1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 100 ya aibu

Admin.WagnerD24 Aprili 2015

Ni miaka mia moja sasa tokea majeshi ya himaya ya Osman (Ottoman) yafanye mauaji ya halaiki ya Waarmenia Milioni moja nusu mnamo mwaka wa 1915. Watu duniani kote wanayakumbuka mauaji hayo

https://p.dw.com/p/1FEEF
Viongozi wa dunia wakumbuka mauaji ya kimbari ya Waarmenia
Viongozi wa dunia wakumbuka mauaji ya kimbari ya WaarmeniaPicha: Reuters/RIA Novosti/Kremlin/A. Nikolsky

Warmenia wa ndani na nje ya nchi, leo wanawakumbuka watu wao waliouliwa na majeshi ya himaya ya Ottoman wakati wa vita kuu vya kwanza.

Nchini Armenia kwenyewe watu watafanya msafara kuelekea kwenye sehemu ya kumbukumbu iliyopo kilimani ambako wataweka maua na mishumaa kwenye mwenge wa daima.

Viongozi wa dunia waenda Armenia

Marais wa Urusi Vladimir Putin na wa Ufaransa Francois Hollande ni miongoni mwa viongozi wa dunia wanaotarajiwa kwenda nchini Armenia ili kushiriki katika kuomboleza na kuwakumbuka watu wa Armenia Milioni moja na nusu waliouliwa na askari wa utawala wa Ottoman.

Nchi zaidi ya 20 duniani ,miongoni mwao Urusi na Ufaransa zinayatambua mauaji hayo kuwa ya kimbari. Katika hotuba yake hapo jana Rais wa Ujerumani Joachim Gauck pia aliyaita mauaji hayo kuwa ni ya kimbari. Hata hivyo Rais Gauck amekumbusha kwamba Ujerumani iliyokuwa mshirika wa himaya ya Ottoman wakati wa vita kuu vya kwanza pia inapasa kubeba lawama.

Wakimbizi wa Armenia mwaka 1915.
Wakimbizi wa Armenia mwaka 1915.Picha: picture-alliance/United Archives/TopFoto

Gauck amekumbusha kwamba askari wa Ujerumani walishiriki katika kuandaa mipango na kwa kiasi fulani walishiriki katika kuwasafirisha kwa nguvu Waarmenia na kuwapeleka kwenda kuuliwa.

Gauck asema Ujerumani pia inawajibika

Rais Gauck amesema maafa yaliyowafika Waarmenia ni mfano wa historia ya maangamizi,ya mauji ya kimbari, na mfano wa watu kutimuliwa kutoka makwao. Amesema ni mfano wa mauaji ya halaiki yanayoionesha kwa kiwango cha kutisha sura ya karne ya 20. Spika wa Bunge la Ujerumani Norbert Lammert pia amesema kuwa mauji ya Waamenia yalikuwa ya kimbari. Leo Bunge la Ujerumani linafanya mjadala juu ya mauaji hayo ya kimbari.

Rais Obama hapo jana aliyaita mauaji hayo kuwa ni mabaya. Hata hivyo Uturuki imekanusha kuwa mauaji hayo yalikuwa ya kimbari. Uturuiki imesema Waarmenia wapatao 500,000 waliuawa lakini kutokana na vita na njaa

Rais wa Armenia Serge Sarkisian ameelezea matumaini kwamba kutambuliwa mauaji ya Waarmenia kuwa ya kimbari kutaliondoa doa la miaka 100 ya kuyakanusha maangamizi hayo.

Kumbumbuku za mauaji hayo leo zitawaleta pamoja mamilioni ya watu katika miji ya Paris, Los Angeles na kwingineko. Hapo jana kanisa Kuu la Armenia lilifanya sala ya maombolezo na kuwapa hadhi ya utakatifu watu hao milioni moja na nusu waliongamizwa na majeshi ya utawala wa Ottoman.

Mwandishi: Mtullya Abdu
Mhariri:Gakuba Daniel