwa sehemu inaitegemea nchi hiyo kwa usambazaji wa samaki.

Rais huyo mpya wa Senegal aliingia madarakani kwa ahadi ya kufanya mageuzi makubwa ikiwemo katika mikataba ya uvuvi na nishati.