1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri: China na Marekani zaweka historia

Mohammed Khelef12 Novemba 2014

Wahariri wanazungumzia makubaliano ya China na Marekani kwenye mabadiliko ya tabia nchi, mazungumzo ya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Petro Poroshenko wa Ukraine na vijana wanaojiunga na siasa kali.

https://p.dw.com/p/1DljQ
Rais Barack Obama wa Marekani (kushoto) na Rais Xi Jinping wa China mjini Beijing.
Rais Barack Obama wa Marekani (kushoto) na Rais Xi Jinping wa China mjini Beijing.Picha: Reuters/G. Baker

Mhariri wa gazeti la Neues Deutschland juu ya mazungumzo ya Merkel na Poroshenko, akisema kuwa mapigano yameongezeka kwenye ngome ya waasi mashariki mwa Ukraine, Donetsk. Ni hofu ya kukuwa kwa mzozo huo, hata baada ya usitishaji mapigano, yumkini ndiyo iliyomfanya Poroshenko kuinua simu na kumpigia Merkel kutaka ushauri.

Anaongeza kwa kusema kuwa hakuna anayejuwa ikiwa Poroshenko alipata alichokitaka kutoka kwa Merkel, maana hata naye Merkel anahitaji sasa kushauriwa cha kufanya, baada ya hapo jana kutangaza kuwa hakutakuwa na vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi, licha ya ukweli kwamba hakuna kilichobadilika mashariki mwa Ukraine.

Moja, hata hivyo, walikubaliana kwamba Urusi, waasi wanaotaka kujitenga na jeshi la Ukraine, wanapaswa kwa pamoja kuyaheshimu makubaliano ya mwezi Septemba yaliyofikiwa mjini Minsk, Belarus.

Rais Petro Poroshenko wa Ukraine.
Rais Petro Poroshenko wa Ukraine.Picha: picture-alliance/dpa

Makundi ya siasa kali yashamiri Ujerumani

Mhariri wa gazeti la Kölner-Stadt Anzeiger anajikita juu ya operesheni ya hivi karibuni ya polisi iliyowatia nguvuni vijana kadhaa kwa tuhuma za kuwa na mafungamano na makundi ya kigaidi.

Misako na kamatamakata za polisi zimeendelea kwenye jimbo la North-Rhine Westphalia. Kufikia jioni ya jana, watuhumiwa tisa wenye umri wa kati ya miaka 28 na 58 walikwishakamatwa, kwa mujibu wa polisi.

Lakini anahoji mhariri huyo kwamba watuhumiwa wa mara hii hawakutoka misikitini pekee kama ilivyozoeleka, bali pia na makanisani. Na miongoni mwa makosa wanayoshukiwa nayo, si kujiunga na makundi ya kigaidi, bali kuchochea chuki dhidi ya wengine.

Mhariri huyo anasema kwamba Ujerumani inapaswa sasa kuukabili uhalisia kwa kutumia uhalisia kwani miongoni mwa vijana wanaokamatwa wakihusishwa na siasa kali, ziwe za kidini au za ubaguzi wa rangi, muna watoto wa Kijerumani, waliozaliwa na Wajerumani toka-nitoke, na sio tu vizazi vya wageni.

Polisi wa Ujerumani mjini Cologne wakilinda maandamano ya kundi la Salafi dhidi ya wahuni waliotaka kuwashambulia mwishoni mwa mwezi Oktoba 2014.
Polisi wa Ujerumani mjini Cologne wakilinda maandamano ya kundi la Salafi dhidi ya wahuni waliotaka kuwashambulia mwishoni mwa mwezi Oktoba 2014.Picha: picture-alliance/dpa/C. Seidel

Makubaliano ya China na Marekani

Mhariri wa Neue Osnabrücker anayaita makubaliano ya China na Marekani juu ya upunguzaji wa gesi chafu kulinda tabaka hewa dunianhayo kuwa ni ya kihistoria, lakini ni ya kushangaza sana kwamba wachafuzi wawili wakubwa wa hewa duniani ndio leo wanaosimama kudai kuisafisha hewa hiyo.

Mataifa hayo mawili yamekubaliana kuwa kufikia mwaka 2025 wawe wamepunguza hewa chafu kwa asilimia 28, huku China ikiahidi kufikia ukomo wake wa utoaji wa chafu kufikia mwaka 2030.

Kheri i matumboni mwa shari, anamalizia mhariri huyo. Labda mchawi akikabidhiwa yeye mwana, atamlea na kumtunza, kwani zilikuwa serikali za China na Marekani ndizo zilizokuwa zikizuwia kufikiwa makubaliano kwenye makongamano ya tabia nchi ya Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman
Vyanzo: Neue Osnabrücker, Neues Deutschland, Kölner-Stadt Anzeiger