1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu aishambulia Iran, Hamas na IS

30 Septemba 2014

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema katika Umoja wa Mataifa, kwamba Iran iliyo na silaha za nyuklia ni kitisho kikubwa kwa amani ya dunia kuliko kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

https://p.dw.com/p/1DNT3
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiuhutubia Umoja wa Mataifa
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiuhutubia Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/dpa/Justin Lane

Katika hotuba hiyo kali Netanyahu ameishambulia Iran, kundi la wanamgambo wa kipalestina la Hamas, bila kusahau baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, ambalo lilikosoa mwenendo wa nchi yake katika vita vya hivi karibuni katika Ukanda wa Gaza ambavyo viliuwa wapalestina zaidi ya 2000, wengi wa wahanga wakiwa raia.

Waziri mkuu huyo wa Israel amesema hakuna tofauti yoyote kati ya Hamas na Kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, akisema makundi hayo mawili ni matawi ya mti mmoja unaotoa sumu, akisisitiza azma yao ni moja, kuitawala dunia kwa kutumia ugaidi kama walivyofanya wanazi miongo sita iliyopita.

Ameonya kuhusu Iran akisema lengo la nchi hiyo katika mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia ni kuondolewa vikwazo, ili hatimaye ifikie azma yake kuu.

''Msihadaiwe na haiba bandia ya Iran. Lengo la taifa la kiislamu ni kuhakikisha inaondolewa vikwazo vinavyoikabili, na kuiacha ikiwa na uwezo wa kurutubisha madini ya Urani, na siku za usoni, kwa muda inaoutaka, Iran, nchi yenye serikali hatari zaidi ulimwenguni, katika kanda yenye hatari zaidi ulimwenguni, itakuwa na silaha hatari zaidi ulimwenguni.'' Amesema Netanyahu.

Rais wa Iran Hassan Rouhani ambaye Netanyahu amesema haiba yake ni hadaa tupu
Rais wa Iran Hassan Rouhani ambaye Netanyahu amesema haiba yake ni hadaa tupuPicha: Reuters

Hamas na IS tofauti kwa jina tu

Netanyahu pia amewashambulia viongozi wa dunia, ambao mmoja baada ya mwingine waliikosoa nchi yake kuhusu vita vya hivi karibuni kwenye Ukanda wa Gaza ambavyo vilikuwa na umwagaji mkubwa wa damu. Amesema viongozi hao hawajui kwamba ukiondoa tu tofauti ya majina, Hamas´ni Dola la Kiislamu, na Dola la Kiislamu ni Hamas.

Shutuma za Netanyahu hazikuuacha nyuma Umoja wa Mataifa, hasa Baraza lake la Haki za Binadamu. Netanyahu amesema baraza hilo huilenga tu Israel kwa ukiukaji wa haki za binadamu, huku likizifumbia macho pande nyingine zinazofanya uhalifu. Kiongozi huyo amekwenda mbali na kuliita baraza hilo Kundi la kutetea magaidi.

Hotuba yenye kupinda ukweli

Akizungumzia hotuba hiyo ya Netanyahu, Hanah Ashrawi ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya chama cha PLO cha Paalestina, amesema hotuba hiyo iliupinda ukweli wa mambo, kwa lengo la kuwahadaa viongozi wa dunia.

Naye mjumbe wa Palestina katika mazungumzo ya amani na Israel Saeb Erakat, amesema hotuba ya Netanyahu imezika uwezekano wa kupatikana kwa suluhu la mataifa mawili kwa misingi ya mipaka ya kabla ya vita vya mwaka 1967.

Viongozi wengi wa Dunia waliikosoa Israel kwa vita vyake dhidi ya Ukanda wa Gaza
Viongozi wengi wa Dunia waliikosoa Israel kwa vita vyake dhidi ya Ukanda wa GazaPicha: DW/T. Krämer

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani Jen Psaki pia ameonyesha tofauti ya nchi yake na Netanyahu kuhusu kuzilinganisha Hamas na IS, akisema kuwa ingawa makundi hayo mawili yanachukuliwa na Marekani kuwa ya kigaidi, IS inatoa kitisho cha aina ya pekee kwa usalama wa Marekani.

Mwanadiplomasia wa Iran katika Umoja wa Mataifa Javad Safaei, amesema hotuba ya Netanyahu ililenga kufunika maovu yanayotendwa na serikali yake dhidi ya raia.

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman