1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Kenyatta atia saini mswada dhidi ya Ugaidi

20 Desemba 2014

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametia saini kuwa sheria mswada wenye utata wenye lengo la kupambana na ugaidi na kusababisha wabunge kutupiana ngumi bungeni na kuzusha madai kuwa unakiuka misingi ya uhuru

https://p.dw.com/p/1E7sW
Kenia Präsident Uhuru Kenyatta in Nairobi
Rais Uhuru KenyattaPicha: Reuters/T. Mukoya

Kenyatta amesema ameridhishwa kwamba mswada huo umepitishwa na bunge la taifa siku ya Alhamis na haukiuki katiba ya nchi hiyo. "Wasi wasi wote uliooneshwa na wadau tofauti umeshughulikiwa na kamati zinazohusika za bunge," amewaambia waandishi habari, na kuwataka Wakenya wote kusoma sheria hiyo mpya na kuamua wao binafsi.

Madaraka makubwa

"Lengo lake ni moja - moja tu- kulinda maisha na mali za raia wote wa jamhuri ya Kenya," amesema rais Kenyatta.

Nairobi Kenia Abgeordnete Parlament Debatte Sicherheitsgesetz 18.12.2014
Wabunge wakitoka katika ukumbi wa bunge baada ya vuruguPicha: Reuters/T. Mukoya

Sheria hiyo mpya inatoa kwa maafisa wa madaraka makubwa kuwasaka watuhumiwa wa ugaidi na kuweka mipaka kwa uhuru wa vyombo vya habari katika nchi ambayo tayari imeathirika na wimbi la mashambulio yanayofanywa na kundi la al-Shabaab kutoka nchi Somalia lenye mafungamano na kundi la kigaidi la al-Qaeda.

Hatua hizo zenye utata zinaongeza muda wa polisi kuwashikilia watuhumiwa wa ugaidi kutoka siku 90 za sasa hadi karibu mwaka mmoja na kuongeza hukumu inayowakabili.

Waandishi habari wanalengwa

Wakati huo huo , waandishi habari wanaweza kukabiliwa na hukumu ya hadi kifungo cha miaka mitatu iwapo ripoti zao zitaingilia uchunguzi ama operesheni za usalama zinazohusika na ugaidi", ama iwapo watachapisha picha za wahanga wa ugaidi bila ya ruhusa ya polisi.

Nairobi Kenia Abgeordnete Parlament Debatte Sicherheitsgesetz 18.12.2014
Ulinzi mkali mjini Nairobi wakati bunge likijadili mswada wa sheria ya usalamaPicha: Reuters/T. Mukoya

Serikali inadai kuwa hatua hizo ni muhimu kuweza kupambana na wanamgambo na inasema mabadiliko ya katiba ya msingi, na kutoa kwa mahakama nafasi kubwa zaidi kwa polisi na idara za usalama, ni sahihi kikatiba.

Wapinzani wanapinga

Upinzani na makundi ya haki za binadamu , hata hivyo, wanakataa mabadiliko hayo na kusema ni kisingizio na wanadai sheria hiyo inahatarisha kuigeuza Kenya kuwa taifa la kipolisi.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Jen Psaki amesema Marekani "inaiunga mkono kwa dhati Kenya katika juhudi zake za kulishinda kundi la al-Shabaab na kuhakikisha usalama wa raia zake.

Nairobi Kenia Abgeordnete Parlament Debatte Sicherheitsgesetz 18.12.2014
Wanajeshi wa kupambana na ghasia walitanda mjini NairobiPicha: picture-alliance/AP Photo/Ben Curtis

Hata hivyo , licha ya kuwa sheria hizo "zimelenga kuongeza uwezo wa Kenya kuzuwia na kuwashinda magaidi," Psaki amesema, "tunakatishwa tamaa kwamba sheria hiyo muhimu haikupewa muda wa kutosha kwa ajili ya kuijadili kwa kina."

"Tunaitaka serikali ya Kenya kuhakikisha kwamba juhudi zake za kupambana na ugaidi zinaheshimu haki za Wakenya wote na kuheshimu katiba na utawala wa sheria," Psaki amesema.

Nairobi Kenia Abgeordnete Parlament Debatte Sicherheitsgesetz 18.12.2014
Wabunge wakitoka katika jengo la bunge mjini NairobiPicha: Reuters/T. Mukoya

Mgawanyiko kuhusu sheria hizo umezusha vurugu bungeni siku ya Alhamis. Wabunge wa upinzani walichana nakala za mswada huo na kurushiana makonde na wale wanaounga mkono mswada huo, na kulazimisha kura hiyo kucheleweshwa mara kwa mara.

Kenyatta ameshutumu hali hiyo na kusema, ni ya " kusikitisha" na kuwashutumu wapinzani kwa kutotambua kitisho kinachoikabili nchi hiyo kwa wakati huu.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Amina Abubakar