1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahouthi waiteka kambi ya kikosi maalumu

Admin.WagnerD25 Februari 2015

Kundi la jamii ya Houthi nchini Yemen ambalo linaudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo Sana'a, limeiteka kambi ya kikosi maalum katika mji huo. Hayo yametokea wakati watu wenye silaha wakiwa wamemteka raia wa Ufaransa.

https://p.dw.com/p/1Egxc
Wapiganaji wa kihouthi wakishika doria katika mitaa ya Sana'a
Wapiganaji wa kihouthi wakishika doria katika mitaa ya Sana'aPicha: picture-alliance/dpa/Str

Wahouthi wameiteka kambi hiyo ya kikosi maalumu cha jeshi baada ya mapigano makali yaliyotokea usiku wa kuamkia leo. Kwa muda wa masaa sita waasi hao waliishambulia kambi hiyo kwa silaha nzito, hayo yakiwa kwa mujibu wa wanajeshi waliotoroka mapigano hayo.

Taarifa zaidi zimeeleza kuwa makamanda wa kikosi hicho kilichoshambuliwa waliamua kuondoka usiku wa manane, baada ya sehemu muhimu za kambi yao kuangukia mikononi mwa wahouthi. Watu wasiopungua kumi waliuawa katika mapigano hayo.

Raia wa Ufaransa achukuliwa mateka

Huku hayo yakiarifiwa, mwanamke raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 30 amechukuliwa mateka na watu wenye silaha mjini Sana'a. Mwanamke huyo Isabelle Prime ni mfanyakazi wa mradi wa Benki Kuu ya Dunia, unaoisaidia serikali ya Yemen kuratibu huduma za kijamii. Baada ya kukamatwa kwake rais wa Ufaransa Francois Hollande amewataka raia wa nchi yake kuepuka sehemu zenye hatari nchini Yemen.

''Nachukua muda huu kwa masikitiko makubwa, kuwaomba raia wetu ambao wako katika maeneo yenye kitisho kikubwa cha usalama kufanya wawezavyo kujiweka mbali na maeneo hayo, kwa sababu kitisho kinachowakabili ni cha dhahiri'' Alisema rais Hollande.

Rais Mansour Hadi aondoa uamuzi wa kujiuzulu

Wapiganaji wa kundi hilo walichukua udhibiti wa mji mkuu wa Yemen mwezi Septemba mwaka jana, na mwezi uliopita waliyazingira makazi ya rais Abd-Rabbu Mansour Hadi, hali ambayo ilimlazimu rais huyo kujiuzulu na kuacha pengo la uongozi katika nchi hiyo.

Abd Rabbo Mansur Hadi Präsident Jemen
Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo//H.Mohammed

Wiki iliyopita Rais Mansour Hadi alifanikiwa kutoroka kizuizi alichokuwa amewekewa na wapiganaji wa kihouthi katika mji wa Sana'a na kukimbilia katika mji wa kusini wa Aden, ambako amekana tangazo la awali la kujiuzulu kwake, akishikilia kuwa yeye ndiye rais halali wa Yemen.

Msaidizi wa raia Abd-Rabbu Mansour Hadi ameiondoa barua ya kijiuzulu kwa rais huyo ambayo ilikuwa imewasilishwa mbele ya bunge, ambalo hata hivyo halikuweza kukutana rasmi kujadili hatua yake hiyo ya awali.

Aidha, Rais huyo amewaandikia barua wabunge wote nchini Yemen akiwaomba ushirikiano katika kuhakikisha hali ya kawaida inarejeshwa katika mikoa yote ya nchi. Aliwataka pia mawaziri wote kukutana haraka mji Aden.

Hata hivyo waziri mkuu pamoja na mawaziri kadhaa wa serikali bado wako kizuizini chini ya ulinzi wa wahouthi katika mji mkuu, Sana'a. Wahouthi kwa upande wao wamezitahadharisha nchi dhidi ya kujihusisha kwa hali yoyote na rais Mansour Hadi, ambaye wamesema anasubiri kufikishwa kizimbani.

Wachambuzi wa masuala ya siasa za mashariki ya kati wanaituhumu Iran inayoongozwa na watu wa madhehebu ya Shia kuwaunga mkono wahouthi kwa lengo la kuiyumbusha Yemen. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry ameihusisha moja kwa moja Iran katika kuanguka kwa serikali ya Yemen.

Wafalme wa nchi za Ghuba ya Uarabu ambao ni kutoka madhehebu ya Suni ambao ni mahasimu wa Iran, wamewaomba wayemen kusimama imara na kumuunga mkono rais wao, kuiondoa nchi yao katika kile walichokiita ''hali ya kutisha iliyosababishwa na wahouthi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman