1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shutuma za Mauaji ya Kikabila Sudan Kusini

22 Aprili 2014

Umoja wa Mataifa umesema wapiganaji wa waasi nchini Sudan Kusini waliwaua mamia ya raia kwa misingi ya kikabila walipouteka mji wa Bentiu na kutaka uchunguzi kuanzishwa kuhusu mauaji hayo

https://p.dw.com/p/1Blv6
Wapiganaji wa waasi wanaoshutumiwa kufanya mauaji ya kikabila
Wapiganaji wa waasi wanaoshutumiwa kufanya mauaji ya kikabilaPicha: AFP/Getty Images

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan kusini umesema zaidi ya watu mia mbili waliuawa katika msikiti mmoja mjini Bentiu na wengine zaidi ya mia nne wamejeruhiwa huku wengine wakiuawa pia katika kanisa,hospitali na kambi ya shirika la umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP.

Afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini Tony Lanzer amesema kile alichokishuhudia baada ya kuuzuru mji wa Bentiu ni jambo baya sana na la kusikitisha kwani miili ya raia imerundikana barabarani, sokoni na katika maeneo ya kuabudu.

Umoja wa Mataifa umesema waasi walisikika katika redio moja nchini humo wakiwataka wanaume wa kabila la Nuer kuwabaka wanawake wa kutoka kabila hasimu la Dinka na kuwafurusha watu hao kutoka mji wa Bentiu.

Waasi wawalenga raia wa kabila hasimu

Wanajeshi wa serikali ya Rais Salva Kiir ambaye anatokea kabila la Dinka wamekuwa wakikabiliana na waasi watiifu kwa aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar ambaye ni wa kabila la Nuer katika siku za hivi karibuni na waasi hao wamefanikiwa kuuteka mji muhimu kwenye sekta ya mafuta Jumanne wiki iliyopita kutoka mikononi mwa wanajeshi hao.

Raia wa Sudan Kusini wanaokimbia mapigano
Raia wa Sudan Kusini wanaokimbia mapiganoPicha: Reuters

Muda mfupi baada ya waasi kuuteka mji wa Bentiu msemaji wa waasi Lul Ruai Koang aliwasifu wapiganaji hao kwa kile alichokitaja zoezi la kuutakasa mji huo.

Wachunguzi wa umoja wa Mataifa wamesema baada ya kuuteka mji huo,waasi hao kwa siku mbili mfululizo walianza kuwasaka watu wa kabila hasimu na kuwaua.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amelaani mauaji hayo yanayolenga kabila moja na raia wa Sudan kutoka jimbo la Darfur na kutaka uchunguzi kamili kuanzishwa nchini humo ili kuwakamata wahusika na viongozi wao.

Pande zote zatakiwa kuwalinda raia

Dujarric amezitaka pande zote mbili zinazo zozana kukumbuka kuwa zinao wajibu wa kuwalinda raia na kuzitaka pande hizo kukoma kuwalenga raia na kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Januari.

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan KusiniPicha: AFP/Getty Images

Waziri wa mambo ya nje wa Sudan Kusini Barnaba Marial Benjamin ameahidi kuwa serikali itaanzisha uchunguzi na kuwakamata waliohusika.Hata hivyo Machar amekanusha kuhusika kwa wapiganajai wake na mauaji hayo ya mji wa Bentiu.

Wanajeshi wa kulinda amani wamewaokoa kiasi ya raia 500 wengi wao wakiwa na majeraha na kuwapa ulinzi maelfu wengine waliokimbilia katika kambi ya umoja wa Mataifa ambapo inawahifadhi zaidi ya watu 22,000 wanaoishi katika hali mbaya kutokana na msongamano mkubwa ulioko katika kambi hiyo.

Kudhibitiwa kwa mji wa Bentiu na waasi kulikuja siku mbili kabla ya watu waliokuwa na silaha kuishambulia kambi ya umoja wa Mataifa mjini humo na kuwaua watu 58.

Baraza la usalama la umoja wa Mataifa limesema shambulizi hilo huenda likazingatiwa kama uhalifu wa kivita.Kuongezeka kwa mashambulizi Sudan Kusini kunakuja huku katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akionya kuwa zaidi ya watu milioni moja nchini humo wanakabiliwa na janga la njaa.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Gakuba Daniel