1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina 107 wauwawa, mwanajeshi wa Israel hajulikani aliko

2 Agosti 2014

Kiasi ya Wapalestina 107 wameuwawa na mwanajeshi mmoja wa Israel hajulikani aliko wakati wimbi jipya la ghasia likilikumba eneo la ukanda wa Gaza leo (02.08.2014)baada ya kushindwa makubaliano ya kusitisha mapigano.

https://p.dw.com/p/1CnkK
Gaza Israel Krieg Angriff 1. August
Mashambulizi dhidi ya ukanda wa GazaPicha: picture alliance/Abed Rahim Khatib

Mashambulio yameendelea usiku kucha , na kusababisha Wapalestina 35 kuuwawa katika mji wa Rafah katika ukanda wa Gaza pekee katika mashambulizi kadhaa ya anga ya jeshi la Israel katika muda kufikia usiku wa manane jana Ijumaa.

Rais wa Marekani Barack Obama ametoa wito wa kuachiliwa bila masharti mwanajeshi ya Israel, mwenye umri wa miaka 23 luteni Hadar Goldin, lakini pia amesema juhudi zaidi zinapaswa kuchukuliwa kulinda raia wa Gaza.

Israel / Gazastreifen / Nahost-Konflikt
Mwanajeshi wa Israel akitayarisha makomboraPicha: Reuters

Hamas watajutia kitendo cha kumteka mwanajeshi

Waziri wa sheria wa Israel Tzipi Livni , ambae ni mjumbe wa baraza la mawaziri wanane wanaohusika na usalama , ameishutumu Hamas kwa kuhusika na upoteaji wa mwanajeshi huyo na kusema kundi hilo litaaadhibitiwa vikali.

Hata hivyo mapema leo Jumamosi(02.08.2014) , tawi la kijeshi la Hamas la Ezzedine al-Qassam , limesema halina taarifa kuhusu aliko mwanajeshi huyo aliyepotea.

Kikosi cha Ezzedine al-Qassam hakina taarifa kuhusu mwanajeshi huyo. "Tumepoteza mawasiliano na moja ya kikosi chetu cha mapambano, ambacho kilikuwa kinapigana katika sekta ambako mwanajeshi huyo amepotea na inawezekana kwamba wapiganaji wetu na mwanajeshi huyo wameuwawa," kundi hilo limesema katika taarifa.

Mapigano hayo makali jana Ijumaa na mapema leo Jumamosi, ambapo yalizuka baada ya mpango wa kusitisha mapigano kwa siku tatu kuvunjika baada ya saa kadhaa. Idadi ya Wapalestina waliouwawa jana imefikia 107 na wengine 350 wamejeruhiwa, amesema msemaji wa huduma za dharura katika ukanda wa Gaz Ashraf al - Qedra.

Kumi na tano kati ya wahanga hao , ikiwa ni pamoja na watoto watano wenye umri wa miaka 3-12, ni kutoka katika familia moja ambao nyumba yao iliharibiwa, ameongeza.

Gaza Israel Krieg 01.08.2014
Maandamano ya kupiga vita katika ukanda wa GazaPicha: Getty Images/Afp/Hazem Bader

Idadi ya vifo yaongezeka

Kiasi ya Wapalestina 1,650 , wengi wao wakiwa ni raia , wameuwawa katika siku 26 za mapigano tangu mzozo wa sasa kuzuka, al-Qedra amesema. Kwa upande wa Israel , wanajeshi 63 na raia wawili wameuwawa.

Mashambulizi ya makombora yamesababisha vifo vya watu kadha kusini mwa Gaza saa chache baada ya kusitishwa mapigano, ambayo yalianza majira ya saa mbili asubuhi saa za mashariki ya kati siku ya Ijumaa na yalikusudiwa kudumu kwa muda wa saa 72.

Hamas imeishutumu Israel kwa kuvunja makubaliano hayo, wakati taifa hilo la Kiyahudi limesema linajibu mashambulizi ya maroketi kutoka kwa wapiganaji.

Wakati huo huo bunge la Marekani jana Ijumaa liliidhinisha mswada wenye thamani ya dola milioni 225 wa kusaidia mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora, ambapo baraza la wawakilishi likiidhinisha mswada huo muda mfupi kabla ya wabunge kwenda likizo ya wiki tano ya majira ya joto.

US Präsident Barack Obama Rede
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: Win McNamee/Getty Images

Fedha hizo zitatumika kuimarisha mfumo wa Israel wa ulinzi wa makombora , unaojulikana kama Iron Dome, ambao umesifiwa kwa kudungua maroketi kadhaa yaliyokuwa yakielekea katika ardhi ya Israel yaliyokuwa yakirushwa na wapiganaji wa Kipalestina katika muda wa wiki tatu na nusu za mapigano.

Kura hiyo imekuja siku mbili baada ya wizara ya ulinzi kutangaza kutuma silaha katika taifa hilo la Kiyahudi. Mswada huo sasa utapelekwa kwa rais Barack Obama kwa ajili ya kutiwa saini. Katika mkutano na waandishi habari, Obama amesisitiza kuunga kwake mkono haki ya Israel kujilinda wakati akihimiza ulinzi kwa raia wa Palestina.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / afpe

Mhariri: Bruce Amani