1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lubitz aliugua msongo wa mawazo

27 Machi 2015

Msaidizi wa rubani aliyeiangusha ndege ya Germanwings iliyokuwa na watu wengine 149 katika milima ya Alpes ya Ufaransa, alitibiwa "msongo wa mawazo" miaka sita iliyopita kwa mujibu wa gazeti la Bild.

https://p.dw.com/p/1EyMZ
Andreas Lubitz-rubani wa ndege ya GermanwingsPicha: picture alliance/AP Photo

Waendesha mashitaka nchini Ufaransa, baada ya kusikiliza sauti zilizonaswa na kisanduku cheusi, hawakutoa sababu kwa nini Andreas Lubitz,mwenye umri wa miaka 27,aliamua kuidhibiti ndege hiyo chapa Airbus A320,kumfungia Rubani mwenzie nje ya chumba cha rubani na kuiangusha makusudi toka kima cha futi 3000 kwa dakika moja.

Likinukuu nyaraka husika na duru za shirika la ndege la Ujerumani Lufthansa,gazeti la Bild limesema Lubitz amepitisha mwaka mmoja na nusu kutibiwa msongo wa mawazo na kwamba nyaraka zinazozungumzia hali hiyo zitakabidhiwa wachunguzi wa Ufaransa mara tu baada ya kuchunguzwa na maafisa wa Ujerumani.

Mwenyekiti wa shirika la ndege la Ujerumani - Lufthansa, Carsten Spohr, aliuambia mkutano na waandishi habari jana kwamba Lubitz alisitisha mafunzo yake ya urubani miaka sita iliyopita,lakini hakueleza kwanini na kuongeza amepasi mitihani yote inayomruhusu kurusha ndege.

Hakuna ushahidi wa maana uliopatikana

Msemaji wa shirika la ndege la Lufthansa amesema shirika hilo halitotoa maelezo kuhusu hali ya afya ya msaidizi huyo wa rubani.

Montabaur Wohnort Andreas Lubitz Durchsuchung Polizei
Numba ya Lubitz huko Montabaur yasachiwa na polisiPicha: Getty Images/T. Lohnes

Wakati huo huo polisi nchini Ujerumani wameisachi nyumba ya msaidizi huyo wa rubani mjini Düsseldorf na kuchukua hati kadhaa ambazo zinahitaji kuchunguzwa kama zinahusiana kwa namna moja au nyengine na kisa cha kuangushwa ndege ya Germanwings na kuangamiza maisha ya watu 150.

Msemaji wa polisi mjini Düsseldorf amekanusha ripoti za kugunduliwa hati zozote muhimu.

"Hakuna ushahidi wowote wa maana uliopatikana hadi sasa" amesema Susan Heusgen mbele ya waandishi habari.Mwendesha mashtaka wa mjini Düsseldorf anapanga kutoa maelezo ziada kuhusu uchunguzi huo unaoendelea,baadae leo mchana.

Maombolezi yanaedelea nchini Ujerumani

Wajerumani wangali bado wameduwaa wanashindwa kuelewa kwanini kijana kama huyo amesababisha msiba kama huu.

Germanwings / Absturz / Wrackteil
Mabaki ya ndege ya Germanwings yaliyogunduliwa mahala ndege hiyo ilikoangukiaPicha: picture-alliance/dpa

Baraza la wawakilishi wa majimbo limeanza kikao chake hii leo kwa kukaa kimya dakika moja kuwakumbuka wahanga wa ndege iliyoangushwa ya Germanwings.

Na katika eneo la milimani la Seyne Les Alpes ,karibu na mahala ndege hiyo ilikoangukia,uchunguzi unaendelea kwa siku ya nne hii leo kukitafuta kisanduku cha pili cheusi pamoja na kugundua miili na kuihamisha toka milimani baada ya kulinganishwa na vipimo vya viini vya miili ya familia zao.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP/dpa
Mhariri: Yusuf Saumu