1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchumi unaporomoka kwa kuwa wanunuaji hawanunui.

Nyamiti Kayora21 Januari 2015

Mtu ungedhani kwamba kuporomoka kwa bei ni jambo jema, lakini wachumi wanasema kila bei za bidhaa zinavyoshuka ndivyo watumiaji wanavyoacha kufanya manunuzi wakingojea punguzo jengine la bei.

https://p.dw.com/p/1ENnj
Wanawake wa Misri wakiwania kununua mikate wakati wa kuadimika kwa bidhaa madukani.
Wanawake wa Misri wakiwania kununua mikate wakati wa kuadimika kwa bidhaa madukani.Picha: Reuters/M. Abd El Ghany

Wachumi ulimwenguni wana wasiwasi. Bei zinaweza kuanguka wakati kila bidhaa zinazotumika siku hadi siku zinaposhuka thamani madukani. Hilo huitwa mporomoko wa bei, ambao licha ya furaha unayoweza kuwa nayo ya kununua vitu kama vile gari au nyumba kwa bei rahisi, bado ni tatizo kubwa.

Na bado ni tatizo linalozalisha tatizo jengine la ziada, nalo ni namna gani wachumi wanaweza kuwafanya watu waelewe kuwa kushuka bei kwa vitu ni tatizo.

Mchumi wa taasisi ya RWI mjini Essen, Ujerumani, Roland Doehrn, anasema kwamba tatizo linakuja pale watu wanapokisia kuwa bei zitaendelea kushuka na hivyo kufikiria kwamba kama akinunua bidhaa fulani ndani ya siku fulani, huenda bei yake itashuka siku inayofuatia, na hivyo kuamua kubakia na pesa zao wakisubiri vitu vishuke bei.

Matokeo ya kuporomoka kwa bei za bidhaa yana athari ya moja kwa moja kwa mapato na matumizi ya watu wa kawaida, kwani kampuni nyingi hulazimika kuchukuwa hatua, kwani nazo huwa zinazalisha fedha kidogo zaidi. Bei zinaposhuka, ni dalili ya kukatwa kwa nafasi za kazi, kupunguzwa mishahara, na katika mazingira mengine ni kufungwa kabisa kwa biashara au kampuni.

Ikiwa hilo litatokezea kwa sehemu kubwa ya biashara na kampuni kwenye nchi, maana yake ni kuwa kila mtu atakumbana na machungu yake, wakiwemo watumiaji wa kawaida wa bidhaa ambao ni wananchi.

Bei zikishuka, madeni hayashuki

Hata kama mfanyakazi atajaaliwa kubakia na kazi yake, katika mazingira kama hayo ni kwamba atalazimika kuishi kwa mshahara mdogo zaidi.

Raia wa Ugiriki wakitoka madukani wakiwa na vitu vichache walivyoweza kununua.
Raia wa Ugiriki wakitoka madukani wakiwa na vitu vichache walivyoweza kununua.Picha: picture-alliance/AP/Petros Giannakouris

Suala la mfanyakazi kupata mshahara mdogo wakati bidhaa nazo zinauzwa kwa bei ya chini lisingelikuwa tatizo ikiwa tu mfanyakazi huyo hana madeni ya ziada. Lakini mara tu suala la madeni likijiingiza hapa, ni wazi kuwa hali inakuwa mbaya zaidi.

Mshahara unaweza kushuka lakini kiwango cha deni hakiwezi kuja chini. Maana yake ni kuwa hata katika wakati ambapo bidhaa zimeshuka thamani, mfanyakazi huyu hupaswa kulipa deni lake akiwa na pato dogo zaidi, na hiyo ndiyo sababu wachumi wengi wanaona kiwango fulani cha mfumuko wa bei ni cha muhimu na lazima pia.

Kiwango fulani cha mfumuko wa bei sio tu kinaonesha kuwa uchumi unaimarika, bali pia kinathibitisha wastani wa maisha ya watu yanakwenda mbele: mshahara unapanda na kiwango cha deni kwa ujumla kinakuwa kwa kasi ndogo.

"Kunapokuwa na mfumuko wa bei, madeni yako yanashuka kila mwaka kwa sababu mapato yako yanaongezeka sambamba na mfumuko huo wa bei," anasema Doehrn.

Mwandishi: Nyamiti Kayora/DPAE
Mhariri: Josephat Charo