1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasemavyo wahariri wa magazeti ya Ujerumani

Admin.WagnerD2 Septemba 2014

Wahariri wa Ujerumani Jumanne hii wanazungumzia juu uamuzi wa serikali ya Ujerumani kuwapelekea silaha wapiganaji wa Kikurdi nchini Iraq, uchaguzi wa jimbo la Saxony, mgogoro wa Ukraine mashariki miongoni mwa mengine.

https://p.dw.com/p/1D5F4
Rais mpya wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk.
Rais mpya wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk.Picha: Reuters

Mhariri wa gazeti la Herbronner Stimme ameandika juu ya uamuzi wa serikali ya Ujerumani kuwapelekea silaha wapiganaji wa Kikurd wanaopambana dhidi ya kundi la Dola ya Kiislamu kaskazini mwa Iraq. Mhariri huyo anasema ni jambo la kushangaza, kwamba katika siku ya kupinga vita serikali iliamua kuvuka msitari mwekundu kwa kupitisha uamuzi wa kupeleka silaha kwa upande unaoshirki vita. Ni uamuzi wa hatari ambao hata bunge kwa kura yake ya ishara limeupitisha, japokuwa wawakilishi hao wa wananchi wanafahamu fika, kwamba raia wengi wanapinga hatua hiyo.

Mhariri wa gazeti la Süddeutsche ameandika juu ya matokeo ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha NPD katika uchaguzi wa jimbo la Saxony siku ya Jumapili. Mhariri huyo anauliza, je, jitihada za kukipiga marufuku chama hicho kinachozidi kudhoofika zilikuwa bure?

Laa hasha, na badala yake siku hiyo ya uchaguzi wa Saxony ilikuwa na habari zake kutatiza. Zaidi ya wakaazi 80,000 wa jimbo hilo walikipa kura zao chama hicho, bila kujali matatizo ya uongozi wa kipuuzi wa chama hicho, na historia ya uhalifu wa maafisa wake na utayari wao kutumia vurugu kimaneno na kivitendo. Hawajaguswa hata na ukweli kwamba kada wa zamani wa ngazi ya juu wa NPD yuko mahakamani kwa mashtaka ya kulipatia silaha genge la wauaji wa chini kwa chini wa NSU.

Mhariri wa gazeti la Landeszeitung ameandika juu ya madai ya ushiriki wa jeshi la Urusi katika mgogoro wa mashariki mwa Ukraine, na hatua ya Umoja wa Ulaya kumteua waziri mkuu wa Poland Donald Tusk kuwa rais mpya wa baraza la umoja huo. Mhariri huyo amesema:

Ulikuwa uamuzi wa busara uliyochukuliwa na mataifa ya Ulaya, katika hali ambapo mipaka ya Ulaya inabadilishwa, kumteua Donald Tusk kuwa rais mpya wa baraza la Umoja wa Ulaya. Pia, inadhaniwa waziri mkuu huyo wa Poland ameipata nafasi kutokana na mgogoro wa Ukraine. Msimamo wa Tusk kukataa matumaini ya hila kuelekea Moscow, na wito wake wa kuiimarisha jumuiya ya NATO, ni utiliaji mkazo wa wazi wa msimamo mpya wa Umoja wa Ulaya.

Miji ya Berlin na Hamburg ya hapa Ujerumani imewasilisha ruwaza zake za gharama nafuu kwa shirikisho la michezo ya olimpiki la Ujerumani yote ikiwania kuteuliwa na shirikisho la Olimpiki la Ujerumani kuwa mwakilishi wa taifa hilo katika kinyanganyiro cha kuandaa michezo ya olimpiki ya mwaka 2024 au 2028. Mhariri wa gazeti la Märkische Oderzeitung ameandika juu ya ruwaza hizi mbili shindani akisema:

Zote zinasismua na itavutia kujua ni ipi imewavutia zaidi watoa maamuzi katika shirkisho la michezo ya olimpiki, au wataamua kuzikataa zote mbili? Pia hilo linawezekana. Lakini kabla ya yote hayo, wakaazi wa Berlin na Hamburg wanapaswa kuhamasishwa kuunga mkono miradi hiyo wa mamiliani, vinginevyo ndoto ya kuanda michezo ya olimpiki inaweza kukatika mapema kuliko ilivyotarajiwa.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/Deutsche Zeitungen.
Mhariri: Josephat Nyiro Charo