1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria iko tayari kuzungunza na Boko Haram

14 Mei 2014

Nigeria imesema ipo tayari kufanya mazungumzo na kundi la waasi wa kiislamu wenye itikadi kali Boko Haram ili iwaachie huru wasichana zaidi ya 200 iliyowateka nyara katika kijiji cha Chibok

https://p.dw.com/p/1BzV9
Boko Haram Video 12.5.2014
Picha: picture alliance/abaca

Waziri anayeshughulika na masuala maalumu katika serikali ya Nigeria Taminu Turaki amesema milango ya majadiliano na kundi hilo la kigaidi ambalo limekuwa likifanya matukio ya umwagaji damu ipo wazi.

"Tupo tayari kufanya mazungumzo katika suala lolote ikiwa ni pamoja na hili la wasichana waliotekwa wa Chibok, kwa sababu kwa sasa hatuwezi kusema hili sio suala litakalazungumziwa" alisema Turaki ambaye mwaka jana aliiongoza kamati iliyokuwa inashawishi kufanyika makubaliano ya kupatiwa msamaha wa baadhi ya wafungwa wanachama wa kundi hilo.

Kauli hiyo ya waziri huyo inakuja siku chache baada ya waziri mwenzake ambaye anashughulika na masuala ya ndani ya nchi hiyo Abba Moro kupinga takwa la Boko Haram la kutaka wanachama wake waliofungwa waachiwe huru ndipo nao watakapo waachia wasichana hao waliowateka.

Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau
Kiongozi wa Boko Haram Abubakar ShekauPicha: picture alliance/AP Photo

Nae Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan ameomba kuongezwa kwa miezi sita muda wa hatari uliotangazwa katika jimbo la Borno pamoja na majimbo mengine mawili jirani ya jimbo hilo mwaka mmoja uliopita kutokana na hali ya usalama kuendelea kuwa tete katika maeneo hayo.

Wataalamu kutoka Marekani, Uingereza, Ufaransa, na Israeli wapo mjini Abuja kutoa msaada wa opereshini ya kuwaokoa wanafunzi hao huku pia China nayo ikiahidi kuisaidia serikali ya Nigeria. Taarifa zaidi kutoka Uingereza zinasema kuwa Afisa wa mambo ya nje wa nchi hiyo anayeshughulika na masuala ya Afrika Mark Simmonds anatarajia kuwasili hii leo Abuja ili kujadiliana na serikali ya Nigeria kama nchi yake inaweza kutoa msaada zaidi katika operesheni hiyo.

Mmoja wa wataalamu wa jeshi la ardhini la Uingereza, Brigedia Ivan Jones, amesema wanashirikiana vizuri na wanigeria lakini amekiri suala la kuwatafuta wasichana nao ni gumu. Wakati jitihada hizo za uokozi zikiendelea, wazazi na walimu wa wanafunzi ambao wametekwa, wamewatambua wasichana 77 kati ya 130 walioonekana katika picha ya video iliyotolewa hivi karibuni wakiwa wamevaa hijabu nyeusi.

Wanajeshi wa Cameroon wakifanya doria katika ziwa Chad
Wanajeshi wa Cameroon wakifanya doria katika ziwa ChadPicha: PATRICK FORT/AFP/Getty Images

"wasichana waliopo katika picha ya video wametambuliwa kwa majina yao katika zoezi ambalo lilijumuisha wazazi wa wasichana hao, wanafunzi wenzao ambao miongoni mwao wapo waliofanikiwa kutoroka katika tukio hilo, walimu, watu wa usalama pamoja na maofisa wa serikali wa Borno" alisema Gavana wa Borno Kashim Shettima ambaye ameongeza kuwa zoezi la kuwatambua linaendelea wakati akiongea na waandishi wa habari. Boko Haram inawashikilia waanfunzi wa kike zaidi ya 200 iliyowateka April 14 wakiwa katika maandalizi ya mitihani katika shule yao iliyopo katika kijiji cha Chibok, kilichopo jimbo la Borno, kaskazini mwa nchi hiyo.

Mwandishi: Anuary Mkama/afpe, dpae,
Mhariri: Josephat Charo