1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Urusi wanawasaidia waasi Ukraine

28 Agosti 2014

Wapiganaji wanaotaka kujitenga wakisaidiwa na wanajeshi wa Urusi wameingia katika mji wa Novoazosk kusini mashariki mwa Ukraine wakati Marekani ikishutumu Urusi kwa kujihusisha moja kwa moja katika vita.

https://p.dw.com/p/1D326
Waasi wanaotaka kujitenga wakiwaonyesha wafungwa wa kivita wa jeshi la Ukraine katika mji wa Donetsk mashariki ya Ukraine.
Waasi wanaotaka kujitenga wakiwaonyesha wafungwa wa kivita wa jeshi la Ukraine katika mji wa Donetsk mashariki ya Ukraine.Picha: Reuters

Kwa mujibu wa mwanamgambo anayepigana kwa upande wa serikali vikosi vya waasi vimeuteka mji wa Savur-Mohyla ulioko kwenye eneo la mlima katika mji wa Donetsk ambao ni muhimu kimkakati katika eneo hilo.

Kurudi nyuma kwa ghafla kwa jeshi la Ukraine kunaonekana kuthibitisha kuwasili kwa vikosi vya Urusi kuwasaidia waasi hao wanaotaka kujitenga ambao katika wiki za hivi karibuni walikuwa chini ya shinikizo kutoka kwa vikosi vya serikali katika ngome zao kuu za Donetsk na Luhansk ambayo ni miji mikuu miwili ilioko mashariki mwa Ukraine.

Mpiganaji huyo kutoka kikosi kinachojulikana kwa jina la Azov ambacho kinalisaidia jeshi la Ukraine ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwa njia ya simu kwamba kuna zana za kijeshi huko Novoazosk ambazo zimewasili kupitia mpakani kutoka Urusi siku mbili zilizopita.

Mpiganaji huyo aliyekataa kutaja jina lake amesema zana hizo zina bendera ya waasi wa Jamhuri ya Donetsk (DNR) lakini hasa ni za vikosi vya Urusi.

Kutekwa kwa mji wa Novoazosk

Mji wa Novoazosk umekuwa kwenye shinikizo kwa siku mbili zilizopita kutokana na msururu wa zana za kijeshi ambazo Waukraine wanasema umetokea mpakani mwa Urusi na kuelekea katika Bahari ya Azov.

Mpiganaji wa waasi akiwa na bendera ya Urusi katika mji wa Donetsk.
Mpiganaji wa waasi akiwa na bendera ya Urusi katika mji wa Donetsk.Picha: picture-alliance/AP

Kuanguka kwa mji wa Novoazosk ambako kumethibitishwa lakini sio rasmi na duru ya kijeshi kutoka serikali ya Ukraine ambayo haikutaka kutajwa jina ni pigo kwa vikosi vya serikali kutokana na kwamba inauweka katika hali ya hatari mji mkubwa wa bandari wa Mariupol ulioko mbali zaidi huko magharibi katika eneo la mwambao.

Balozi wa Marekani kwa Ukraine Geoffrey Pyatt ameandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba baada ya Urusi kuwapatia waasi wa Ukraine vifaru,magari ya kijeshi na zana za kivita zikiwemo zile za kufyetulia maroketi na kutotosha kuvishinda vikosi vya jeshi la Ukraine sasa idadi ya wanajeshi wa Urusi inayozidi kuongezeka wanaingilia kati moja kwa moja katika mapigano yanayoendelea katika ardhi ya Ukraine.

Amesema Urusi pia imetuma mizinga mipya ya kujihami na mashambulizi ya anga ikiwemo ile ya chapa SA-22 mashariki kwa Ukraine na kwamba sasa inahusika moja kwa moja katika vita hivyo.

Urusi yaonywa

Rais Francois Hollande wa Ufaransa ameonya leo hii litakuwa ni jambo lisilovumilika na lisilokubalika ikiwa vikosi vya Urusi viko kwenye mapambano kwenye ardhi ya Ukraine.

Waziri Mkuu wa Ukraine Arseny Yatsenyuk.
Waziri Mkuu wa Ukraine Arseny Yatsenyuk.Picha: picture-alliance/dpa

Waziri Mkuu wa Ukraine Arseny Yatsenyuk ametowa wito kwa Marekani,Umoja wa Ulaya na nchi za Kundi la Mataifa Saba tajiri duniani G7 kuzuwiya mali za Urusi hadi hapo vikosi vya nchi hiyo vitakapondolewa katika ardhi ya Ukraine.

Katika mkutano wa serikali leo hii Yatsenyuk amezitaka nchi hizo kuchukuwa hatua hiyo hadi hapo Urusi itapoondowa wanajeshi wake,zana za kijeshi na mashushu.

Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters/

Mhariri: Mohammed Khelef