1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo ya Jumuiya ya madola, mataifa ya Afrika yaanza kupata medali

28 Julai 2014

Michezo ya jumuiya ya madola mjini Glasgow yaingia siku ya tano, medali 27 kuwaniwa hii leo, lakini jana ilikuwa siku ya firaha kwa mataifa ya Afrika .

https://p.dw.com/p/1Cklj
Indien Olympia 2012 - Soniya Chanu Ngangbam
Wachezaji katika michezo ya Jumuiya ya madolaPicha: dapd

Wanariadha wamekuwa wakiwania medali nyingine 27 katika siku ya tano ya michezo ya jumuiya ya madola ya mwaka huu wa 2014 leo(28.07.2014) mjini Glasgow. Fainali ya wanaume na wanawake katika mita 100 itafanyika katika uwanja wa Hampden Park , wakati medali ya kwanza ya dhahabu katika mchezo wa badminton, kwa wachezaji mchanganyiko , pamoja na squash , kwa wanaume na wanawake, pia zitawaniwa.

Uingereza na Singapore zilitarajiwa kupambana katika tuzo ya juu kwa mchezo wa mpira wa meza kwa wanaume , wakati medali nyingine nane za dhahabu zitapatikana katika kuogelea, ambapo mchezo muhimu utakuwa fainali ya mtindo wa freestyle wanawake katika kuogelea.

Glasgow 2014 Commonwealth Games
Mbio za baisikeli ndani ya ukumbiPicha: Getty Images

Mchezo wa rugby umepata msukumo mkubwa kabla ya matarajio yake ya kujumuishwa katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 2016 mjini Rio de Janeiro wakati ulipotoa burudani safi kwa mashabiki wanaomiminika katika michezo hiyo ya jumuiya ya madola mjini Glasgow. Hofu yoyote kwamba mchezo huo hautapata mashabiki katika mji mkuu wa Scotland ambao ni maarufu kwa mashabiki wake wanaopendelea sana kandanda zilifutika wakati mashabiki 171,000 waliposheheni katika uwanja wa Ibrox kushuhudia michezo hiyo kwa muda wa siku mbili mfululizo.

Afrika kusini imefikisha mwisho ubabe wa mabingwa New Zealand ambao wameshinda kombe la rugby mara nne katika michezo ya jumuiya ya madola na kufuta rekodi ya kutoshindwa katika michezo 30 na kunyakua medali ya dhahabu katika uwanja uliosheheni mashabiki wa Ibrox.

Die pakistanische Badmintonspielerin Palwasha Bashir
Mchezo wa badmintonPicha: DW/T.Saee

New Zealanda ambayo ubingwa wake ulianzia kupata medali ya dhahabu mjini Kuala Lumpur mwaka 1998, ilifunga mabao yake kupitia Sherwin Stowers na Joe Webber, na Gillies Kaka.

Na sasa kandanda.

Katika mchezo wa nne wa kombe la ligi ya mabingwa barani Afrika Champions League, jana Vita Club ya Kinshasa iliishinda El-Hilal ya Sudan kwa mabao 2-1 mjini Kinshasa, wakati Zamalek ya Misri iliambulia sare ya bila kufungana dhidi ya TP Mazembe ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo katika mchezo uliochezwa mjini Alexandria nchini Misri. Katika kundi B CS Sfaxien imepata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Esperance pia ya Tunisia , wakati Al-Ahly ya Benghazi nchini Libya ilipata kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Entente Setif ya Algeria.

Michezo inayofuata itafanyika Agosti 8 - 10 ambapo TP Mazembe itaikaribisha El-Hilal ya Sudan na Zamalek itakumbana na Vita Club ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo nchini Misri. Wakati Al-Ahly ya Benghazi Libya itakwaana na CS Sfaxien ya Tunisia , na Setif ya Algeria itaoneshana kazi na Esperance ya Tunisia.

Fußball Ägypten Verein Al Ahli
Wachezaji wa Al-Ahly ya MisriPicha: Reuters

Na katika kombe la shirikisho la kandanda barani Afrika Real Bamako ya Mali iliishitua AC Leopards ya Kongo kwa kuishinda kwa mabao 2-1 mjini Brazzaville mwishoni mwa juma na kuliacha kundi A kuwa halina mwenyewe.

