1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya wakimbizi 700 wahofiwa kufa maji

Admin.WagnerD20 Aprili 2015

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini amesema ni wajibu wa kiutu kwa Umoja wa Ulaya kushuguhulikia janga la wakimbizi katika Bahari ya Meditarenia

https://p.dw.com/p/1FB0o
Symbolbild Flüchtlingsboot Mittelmeer
Tukio la wakimbizi walivyofikwa na mkasa katika Bahari ya MediraniaPicha: Opielok Offshore Carriers/dpa

Akizungumza baada ya katika ofisi za Umoja wa Ulaya mjini Brussels Mogherini amesema kila mtu ana wajibu wa kukabiliana na janga hilo lenye kugharimu maisha ya watu. Amezitaka serikali zilizo katika Umoja wa Ulaya kuunga mkono kwa vitendo katika jitihada za kuwalinda wahamiaji katika Bahari ya Meditarenia.

Akikisitza wakati kuwa "wakati ni huu" wa kushughulikia kwa haraka kwa umoja huo kukabiliana na matukio mabaya ya kufa kwa wahamiaji, amesema wanapaswa kuokoa maisha ya wanadamu pamoja, wote kwa pamoja wanapaswa kulinda mipaka yao sambamba na kudhibiti biashara haramu ya binaadamu. Aidha kiongozi huyo wajuu wa Umoja wa Ulaya alisema Mawaziri wa Umoja wa Ulaya watalijadili jambo hilo nchini Luxembourg.

Idadi ya watu waliokufa

Zaidi ya watu 700 wanahofiwa kufa maji baada ya bodi iliyokuwa na msongamano mkubwa wa watu, wenye kusafrishwa kwa magendo kuzama katika eneo la nje ya mwambao wa Libya. Tukio hilo limezusha ulazima wa Umoja wa Ulaya kuchukua hatua ya kudhibiti mikasa ya vifo vya mauwaji hao kwa wakati huu.

Flüchtlinge Mittelmeer Katastrophe Sizilien
Janga la wakimbizi na jitihada za uokozi katika mji wa SicilyPicha: REUTERS/Alessandro Bianchi

Walinzi wa ufukwe wa Italia ambao wanaratibu jitihada za uokozi wa manusura na miili ya walokufa wanasema watu 28 tu wamefanikiwa kuokolewa katika meli hiyo iliyozama, ambayo imeibua miito mipya kutoka kwa kiongozi wa kanisa Katoliki dunini Papa Francis na viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya katika kile kinachoonekana kama mkasa unaoweza kuepukika.

Msisitzo wa UNHCR

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani UNHCR limesema ushahidi wa walionusurika unaonesha kwamba katika boti ya uvuvi ya urefu wa futi 70 iliyozama kulikuwemo kiasi ya watu 700.

Kwa mujibu wa mwendesha mashitaka katika jiji la Catania, manusura mmoja kutoka Bangladeshi ambae alipelekwa hospitali mjini Sicily kwa kutumia helkopta anasema idadi ya waliokuwemo katika boti hiyo inafikia watu 950 na kutaja idadi ya wanawake 200, watoto 50.

Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk anaangaliwa uwezekano wa kufanyika mkutano mkuu maalumu wa umoja huo wakati huu kukigubikwa na miito kutoka katika matiafa wanachama kama Ujerumani, Uhispania, Ugiriki na Ufaransa. Katika mtandao wake wa Twitter kiongozi huyo amesema ataendelea kuzungumza na viongozi wa Umoja wa Ulaya, Kamisheni kwa lengo la kuondosha kabissa mikasa ya ajali.

Tukio hili la sasa lenye kuchochewa na machafuko katika eneo la Afrika ya Kaskazini, linavunja rekodi ya lile la Malta la Septemba 2014 ambapo watu inakadiriwa wahamiaji 500 walipoteza maisha. Na Oktoba 2013 zaidi ya watu wengine 360 walikufa baada ya boti ndogo walikuwemo kushika moto katika mwambao wa kisiwa cha Lampedusa. Kama tukio hili la sasa likithibitka idadi ya watu waliokufa kwa mwaka huu wa 2015 itapundukia 1,600.

Mwandishi: Sudi Mnette RTR/AFP
Mhariri: Saumu Mwasimba