1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Platini abakia na changamoto moja ya mwisho

27 Machi 2015

Michel Platini ameliweka jicho lake kwenye changamoto moja ya mwisho katika mwaka wa 2019, mwaka ambao FIFA itamchagua rais wake. Atalenga kuwa mrithi wa Sepp Blatter katika FIFA

https://p.dw.com/p/1EyfL
Österreich Michel Platini beim UEFA-Kongress in Wien
Picha: Reuters/L. Foeger

Baada ya kupewa miaka mingine minne ya uongozi wa Shirikisho la Kandanda Ulaya, Platini alidokeza kuwa hatogombea tena muhula mwingine wa UEFA. Mfaransa huyo atakayefikisha umri wa miaka 60 mwezi Juni, baadaye aliwaambia waandishi wa habari kuwa amesalia tu na kazi moja ya kufanya katika taaluma yake

Michael van Praag
Michael van PraagPicha: Getty Images/D. Mouhtaropoulos

Alionekana kwa muda mrefu kama rais ajaye wa FIFA hadi Sepp Blatter alipoibatilisha ahadi yake ya mwaka wa 2011 ya kuondoka mwezi Mei. Badala yake, Blatter mwenye umri wa miaka 79 anapigiwa upatu kushinda muhula wa tano dhidi ya wapinzani wake watatu wanaoungwa mkono na UEFA.

Blatter mapema wiki hii alikabiliwa na shutuma kali wakati alialikwa katika mkutano mkuu wa UEFA mjini Vienna, kutoka kwa wapinzani wake wa wadhifa wa urais wa FIFA.

UEFA imesema haitamuunga mkono Blatter wakati akiwania muhula wa tano mnamo Mei 29, ambapo atashindana na Luis Figo, Michael van Praag na Prince Ali Bin Al Hussein. Platini alisema hana ubaya wowote na kazi ya FIFA "Mashirikisho yote ya kitaifa ulimwenguni yanapenda FIFA. Kwa sababu FIFA ni makao ya kandanda. Iliundwa mwaka wa 1904 na UEFA ikaanzishwa 1955. Na sote tunapenda FIFA. Mashirikisho yote ya kitaifa yanaipenda FIFA, lakini hayaridhishwi na uendeshwaji wa FIFA na wameonyesha masikitiko yao. Lakini sote tunaipenda FIFA kwa sababu FIFA ni makao yetu, makao ya kila mmoja, shirikisho la kandanda ulimwenguni.

London Kandidat FIFA Präsidentschaft Ali bin Al-Hussein
Prince Ali Bin Al HusseinPicha: picture-alliance/dpa/A. Rain

Van Praag alizungumza sana akisema kuna wajibu wa kuusafisha uchafu uliopo katika uongozi wa FIFA. Alisema "Nahisi haja ya kuimarisha FIFA, kwa sababu baada ya maisha yenye majukumu mengi ya kandanda, kamwe siwezi kukubali tuiache FIFA katika hali yake ya sasa kwa ajili ya kizazi kijacho. Utamaduni mzuri wa kandanda la kimataifa umechafuliwa na shutuma za ufisadi, hongo na mapendeleo na kupoteza fedha. Usinichukulie vibaya, FIFA imefanya mengi mazuri lakini hali ya sasa ya mparaganyiko inahitaji mabadiliko ya uongozi".

Na wakati Prince Ali alisimama kuhutubia, alisisitiza kuwa mabadiliko ya uongozi hayaepukiki akiongeza kuwa kama atachaguliwa kuwa rais wa FIFA atautanua mchezo wa kandanda katika soko la ulimwengu "Mafanikio ya sasa ya kibiashara pamoja na fedha za kupindukia kutoka kwenye hazina zetu vinaweza kuungana na kuunda mfumo bora tunaohitaji kwa ajili ya mipango ya maendeleo ya FIFA. Lengo linapaswa kuwa ni kuutanua mchezo katika masoko na mipaka mipya, na kuzipa nchi zaidi nafasi za kutoa vipaji vipya na kupata mafanikio katika kiwango cha kimataifa, kwa kandanda ya wanaume na wanawake. Na kuyaruhusu mashirikisho wanachama kudhamiria kuandaa vinyang'anyiro hivi na kupokea uugwaji mkono unaofaa".

FIFA-Präsidentschaft Luis Figo Pressekonferenz
Luis FigoPicha: picture-alliance/dpa

Mgombea wa tatu Luis Figo alizungumzia zaidi mipango yake ya kuimarisha kandanda la mashinani na lengo la kukuza vipaji vya chipukizi kote ulimwenguni: Alisema "FIFA haipaswi kumtegemea rais. Hiyo haifai katika kampuni yoyote au shirika lolote. Hivyo nini kinakosekana? Kinachokosekana katika FIFA ni wewe. Kila rais katika kila shirika ulimwenguni anaoa hilo. Nyote mnahitaji kuwepo katika maisha ya FIFA. Tukiwa pamoja, kazi hii na fililosofia hii mpya ya usimamizi wa FIFA itakuwa ngumu zaidi, na tutaendesha mchezo huu tunaoupenda kwa kuwa na ufahamu wa faida ya wachezaji, makocha, waamuzi, mashabiki na bila shaka watoto ambao wanapenda kandanda".

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu