1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua kali zichukuliwe

19 Mei 2015

Kisa cha kudhalilishwa wakimbizi katika kituo cha polisi mjini Hannover na juhudi za Umoja wa Ulaya za kupambana na makundi yanayowasafirisha wakimbizi kupitia bahari ya Mediterenia kinyume na sheria magazetini

https://p.dw.com/p/1FRpW
Kituo cha ulinzi cha polisi mjini HannoverPicha: picture-alliance/dpa/J. Stratenschulte

Mada mbili kuu ndizo zilizohanikiza magazetini hii leo:Kisa cha kudhalilishwa wakimbizi wawili katika kituo cha polisi ya shirikisho mjini Hannover na juhudi za Umoja wa Ulaya za kupambana na makundi yanayowasafirisha wakimbizi kupitia bahari ya Mediterenia kinyume na sheria.

Tunaanzia lakini huku huku Ujerumani ambako kisa cha kudhalilishwa wakimbizi wawili waliokuwa wakishikiliwa katika kituo cha polisi ya shirikisho mjini Hannover kinazusha fadhaa na kulaaniwa na kila anaekisikia.Gazeti la Südwest Presse linasema kisa hicho kinakumbusha yaliyotokea katika jela ya Abu-Ghoreib nchini Iraq.GHazeti linaendelea kuandika:"Pindi tuhuma hizo zikidhihirika kuwa ni kweli,basi visa vilivyotokea katika kituo cha ulinzi wa polisi ya shirikisho mjini Hannover vitakuwa vimekithiri kupita kiasi.Kwasababu visa hivyo vinakumbusha picha zilizopigwa na walinzi wa Marekani katika jela ya Abu-Ghoreib nchini Iraq-kwa hivyo visa hivyo vinahitaji kuchunguzwa kikamilifu-hasa kwaajili ya masilahi ya polisi walio wengi wanaofanya kazi zao kila siku kwa kuheshimu maadili.Hali ya kutoaminiana kati ya raia na polisi,mfano wa ile iliyoko nchini Marekani,isiachiwe hata kidogo kuchomoza nchini Ujerumani."

Hishma ya binaadam haiguswi

Gazeti lionalosomwa na wengi humu nchini,"Bild" linahimiza hatua kali zichukuliwe pindi ikidhihirika yanayosemwa yapo.Gazeti linaendelea kuandika:"Polisi ya shirikisho wanafanya kazi inayostahiki kusifiwa.Wanawajibika wahuni wanapofanya fujo katika viwanja vya dimba,wanalinda mipaka,wanapambana dhidi ya makundi yaliyojiandaa ya wahalifu.Ndio maana inachoma unapoona baadhi wanataka kuipaka matope hadhi ya walio wengi.Polisi wa shirikisho anapomdhalilisha mkimbizi,anapomsumbuwa na kumtesa ,waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maiziere ndie anaebidi kuwa wa mwanzo kuingilia kati.Kwasababu kimoja ni dhahir,naawe mjerumani,naawe mgeni,naawe halifu seuze tena mkimbizi asiyeweza kujitetea:hishma ya binaadam haiguswi!Hishma hiyo imetajwa mpaka katika katiba yetu:Kuitetea na kuilinda ni jukumu muhimu la kila mtumishi wa serikali.Kwa maneno mengine bayana:Polisi anaemshambulia mkimbizi hastahiki kuitumikia nchi!

Kuzamisha mashuwa za wakimbizi sio dawa

Mada ya pili magazetini inahusiana na juhudi za Umoja wa Ulaya za kupiga vita shughuli za kuwasafirisha wakimbizi kinyume na sheria.Miongoni mwa hatua zinazopangwa kuchukuliwa ni kuzizamisha mashua kabla hazijaondoka Libya kuelekea katika bahari ya Mediterenia.Gazeti la "Rhein Zeitung" linaandika:"Kwa wakati wote ambao vurugu zitaendelea kutawala nchini Libya,makundi ya wanaosafirisha watu kinyume na sheria wataendelea na shughuli zao bila ya pingamizi.Ulaya kwa hivyo inabidi ipanie zaidi badala ya kutaka kuzizamisha mashua mbovu katika bahari ya Mediterenia.Ni sawa kwamba Umoja wa Ulaya unaweza kwa sehemu tu kusimamia utulivu wa nchi-lakini serikali ya umoja wa taifa wakuiunda ni walibya tu.Na kwa wakati wote ambao dhiki na shida hazishi katika nchi jirani ya Umoja wa Ulaya,kinachohitajika zaidi hapo ni njia halali kwa wanaoomba kinga ya ukimbizi katika umoja wa Ulaya.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahmand