1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni :Mkataba wa amani Msumbiji

Abdu Said Mtullya26 Agosti 2014

Serikali ya Msumbiji imetiliana saini mkataba wa amani na waasi wa Renamo ,siku chache kabla ya kuanza kampeni za uchaguzi utakaofanyika mwezi wa Oktoba. Jee mkataba huo utatekelezwa? Claus Stäcker atoa maoni yake.

https://p.dw.com/p/1D1EC

Mkataba huo wa amani unayamaliza mapigano yaliyozuka tena mnamo mwaka wa 2012 unaokumbusha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mnamo mwaka 1975 hadi 1992 nchini Msumbiji.

Chama cha waasi cha Renamo kiliyaanzisha tena mapigano dhidi ya chama kinachotawala, Frelimo kwa kufanya mashambulio kwenye njia muhimu za biashara kwa uhodari mkubwa. Kama pana kitu ambacho chama cha Renamo kinaweza kukifanya kwa uhodari, basi ni vita vya msituni.

Deutsche Welle Claus Stäcker
Mwandishi wa DW Claus StäckerPicha: DW

Mashambulio yaathiri uchumi

Mashambulio yaliyobabisha vifo vya watu 50 yaliitia Msumbiji uchungu.Hali ya uchumi ilikuwa mbaya kutokana na mashambulio hayo.Usafirishaji wa makaa ya mawe nchi za nje ulizuiwa na watalii waliipa Msumbiji kisogo.Kila shambulio liliivuruga sifa ya Msumbiji kwa kiwango kikubwa.

Chama cha waasi, Renamo kilijipatia umaarufu mkubwa zaidi wa kisiasa kuliko hapo awali kutokana na kutumia nguvu. Lakini katika chaguzi za mwaka wa 2004 na 2009 chama hicho hakikuweza kuwahamasisha wapiga kura wengi.Pamoja hayo chama hicho kilifarakana na chama kingine cha upinzani, MDC kilichofanikiwa kuichukua ngome kuu ya kwanza ya Renemo katika uchaguzi uliopita.

Jeshi la msingi la kiongozi wa chama cha Renamo Alfonso Dhlakama ,lilikuwamo hatarini kuupoteza umuhimu wake. Na ndiyo sababu liliamua kuyaanzisha tena mapigano.

Mkataba mwingine wa amani

Na sasa kwa mara nyingine Renamo imelitiliana saini mkataba wa amani na chama kinachotawala Frelimo. Jee mambo yatarejea kule kule yalikotokea?

Mnamo mwaka wa1992 vyama vya Frelimo na Renamo vilitiliana saini mjini Rome mkataba wa amani baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya watu karibu Milioni moja. Na hapo hasa ndipo ulipo mzizi wa fitina.

Milango ya jeshi imefungwa kwa Renamo

Wapiganaji wa Renamo hawakuingizwa katika jeshi kama ilivyokubaliwa. Kampeni za uchaguzi zinaanza Jumapili ijayo kwa ajili ya uchaguzi utakaofanyika kati kati ya mwezi wa Oktoba. Ndiyo sababu kwamba pande zote mbili,Frelimo na Renamo zinahitaji ishara ya amani. Bila ya hatua hiyo iisingeliwezekana kwa kiongozi wa Renamo Dhlakama kuingia katika kinyang'anyiro cha kuwania urais.

Kwa mujibu wa katiba ya Msumbiji Rais wa sasa Armando Guebuza hatagombea tena, kwa sababu ameshaimaliza mihula miwili. Mgombea wa urais kwa niaba ya Frelimo atakuwa Filipe Nyussi. Rais Guebuza ameiweka Msumbiji katika hadhi ya kimataifa. Msumbiji inafikia ustawi wa uchumi wa asilimia 7 kila mwaka kutokana na maliasilia,nishati na kilimo. Na punde tu, Msumbiji inaweza kushika nafasi ya tatu duniani katika kuuza gesi. Msumbiji pia ina utajiri mkubwa wa madini.

Umasikini mkubwa

Rais Guebuza na familia yake wana leseni za migoni,usafirishaji na kampuni nyingine kadhaa. Lakini nusu ya wananchi wa Msumbiji ni masikini sana. Mazingira hayo yanastawisha,ufisadi,biashara ya mihadarati na ujangili .

Chama cha Frelimo kinahitaji utulivu nchini ili kupata mafanikio zaidi. Mkataba mpya wa amani umetiwa saini. Lakini pande zote mbili zinautathmini mkataba huo kuwa ni mwanzo tu wa zama mpya. Kwani Renamo bado wanawekwa nje ya jeshi la Msumbiji na wapiganaji wake bado wanazo silaha zao. Ndiyo kusema haijulikani ni kwa muda gani mkataba huo utaendelea kutekelezwa. Kwa sasa hakuna anaeweza kuyatarajia mengi.

Mwandishi: Claus Stäcker.

Tafsiri:Mtullya Abdu.

Mhariri; Yusuf Saumu