1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 14 wauwawa katika shambulio la hoteli Somalia

28 Machi 2015

Kuzingirwa kwa hoteli moja na wanamgambo wa kundi la al Shabab katika mji mkuu wa Somalia kumekomeshwa na kupelekea mauaji ya watu 14 akiwemo balozi wa Somalia mjini Geneva.

https://p.dw.com/p/1Eywj
Polisi wa Somalia wakiwa nje ya hoteli iliovamiwa Mogadishu. (27.03.2015)
Polisi wa Somalia wakiwa nje ya hoteli iliovamiwa Mogadishu. (27.03.2015)Picha: Reuters/F. Omar

Kuzingirwa kwa hoteli moja na wanamgambo wa kundi la al Shabab katika mji mkuu wa Somalia kumekomeshwa na kupelekea mauaji ya watu 14 akiwemo balozi wa Somalia mjini Geneva.

Wapiganaji wa Al Shabab wamevamia hoteli hiyo ya Maka Al Mukaram hapo Ijumaa mchana wakati maafisa wengi wa serikali wakiwa ndani ya hoteli hiyo.

Wana usalama wakiongozwa na kikosi maalum kilichopatiwa mafunzo na Marekani kinachojulikana kama "Gaashaan" ikimaanisha Ngao walijipenyeza kwenye hoteli hiyo Ijumaa jioni na kupambana na wavamizi hao wa Al Shabab hadi Jumamosi.

Waziri wa habari Mohamed Abdi amesema watu 14 waliouwawa ni pamoja na balozi wa Somalia kwa Geneva, raia watano,walinzi wanne wa hoteli na wanajeshi wanne wa serikali.Washambuliaji wanne waliovamia hoteli hiyo akiwemo yule ayeliripuwa bomu lililotegwa kwenye gari pia wameuwawa.

Akizungumza katika eneo la tukio huku akionyesha miili ya wanamgambo hao kwa waandishi wa habari amesema operesheni ya kuikombowa hoteli hiyo imemalizika na hiyo ndio miili ya wanamgambo waliokufa waliokuwa wakitaka kuwauwa wananchi wao.Amevishukuru vikosi vya serikali kwa kuwanusuru wananchi waliokuwemo kwenye hoteli hiyo.

Ari ya vikosi vya Afrika haitopwaya

Awali polisi ilisema watu waliouwawa ni 15 na wengine 20 wamejeruhiwa.

Kikosi cha usalama kwenye eneo la hoteli iliovamiwa Mogadishu. (27.03.2015)
Kikosi cha usalama kwenye eneo la hoteli iliovamiwa Mogadishu. (27.03.2015)Picha: Reuters/F. Omar

Vikosi vya kulinda vya Umoja wa Afrika viliwatimuwa Al Shabab kundi lenye mafungamano na Al Qaeda kutoka Mogadishu hapo mwaka 2011 lakini kundi hilo limekuwa likiendelea kufanya mashambulizi ya kuvizia nia ikiwa ni kutaka kuipinduwa serikali na kuanzisha utawala wa sheria za Kiislam "Sharia" nchini humo.

Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini humo kimelaani shambulio hilo ikiwa ni pamoja na mauaji ya mwakilishi wa Somalia katika ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva Yusuf Bari-Bari.

Taarifa yao imesema "Ujumbe wetu kwa wahusika wa kitendo hicho cha kinyama ni kwamba matendo yao hayatouwa mwamko wao wa kuitakia mema Somalia."

Mashambulizi zaidi kufanyika

Sheikh Ali Mahmud Rage msemaji wa Al Shabab amesema katika taarifa ya baruwa pepe kwamba wapiganaji walionusurika katika shambulio hilo wameondoka kwenye hoteli hiyo na ametishia kufanyika kwa mashambulio zaidi.

Wana usalama wakiwa na majeruhi wa mripuko wa bomu lililotegwa kwenye gari nje ya hoteli iliovamiwa Mogadishu. (27.03.2015)
Wana usalama wakiwa na majeruhi wa mripuko wa bomu lililotegwa kwenye gari nje ya hoteli iliovamiwa Mogadishu. (27.03.2015)Picha: picture-alliance/dpa/ S. Y. Warsame

Hakusema watu wangapi walihusika katika shambulio hilo.

Abdiasis Abu Musab ambaye ni msemaji wa operesheni za kijeshi wa al Shabab amesema kwamba waliwalenga maafisa wa serikali tu katika shambulio hilo na hawakuwadhuru raia.

Barabara zilio karibu na hoteli hiyo zimefungwa na vikosi vya serikali na vile vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika.

Mashambulizi yalioanzishwa mwaka jana na vikosi vya Umoja wa Afrika pamoja na jeshi la Somalia yamewatimuwa al Shabab kutoka ngome zao kuu katikati na kusini mwa Somalia wakati mfululizo wa mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani ya Marekani yameuwa viongozi kadhaa wa kundi hilo.

Hapo mwezi wa Februari wapiganaji wa al Shabab waliishambulia hoteli nyengine mjini Mogadishu na kuuwa takriban watu 25.

Mwandishi : Mohamed Dahman / Reuters

Mhariri : Sudi Mnette