Leopards ambayo iliishinda Djoliba ya Mali katika fainali ya mwaka 2012, ina points tano, ikifuatiwa na Real Bamako yenye points nne na mabingwa wa zamani wa Afrika ASEC Abidjan ina point mbili tu.

Katika michezo mingine ilikuwa kati ya Al-Ahly ya Misri ikaishinda Sewe San Pedro ya Cote D'Ivoire kwa bao 1-0 mjini Cairo katika kundi B na Nkana Red Devels ya Zambia iliishinda Etoile Sahel ya Tunisia kwa mabao 4-3 mjini Kitwe, Zambia.

Timu ya taifa ya Tanzania bara, Taifa Stars inawania kusonga mbele katika kinyang'anyiro cha kuwania kukata tikiti kwa ajili ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika mwakani wakati itakapochuana na Msumbiji, Black mambas tarehe 3 mwezi ujao wa Agost mjini Maputo.

Ubaguzi michezoni

Shirikisho la kandanda duniani FIFA leo limelitaka shirikisho la kandanda la Italia kufanya uchunguzi juu ya matamshi ya kibaguzi yaliyotolewa na mgombea wa kiti cha urais katika shirikisho hilo nchini Italia. Carlo Tavecchio , mwenye umri wa miaka 71 anaonekana kuwa huenda akachaguliwa kuwa rais wa shirikisho hilo lakini matamshi yake katika mjadala kuhusu wachezaji wa kigeni Ijumaa iliyopita yamesababisha hasira. Matamshi yake yamevuka mpaka ambapo amesema , "nchini Uingereza , wanatambua wachezaji wanaoingia ambapo ni wale wenye kiwango cha juu tu ndio wanacheza," Tavecchio amesema. Anaongeza , "kwetu sisi , badala yake tunapata "Opti Poba" ambao hapo zamani walikuwa wanakula ndizi na ghafla wanakuwa wachezaji wa timu ya kwanza ya Lazio.

FIFA imeongeza kuwa imelikumbusha shirikisho la kandanda la Italia kuwa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi yako katika umuhimu wa juu."

WM 2014 Finale Deutschland Argentinien PK Schweinsteiger
Bastian Schweinsteiger wa Bayern Munich na timu ya taifa ya UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa

Nae mchezaji wa kati wa timu ya taifa mabingwa wa dunia Ujerumani bastian Schweinsteiger ameomba radhi leo baada ya kupatikana video inayomuonesha mchezaji huyo nyota wa Bayern Munich akiimba nyimbo yenye kuikashifu timu hasimu ya Borussia Dortmund.

Schweinsteiger alionekana katika kanda hiyo akiimba , BVB ni watoto wa malaya, wimbo ambao ni maarufu kwa mashabiki wa Bayern Munich, wakati akiwa katika na kundi la mashabiki katika pati ya faragha.

Video hiyo ambayo ilipigwa siku mbili baada ya ushindi wa Ujerumani wa bao 1-0 dhidi ya Argentina katika fainali ya kombe la dunia, imemlazimu Schweinsteiger kuomba radhi katika ukurasa wake wa facebook.

Katika michezo ya Tennis.

Serena Williams ameendelea kuwa juu ya msimamo wa wachezaji bora wa mchezo huo katika orodha iliyotolewa leo Jumatatu na shirikisho la mchezo huo duniani. Serena anafuatiliwa na Li Na wa China, Simona Halep wa Romania na Petra Kvitova wa jamhuri ya Cheki.

Bundesliga Vorbereitungen für die Saison 2014/2015
Timu ya BVB ikifanya matayarisho kwa msimu wa 2014/2015Picha: imago

Katika mbio za magari , magari ya Mercedes yametamalaki katika mchezo huo wa mbio za magari za formula one msimu huu hadi sasa lakini ushindi wa kusisimua wa Daniel Ricciardo wa magari ya Red Bull katika mbio hizo jana nchini Hungary umeipa timu hiyo ya waendesha magari ya Austria matumaini kwa ajili ya sehemu ya pili ya kampeni .

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre

Mhariri: Josephat Charo