1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 1,200 wamekufa kwa Ebola

19 Agosti 2014

Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema zaidi ya watu 1,200 wamekufa katika mataifa ya Afrika Magharibi kutokana na ugonjwa hatari wa Ebola, tangu ulipozuka mwezi Disemba mwaka uliopita.

https://p.dw.com/p/1Cx8p
Madaktari wakijiandaa kubeba maiti ya mgonjwa aliyekufa kwa Ebola Liberia
Madaktari wakijiandaa kubeba maiti ya mgonjwa aliyekufa kwa Ebola LiberiaPicha: Reuters

Taarifa hiyo ya Shirika la Afya Duniani iliyotolewa leo, imeeleza kuwa kulingana na takwimu za hivi karibuni, zaidi ya watu 2,200 wameshaambukizwa virusi vya Ebola. Maafisa wamekuwa wakiendelea kupambana na hatua za kuudhibiti ugonjwa huo ulioanzia nchini Guinea na kusambaa hadi Liberia, Sierra Leone na Nigeria.

Chakula kinapelekwa kwenye hospitali zenye wagonjwa pamoja na watu walioko kwenye maeneo maalum yaliyotengwa, ambao wanashindwa kwenda majumbani kwao kununua chakula, lakini maafisa wanasema masharti ya kuzuia safari za wagonjwa hao yanafanya zoezi la kupeleka chakula kuwa gumu.

WFP yajiandaa kupeleka chakula

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa-WFP, limesema linajiandaa kupeleka chakula kwa watu milioni moja katika kipindi cha miezi mitatu ijayo. Msemaji wa WHO, Fadela Chaib, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa kwa sasa nchi zote zinahitaji msaada wa dharura na kwamba hakumbuki ni lini mara ya mwisho waliwalisha watu milioni moja waliotengwa kwenye maeneo maalum.

Maafisa wa polisi mjini Berlin wakiwa wamevaa vifaa maalum kujikinga na Ebola
Maafisa wa polisi mjini Berlin wakiwa wamevaa vifaa maalum kujikinga na EbolaPicha: Reuters

Wakati huo huo, Waziri wa Habari wa Liberia, Lewis Brown amesema leo kuwa watu wote 17 wanaosadikiwa kuambukizwa virusi vya Ebola, ambao walitoroka katika mashambulizi yaliyofanywa kwenye kituo maalum kilichotengwa mjini Monrovia, wamepatikana. Brown amesema watu hao waliokimbia mwishoni mwa juma lililopita, wamepelekwa kwenye zahanati nyingine.

Waziri huyo amesema watu hao wamehamishiwa katika kituo maalum cha wataalamu wa Ebola kinachoendeshwa na hospitali kuu ya John F. Kennedy. Aidha, amesema madaktari watatu wa Kiafrika walioambukizwa virusi vya Ebola, ambao wamepatiwa dawa za majaribio za ugonjwa huo, ZMAPP, wanaonyesha dalili za kupata nafuu. Kauli hiyo ameitoa kutokana na tathmini iliyotolewa na daktari anayesimamia matibabu yao.

Ama kwa upande mwingine, kitengo cha huduma za dharura mjini Berlin, Ujerumani, imekifunga kituo kinachowahudumia watu wasio na ajira na kumpeleka hospitali mwanamke mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola, ikiwemo homa kali. Hata hivyo, hakuna taarifa zaidi kuhusu utambulisho wa mwanamke huyo, wala kama iwapo alisafiri kutoka nchi za Afrika Magharibi zilizoathiriwa na Ebola.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE,APE
Mhariri: Mohammed Khelef