1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani Syria waichimbia mkwara UN

Admin.WagnerD20 Januari 2014

Muungano wa upinzani nchini Syria ulitoa muda wa masaa sita kwa Umoja wa Mataifa kufuta mwaliko uliotolewa kwa Iran kuhudhuria mkutano wa Geneva II, vinginevyo wanajitoa.

https://p.dw.com/p/1AttW
Wajumbe wa muunagano wa upinzani wa Syria SNC wakiwa katika mkutano wao mjini Istanbul, Uturuki wiki iliyopita.
Wajumbe wa muunagano wa upinzani wa Syria SNC wakiwa katika mkutano wao mjini Istanbul, Uturuki wiki iliyopita.Picha: Bulent Kilic/AFP/Getty Images

Balozi wa muungano huo mjini London Walid Sayfour aliliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwa njia ya simu siku ya Jumatatu, kuwa aliarifiwa na muungano huo kwamba umetoa masaa sita kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataida Ban Ki-Moon kufuta mwaliko huo vinginevyo wanajiondoa katika mazungumzo.

Naye mjumbe wa kamati ya kisiasa ya muungano huo Anas Abdah, aliliambia shirika la habari la Reuters, kwamba wametoa hadi saa tatu za usiku kwa saa za Afrika mashariki siku ya Jumatatu kwa mwaliko huo kufutwa, na kurudia msimamo wao kuwa watakubali tu ushiriki wa Iran itakapotangaza wazi kwamba inaondoa wanajeshi wake nchini Syria, kukubaliana na maazimio ya mkutano wa Gevena moja, na kujifunga kutekeleza maazimio yote ya Geneva mbili.

Kiongozi wa muungano wa wapinzani wa Syria, Ahmad al-Jarba.
Kiongozi wa muungano wa wapinzani wa Syria, Ahmad al-Jarba.Picha: picture-alliance/dpa

Ban Ki-Moon alipoushangaza upinzani

Iran ndiyo muungaji mkubwa wa kigeni wa utawala wa rais Bashar al-Assad, na ushiriki wake katika mkutano huo umekuwa mmoja ya masuala yaliyozua mjadala mkubwa kuelekea mkutano huo. Katibu mkuu Ban Ki-Moon aliushangaza muungano wa upinzani siku ya Jumapili, alipoialika Iran katika mkutano huo wa Geneva mbili, ambao unatizamwa kama juhudi kubwa zaidi ya jumuiya ya kimataifa kukomesha mgogoro wa Syria unaokaribia kuingia mwaka wa tatu.

Iran ilitangaza leo kuwa imekubali mwaliko huo bila masharti yoyote, lakini vyanzo viwili kutoka nchini humo vilisema kwamba kushiriki kwa Iran katika mazungumzo hayo hakutomaanisha kuwa inaunga mkono mpango wa mpito uliokubaliwa na mkutano wa kwanza uliyofanyika Juni 2012.

Mataifa ya magharibi yale ya kiarabu ya kanda ya Ghuba yanasema yamekuwa yanasita kuunga mkono wazo la kushirikishwa kwa Iran katika mkutano huo unaofanyika mjini Montreux kwa sababu inamsaidia Assad kijeshi, na haikuunga mkono mpango wa mpito wa mwaka 2012. Marekani na washirika wake wanasema mpango huu unamaanisha kuwa Assad anapaswa kujiuzulu.

Usalama ukiimarishwa mbele ya Hotel utakapofanyika mkutano wa amani mjini Montreux.
Usalama ukiimarishwa mbele ya Hotel utakapofanyika mkutano wa amani mjini Montreux.Picha: picture-alliance/dpa

Ufaransa, Saudia zaonyesha mashaka

Ufaransa imesema leo kuwa Iran haipaswi kualikwa katika mkutano huo ikiwa haikubaliani na kuundwa kwa serikali ya mpito yenye mamlaka kamili ya kiutawala. Saudi Arabia, ambayo inawaunga mkono waasi wanaopigana kumuondoa rais Bashar al-Assad, pia inaamini Iran haipaswi kuhudhuria kutokana na msimamo wake juu ya Geneva moja, na hatua yake ya kumuunga mkono kijeshi rais Bashar al-Assad.

Katibu Mkuu Ban alisema wakati akitangaza mwaliko kwa Iran siku ya Jumapili, kwamba alizungumza kwa kirefu na waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif katika siku za karibuni, na kwamba aliamini kuwa utawala mjini Tehran unaunga mkono mpango wa mwaka 2012 wa mazungumzo ya Syria. Ban alisema Zarif alimhakikishia kuwa Iran ingetoa mchango mzuri mjini Montreux.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre,afpe,dpae.
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman.