1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini na kombe la dunia 2010

11 Juni 2009

Heba ya Afrika itategemea jinsi Kombe hilo litavyoandaliwa.

https://p.dw.com/p/I7Xa

Kombe la Dunia la dimba 2010 nchini Afrika Kusini, litakuwa mashindano makubwa kabisa ya kimichezo kuwahi kufanyika barani Afrika. Kwahivyo, mustakbala wa heba ya Afrika na nafasi yake ya kuandaa mashindano mengine zaidi kama hayo mfano wa olimpik pamoja na raslimali kubwa zinazofuatana na mradi kama huo,utategemea jinsi Kombe hili litakavyoandaliwa.

Uchumi wa mwenyeji wa kombe hili-Afrika kusini ,unadorora i- kwa mara ya kwanza tangu kupita miaka 17 na inaongozwa sasa na rais mpya Jacob Zuma ambae hajulikani wazi ana dira gani ya kuiongoza nchi hii.

Mashindano yoyote ya Olimpik au kombe la dimba la Dunia (FIFA World CUP), yana umuhimu mkubwa wa kujenga au kuibomoa heba ya nchi mwenyeji.Huchangia mno kupitia ujenzi wa miundombinu kunyanyua uchumi wa nchi na maendeleo yake .kwahivyo, Ikiandaa Kombe la kwanza la dunia barani Afrika,Afrika Kusini inaelewa inabebea mabegani mwake jukumu kwa Afrika nzima,kwani hatima ya Afrika kutunukiwa nafasi za kuandaa mashindano zaidi ya kilimwengu itategemea vipi Afrika kusini imeandaa Kombe hili la dunia,litakaloanza wiki hii,mwakani na likitanguliwa na Kombe la mashirikisho litakaloifungulia pazia jumapili hii huko Johannesberg.

Waandazi wa Kombe la dunia huko afrika kusini wamesema kwahivyo, litakuwa Kombe la dunia la aina ya kipekee na lisilosahaulika na litakalobadilisha kabisa dhana za walimwengu juu ya uwezo wa waafrika kuandaa mashindano kama hayo.

Hivyo ndivyo alivyoahidi Rais Jacob Zuma alipotawazwa kitini rais mpya mwezi uliopita.

Wakati kombe la mashirikisho-confederations Cup laanza jumapili hii,Juni 14 hadi finali,juni 28, firimbi ya kuanzisha Kombe la dunia mwakani italia Juni 11.Kwahivyo, kila kitu kitategemea jinsi kombe linaloanza jumapili hii la mashirikisho linaenda bila matatizo au misukosuko.

Maandalio ya Afrika kusini ya kombe hilo la dunia, yaliwahi kukumbwa na misukosuko kamavile ya migomo ya wafanyakazi,kukawia kukamilishiwa viwanja vipya na vile vinavyofanyiwa ukarabati n a hata mivutano ya kisiasa.Kulienea hata uvumi kuwa FIFA-shirikisho la kabumbu ulimwenguni lilikuwa na mpango B wa akiba kibindoni,endapo Afrika kusini ikiteleza.

Hivi punde lakini, Afrika kusini imekuwa ikipongezwa kwa maendeleo iliopiga katika maandalio ya Kombe la dunia.Katibu-mkuu wa FIFA Jerome Valcke amesema majuzi kuwa viwanja 9 kati ya 10 -nusu vikiwa vipya kabisa,vitakamilika ujenzi wake desemba mwaka huu na kiwanja cha mwisho kile cha Cape Town,kitakamilika Februari,mwakani.

Akaarifu kwamba FIFA yaamini mashabiki 450.000 wa kigeni watakwenda afrika kusini kujionea kombe la dunia na tijeti zimeanza kuuzwa kwa wingi.Mechi 28 kati ya zote 64 tiketi zake zimeshamalizika kuuzwa.Bw.Danny Jordaan,mwenyekiti wa Kamati ya maandalio ya Kombe la Dunia wa Afrika Kusini,ameondoa hofu za wale wanaohofia uhalifu utawarudisha nyuma mashabiki wa nje kwenda kuangalia Kombe la dunia.Ametaja kuandaa kwa Afrika kusini bila fujo kwa kombe la dunia la rugby na majuzi lile la Cricket na hata mashindano ya crickedt ya Ligi kuu ya india ,ni ushahidi wa hayo.

Ikiwa kuna hofu basi ni zile za kufanya vibaya tangu katika Kombe la wiki ijayo la mashirikisho na baadae mwakani la dunia kwa timu ya nyumbani Bafana bafana.Kwani, wenyeji hao wameshindwa hata kukata tiketi ya Kombe la Afrika la mataifa likaloaniwa upande wapili wa mpaka angola,mapema mwakani.

Kwa ufupi, bila kujali ni matatizo gani yataikumba Afrika Kusini,Kombe lijalo la dunia, limeshainufaisha Afrika kusini: Ujenzi wa barabara,njia za reli na viwanja vya dimba umestawi.FIFA nayo inayovuna fedha zake nyingi kutoka kombe la dunia,tayari inacheka kwa furaha:FIFA yatumai kuvunja rekodi kwa mavuno ya fedha kutoka kombe hili la 2010:Makadirio ya mtandao wa Sportcal.com yaasema FIFA imeshatia mfukoni dala bilioni 3.4.Kima hicho ni 50% zaidi kuliko katika kombe lililopita 2006, Ujerumani.

Mwandishi : Ramadhan Ali/RTRE

Mhariri:M.Abdul-Rahman