1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Angela Mdungu Mhariri: Mohammed Khelef
3 Mei 2024

Miongoni mwa masuala ya Afrika yaliyopewa umuhimu na magazeti ya Ujerumani wiki hii ni pamoja na maafa yaliyosababishwa na mvua kubwa Afrika ya Mashariki.

https://p.dw.com/p/4fTdy
Magazeti ya Ujerumani
Magazeti ya UjerumaniPicha: Jan Woitas/dpa/picture alliance

die tageszeitung

die tageszeitung liliarifu, mvua kubwa na mafuriko yamesababisha vifo vya watu wengi hasa Kenya na Tanzania. Mvua hizo zilisababisha mito na maziwa kufurika na hata mabwawa kupasuka.

Kwa mujibu wa maafisa, nchini Kenya pekee, watu 169 wamefariki dunia kutokana na mafuriko. Wengine zaidi ya 100 wamelazwa hospitalini. Katika mji mkuu Nairobi, watu 10,000 walibaki bila makazi hasa katika maeneo yenye mifumo duni ya maji taka.

Wana jiolojia wa Kenya wamekuwa wakiikosoa serikali kuwa haichukui hatua za kuzuia maafa katika kutambua mapema majanga ya aina hii ili kuzuia vifo vya raia. Kulingana na die tageszeitung, nchini Tanzania nako, watu 155 wamekufa kutokan na mafuriko na maporomoko ya ardhi. Kulingana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, zaidi ya nyumba 50,000 zimeharibiwa na zaidi ya watu 200,000 hawana makazi kutokana na maafa hayo.

Frankfuter Allgemeine

Frankfuter Allgemeine wiki hii liliandika juu ya sababu za bara la Afrika kuendelea kuwa dhaifu kiuchumi licha ya kuwa na rasilimali nyingi. Gazeti hilo linabainisha kuwa, wakati idadi ya watu katika mataifa ya magharibi na nchi zenye ustawi wa viwanda ikizidi kupungua huku watu wengi wakielekea kuzeeka, bara la Afrika linaonesha picha tofauti. Kwa sasa kuna takribani watu bilioni 1.5.  Kufikia mwaka 2050, wanademografia wanatarajia idadi ya watu barani humo itafikia bilioni 2.5. Bara hilo si tu kuwa linakua kwa kasi bali pia lina vijana wengi .

Vijana ndiyo wateja muhimu na wafanyakazi nyumbani na hata nje ya nchi zao. Hata hivyo vijana hawa hawana kazi, wakati Ujerumani na Ulaya zina upungufu na zinatafuta wafanyakazi wenye ujuzi.

Frankfuter Allgemeine linaendelea kuandika kuwa, moja ya sababu ya udhaifu wa Uchumi katika mataifa ya Afrika  ni uhaba wa wawekezaji wa ndani na nje ya bara hilo. Limetaja pia baadhi ya vikwazo kwa wajasiriamali  barani humo kuwa ni miundombinu dhaifu hasa barabara na tatizo la umeme.

die tageszeitung

Mwanzoni mwa juma, die tageszeitung  liliiutupia jicho uchaguzi wa bunge wa Togo.  Linaeleza kuwa, barani Afrika hakuna tena utawala wa kurithishana madaraka kifamilia, lakini familia inayotawala Togo  bado inaendeleza utamaduni huo. Kwa zaidi ya miaka 60 taifa hilo ambalo ni koloni la zamani la Ujerumani linaongozwa na familia moja.

Mtawala wa kwanza wa kijeshi Gnassingbé Eyadema, alishika Madaraka mwaka 1967. Tangu mwaka 2005, baada ya kifo chake, mwanaye anaiongoza nchi hiyo. Gnassingbé  mwenye miaka 57 sasa anatumikia muhula wake wanne madarakani. Uchaguzi wa wabunge unafanyika na hili ni tukio muhimu.

Faure Gnassingbé
Rais wa Togo Faure GnassingbéPicha: Gbemiga Olamikan/AP Photo/picture alliance

Hii ni kwa saabu ya mageuzi ya yaliyopitishwa kwa kauli moja na bunge la Togo Aprili 19 na kusababisha mgawanyiko mkubwa. Wabunge nchini humo walipiga kura iliyoidhinisha kuwepo kwa nafasi inayofanana na ya waziri mkuu. Wanasiasa wa upinzani wanalalamika kuwa, nafasi hiyo imeundwa ili kumsaidia Rais Gnassingbe kuepukana na ukomo wa kukaa madarakani.

Rais huyo wa Togo ameshashinda katika chaguzi nne ambazo zote zilipingwa na vyama vya upinzani kutokana na kile walichokiita kuwa ni dosari. Kulingana na katiba ya awali, Gnassingbe angeweza kugombea urais mwaka 2025 pekee katika muhula mmoja uliosalia.

Welt Plus

Kwa upande wake gazeti la Welt Plus limeandika, siku chache baada ya bunge la Uingereza kuidhinisha sheria ya kuwapeleka wahamiaji Rwanda, muomba hifadhi wa kwanza kutoka Uingereza alipanda ndege kuelekea Kigali. Hakupelekwa katika taifa hilo la Afrika ya Mashariki kwa sababu ya sheria hiyo mpya, bali chini ya programu maalumu ya wahamiaji kuchagua kuondoka London kwa hiyari. Licha ya hilo makubaliano ya Uingereza na Rwanda tayari yameanza kusababisha hofu miongoni mwa wahamiaji

Muda mfupi ujao, London itaanza msako na kuwasafirisha kwa nguvu wahamiaji walioingia nchini humo kinyume cha sheria  ikiwa hawataondoka kwa hiyari yao. Katika taifa jirani la Ireland ambalo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya tayari athari za hatua hii zimeanza kuonekana. Siku chache zilizopita gazeti la kila siku la The Times liliripoti uwepo wa waomba hifadhi mjini Dublin ambao kwa kuhofia kupelekwa Rwanda walikimbia wakitokea Uingereza. Wiki iliyopita waziri wa haki wa Ireland Helen Mc Entee alilieleza bunge la nchi hiyo kuwa, zaidi ya asilimia 80 ya wakimbizi walishaingia Ireland kupitia mpaka wa Ireland Kaskazini.

Welt online

Welt online, liliiangazia kuhusu ripoti ya mauaji ya halaiki huko Burkina Faso iliyosababisha kusimamishwa kwa matangazo ya redio za kimataifa. Mhariri wa gazeti hili ameandika, shirika la haki za binadamu la Human rights watch liliandika ripoti kuhusu mauaji ya raia katika taifa hilo. Katika mauaji hayo wanajeshi wanadaiwa kuwa waliwauwa raia 223. Mara baada ya vyombo vya habari vya kimataifa kuanza kuimulika taarifa hiyo, serikali iliingilia kati. Kilichofuata ni kuwa, vituo viwili maarufu vya redio vilifungwa kwa muda wa wiki mbili.

Hatua hiyo ilitangazwa na msemaji wa serikali ya Burkina Faso Tonssira Myrian na kuvitahadharisha vyombo vya habari kuacha kuripoti taarifa zinazotolewa na shirika hilo la kutetea haki za binadamu la Human Rights watch. Shirika hilo lililituhumu jeshi la Burkina Faso kwa kufanya mauaji hayo kwenye vijiji viwili. Kati ya watu 223 waliouwawa, 56 ni watoto. Raia hao waliuwawa kwa madai kuwa walikuwa wakishirikiana na makundi ya itikadi kali.