1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya17 Septemba 2014

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni juu ya vifo vya mamia ya wakimbizi na pia wanazungumzia juu ya mfungamano wa kimataifa dhidi ya magaidi wa dola la Kiislamu.

https://p.dw.com/p/1DDhF
Maafa kwenye bahari ya Mediterania
Maafa kwenye bahari ya MediteraniaPicha: picture alliance/ROPI

Gazeti la "Landeszeitung Lüneberg"linasema bara la Ulaya linapaswa kulaumiwa kwa kutokea maafa ya wakimbizi katika sehemu yenye ulinzi mkali kuliko kwengine kote kule duniani.Bara la Ulaya limeshindwa kuchangia katika juhudi za kuiweka misingi imara ya maisha kwa wakimbizi hao katika nchi zao.

Gazeti la "Eisenacher Presse" pia linatoa lawama kwa bara la Ulaya juu ya kutokea maafa ya wakimbizi. Mhariri wa gazeti hilo anasema sera ya Umoja wa Ulaya juu ya wakimbizi inastahiki kupata cheti cha kufeli mtihani. Mhariri anasema haitoshi kwa bara la Ulaya kujifungia ndani ya kuta. Baada ya muda fulani kuta hizo hazitaweza kusimama tena. Mazingira yanayosababisha tatizo la ukimbizi lazima yashughulikiwe. Lakini awali ya yote Italia iliyopo mpakani inatakiwa iounyeshe moyo wa mshikamano.

Mfungamano dhidi ya magaidi
Nchi kadhaa zimekubaliana kuunda muungano ili kupambana na magaidi wa kinachoitwa dola la Kiislamu.Makubaliano hayo yalisisitizwa kwenye mkutano uliofanyika hapo jana mjini Paris.Lakini mhariri wa gazeti la "Badische" anasema suala muhimu halikuzingatiwa.

Mhariri huyo anauliza jee nani atachukua mahala pa dola la Kiislamu baada ya magaidi hao kufurushwa? Tokea kuangushwa kwa madikteta Saddam Hussein wa Iraq na Kanali Gaddafi wa Libya, imedhihirika wazi kabisa kwamba matokeo ya kutumia nguvu za kijeshi pekee, ni kuzuka kwa pengo la maamlaka, na wanasiasa wanaofuatia hushindwa kukubaliana juu ya namna ya kuijenga nchi upya. Ni kutokana na kuyatambua hayo ,mhariri anauliza kwa nini wajumbe kwenye mkutano wao hawakujaribu kuyatafuta masuluhisho tokea mwanzo.

Mazoezi ya kijeshi ya NATO

Nchi za Nato, zinazoongozwa na Marekani zinafanya mazoezi ya kijeshi magharibi mwa Ukraine. Mhariri wa gazeti la "Märkische Oderzeitung" anauliza iwapo ni lazima kuyafanya mazoezi hayo sasa. Anaeleza licha ya hatua ya kuyasimamisha mapigano, bado pana hatari ya mapigano hayo kuripuka tena baina ya waasi na majeshi ya serikali ya Ukraine. Mbali na hayo Urusi imeijibu hatua ya Nato ya kufanya mazoezi ya kijeshi kwa kukataa kushiriki kwenye mkutano juu ya ugavi wa gesi kwa Ukraine uliokuwa ufanyike mjini Berli. Ndiyo kusema hatua ya nchi za Nato imezihujumu juhudi za kidiplomasia zenye lengo la kuutatua mgogoro wa nchini Ukraine.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman