1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ansar Dine yatanga vita tena Mali

4 Januari 2013

Kundi la Kiislamu la Ansar Dine nchini Mali, limetangaza kusimamisha mpango wake wa kusitisha mapigano na serikali ya nchi hiyo, likiilaumu kwa kufanyia mzaha mazungumzo ya amani na kujiandaa na vita.

https://p.dw.com/p/17EHL
Wapiganaji wa kundi la Ansar Dine.
Wapiganaji wa kundi la Ansar Dine.Picha: REUTERS

Kundi la Ansar Dine ni moja ya makundi yenye silaha yanyodhibiti upande wa kaskazini mwa Mali tanfu kutokea kwa uasi mwezi Aprili mwaka uliyopita, ambao mataifa ya magharibi na ya kanda hiyo yanahofia unaweza kuweka mazingira salama kwa Waislamu wenye itikadi kali za dini kupanga mashambulizi ya kimataifa.

GettyImages 155662170 Wajumbe wa Ansar Dine waliyohudhuria mazungumzo ya amani mjini Ouagadougou Novemba 6, 2012.
Wajumbe wa Ansar Dine waliyohudhuria mazungumzo ya amani mjini Ouagadougou Novemba 6, 2012.Picha: AFP/Getty Images

Katika taarifa yake iliyotolewa tarehe 26 Disemba, kundi hilo lilisema kuwa halina njia nyingine isipokuwa kuondoa ahadi yake ya kusitisha uhasama, ambayo ilipiganiwa na wapatanishi, lakini inafanyiwa mzaha na Wamali. Serikali ya Mali, Ansar Dine na kundi linalopigania kujitenga la watu wa kabila la Tuareg MNLA, walikubaliana kusitisha uhasama wakati wa mazungumzo ya amani yaliyoandaliwa na mpatanishi wa kanda hiyo, nchi ya Burkina Faso Disemba 5.

MUJWA waendelea na mapigani

Kundi la Kiislamu la MUJWA, ambalo linaonekana kuwa na uhusiano wa karibu na kundi la kigaidi la Al-Qaeda katika magharibi, AQIM lilitengwa katika mazungumzo hayo na limeendelea kupigana. Hata hivyo, juhudi za kidiplomasia za kuweka amani kati ya Ansar Dine na MNLA zilikuja wakati wa maandalizi ya kupeleka jeshi la kimataifa nchi humo kuisaidia serikali kurejesha sehemu ya kaskazini kutoka kwa waasi.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Disemba 20 liliidhinisha uingiliaji kijeshi nchini Mali, na pia liliruhusu umoja wa Ulaya na na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa kusaidia kutoa mafunzo kwa jeshi la Mali katika maandalizi ya vita dhidi ya waasi. Lakini hakutarajiwi kuwapo na operesheni ya kijeshi hadi mwishoni mwa mwaka huu. Kundi la Ansar Dine lilisema katika taarifa yake kuwa halijaona nia ya kweli ya amani kutoka kwa serikali ya Mali na badala yake, wakati wajumbe wa kundi hilo wakiwa (mji mkuu wa Burkina Faso) Ouagadougou, serikali ya Mali ilikuwa inaendelea kujipanga kwa ajili ya vita.

GettyImages 155662354 Rais wa Burkina Faso Blaise Compaore (kati kati) akikutana na wajumbe wa Ansar Dine mjini Ougadougou tarehe 6 Novemba 2012.
Rais wa Burkina Faso Blaise Compaore (kati kati) akikutana na wajumbe wa Ansar Dine mjini Ougadougou tarehe 6 Novemba 2012.Picha: AFP/Getty Images

Ansari Dine na uharibifu wa turaathi za kidini

Waasi wa Kiislamu wameharibu nyingi ya turaathi za kidini kaskazini mwa Mali, na kuwakata watu kadhaa viungo katika utekelezaji wa sheria za kiislamu, Shariah dhidi ya wakaazi wa maeneo hayo, ambao wamekuwa wakitekeleza Uislamu wa wastani kwa karne kadhaa. Karibu watu 400.000 wameyakimbia makaazi yao mwaka huu.

Uasi huo ulianzishwa na kundi linalopigania kujitenga la watu wa kabila la Tuareg, lakini ukandaniwa na makundi yaliyojipanga vizuri na yaliyo na zana nzuri za kivita yanayodaiwa kufadhiliwa na makundi yeyne itikadi kali za Kiislamu na wapiganaji wa Al-Qaeda katika eneo la Sahara. Pamoja na kuondoa ahadi yake ya kusitisha mapigano, Ansar Dine imesema bado ina dhamira ya kufanya mazungumzo na serikali mjini Bamako.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre,ap
Mhariri: Josephat Nyiro Charo.