1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahudumu wa afya wagoma Liberia

mjahida 13 Oktoba 2014

Kiongozi wa chama cha wahudumu wa afya Liberia, nchi ilioathirika pakubwa na ugonjwa hatari wa ebola, amesema wahudumu hao wameanza mgomo kudai nyongeza ya mshahara kufuatia huduma yao wanayoitoa kwa wagonjwa wa ebola

https://p.dw.com/p/1DUE6
Wauguzi wa afya Liberia
Wauguzi wa afya LiberiaPicha: Reuters/Christopher Black/WHO

Kiongozi wa chama cha wahudumu wa afya Joseph Tamba, amesema kuanzia leo kutakuwa na mgomo wa nchi nzima katika hospitali zote na kliniki zote zikiwemo zile zinazowahudumia wagonjwa wa Ebola.

Wafanyakazi katika hospitali ya Monrovia ambayo ndio kubwa ya serikali inayowashughulikia wagonjwa hao, wamekuwa katika mgomo wa chini kwa chini siku chache zilizopita wakidai nyongeza ya mishahara, huku wakitupilia mbali ombi la maafisa wa afya kutofanya mgomo huo wakati huu wa janga la ebola, ambalo tayari limeshasababisha vifo vya watu 4,000 katika mataifa ya Afrika Magharibi.

Aidha muakilishi wa wafanyakazi katika hospitali hiyo Alphonso Wesseh amesema wagonjwa kadhaa wamefariki hospitalini humo tangu wahudumu walipoanzisha mgomo wao siku ya Ijumaa. Wiki iliopita Wesseh aliliambia shirika la habari la AFP kwamba mshahara wa wahudumu wa afya umesalia kuwa chini ya dola 250 kila mwezi.

Mtu anayeshukiwa kuugua ugonjwa wa Ebola Liberia
Mtu anayeshukiwa kuugua ugonjwa wa Ebola LiberiaPicha: Reuters/Bindra/UNICEF

Hata hivyo msemaji wa serikali ya Liberia Isaac Jackson amekanusha kuwepo na usumbufu wa aina yoyote katika kliniki iliofunguliwa na shirika la afya duniani WHO mwezi Septemba kwa nia ya kuudhibiti ugonjwa huo uliowauwa watu 2,300 nchini Liberia mwaka huu. Lakini imekuwa vigumu kwa waandishi kuthibitisha hilo kwa kuwa serikali ilipiga marufuku waandishi habari kuingia katika kliniki hizo.

Wakati huo huo WHO imeuelezea ugonjwa wa Ebola kama dharura kubwa ya kiafya kushuhudiwa wakati huu huku likisema msukosuko wa kiuchumi kutokana na ugonjwa huo unaweza kuzuiwa iwapo watu wataelimishwa zaidi juu ya Ebola ili kuzuwiya maambukizi zaidi.

Shirika la afya lasema elimu ya ebola inahitajika zaidi

Mkurugenzi wa shirika hilo Margaret Chan amesema kitu kinachoshuhudiwa kwa sasa ni namna virusi vya ebola vinavyoweza kuuharibu uchumi wa nchi na jamii duniani kote. Chan amesema kuelimisha jamii ni mkakati unaofaa kuzuwiya kuanguka kwa uchumi.

Mwezi uliopita Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon aliwahimiza viongozi katika nchi zilizoathirika kuanzisha vituo maalumu vya kuwatenganisha watu walioambukizwa na watu ambao hawajaambukizwa hii ikiwa ni katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa ebola.

Mkurugenzi wa shirika la afya duniani WHO Margaret Chan
Mkurugenzi wa shirika la afya duniani WHO Margaret ChanPicha: AP

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia alitoa wito kwa mashirika ya ndege za kimataifa na kampuni za usafiri wa majini kutosimamisha huduma zao kuelekea nchi zilizoathirika kutokana na kwamba hatua hiyo inatatiza huduma za kiutu katika maeneo hayo na hata usaidizi wa huduma za afya.

Huku hayo yakiarifiwa maafisa wa afya nchini Marekani wameimarisha ukaguzi wa wafanyakazi wa afya waliomhudumia mtu wa kwanza kuambukizwa ugonjwa wa ebola nchini Marekani baada ya mmoja wao kuambukizwa ugonjwa huo kando na kwamba alikuwa amevalia nguo maalum za kujikinga na virusi.

Hapo jana mkuu wa shirika la kudhibiti na kuzuwiya magonjwa CDC daktari Tom Frieden amesema kumekuwa na uvunjifu wa kanuni uliopelekea muunguzi kuambukizwa ugonjwa wa ebola wakati wa kumhudumia Thoma Duncan aliyefariki mwezi uliopita.

Mkuu wa shirika la kudhibiti na kuzuwiya magonjwa CDC daktari Tom Frieden
Mkuu wa shirika la kudhibiti na kuzuwiya magonjwa CDC daktari Tom FriedenPicha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo Haijajulikana ni vipi kanuni hizo zilivyovunjwa lakini Rais Barrack Obama ameliomba shirika hilo kuchukua hatua za haraka kuchunguza kisa hicho.

Kwa sasa Hospitali ya mjini Texas inafanya ukaguzi wa takriban watu 50 wanaoaminika kumsogelea kwa karibu mtu wa kwanza aliyeambukizwa ugonjwa nchini Marekani Thomas Duncan wakati walipokuwa wanamhudumia.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/AP

Mhariri Yusuf Saumu