1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Kerry ziarani Ujerumani

Josephat Nyiro Charo22 Oktoba 2014

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry atazungumza na maafisa wa Ujerumani kuhusu mapambano dhidi ya wanamgambo wa kundi la Dola la kiislamu, ugonjwa hatari wa Ebola na mpango wa nyuklia wa Iran.

https://p.dw.com/p/1DZgk
John Kerry und Frank-Walter Steinmeier 22.10.2014
Picha: Tobias Schwarz/AFP/Getty Images

Alipowasili Berlin, Kerry alikwenda moja kwa moja kukutana na waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier, kwa chakula cha jioni, ambapo ajenga yao ya mazungumzo ilituwama juu ya juhudi za kupambana na wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu nchini Iraq na Syria, pamoja na mzozo unaoendelea nchini Ukraine, ambako inaripotiwa raia mmoja ameuwawa leo na wengine watano kujeruhiwa katika shambulizi la kombora katika mji wa mashariki wa Donetsk unaodhbitiwa na waasi.

Kerry anatarajiwa kukutana tena na Steinmeier baadaye leo na kushiriki katika shughuli maalumu iliyoandaliwa leo kwa ajili ya kumbukumbu za miaka 25 tangu kuanguka kwa ukuta wa Berlin zitakazofanyika mwezi ujao. Viongozi hao wawili wataweka shada la maua katika kumbukumbu ya ukuta wa Berlin ulioanguka mnamo Novemba 9 mwaka 1989.

Kerry kukutana na Merkel

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani anapanga pia kukutana na kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ambaye alikutana wiki iliyopita na rais wa Urusi Vladimir Putin na kuzungumzia njia za kuutanzua mzozo nchini Ukraine.

Merkel mit Steinmeier im Bundestag 16.10.2014
Kansela Angela Merkel (kulia) na Frank Walter SteinmeierPicha: Reuters/Fabrizio Bensch

Waziri huyo aliwasili Berlin jana jioni kwa ziara ya siku mbili akitokea Jakarta Indonesia ambako alikwenda kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa rais mpya wa nchi hiyo, Joko Widodo Jumatatu iliyopita. Akiwa Jakarta Kerry alikutana na mawaziri wakuu kutoka Malaysia na Singapore, Sultan wa Brunei, waziri mkuu wa Australia na waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Ufilipino, ambapo alisifu juhudi zinazofanywa kupambana na kundi la Dola la Kiislamu, lakini akaitaka jumuiya ya kimataifa iongeze juhudi zaidi kukabiliana na wapiganaji wa kigeni.

Ziara ya Kerry mjini Berlin inafanyika wakati uhusiano kati ya Ujerumani na Marekani ukiwa bado umegubikwa na ufichuzi wa taarifa mnamo mwaka uliopita kwamba wakala za ujasusi za Marekani zilifanya ujasusi nchini Ujerumani, ikiwa ni pamoja na kuyafuatilia mawasiliano ya simu ya mkononi ya kansela Merkel.

Mwandishi: Josephat Charo/DPAE/APE/AFPE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman