1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WADA yaelezea wasiwasi kuhusu hali ya Kenya

18 Aprili 2015

Shirika la Kupambana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni – WADA limesema kuwa litafanya mazungumzo na maafisa wa Kenya kuhusiana na tatizo la matumizi ya madawa yaliyopigwa marufuku

https://p.dw.com/p/1FASO
Chicago Marathon 2013 Rita Jeptoo
Picha: picture-alliance/dpa/Tannen Maury

WADA inasema makala hiyo iliyorushwa na televisheni moja nchini Kenya ilidaiwa kumwonesha mwanamme akichomwa sindano ya kuisisimua damu mwilini katika duka moja la madawa inadhihirisha madai ya awali ya kuwepo visa vya matumizi ya dawa hizo nchini Kenya.

Makala hiyo iliyopewa jina la “Miiba ya Sumu” na kurushwa na Televisheni ya Citizen, ilizusha wasiwasi na inaongeza ushahidi wa ufichuzi zaidi uliofanywa mwaka wa 2012 na kipindi cha televisheni ya ujerumani ya ARD ambacho awali kilifichua matatizo ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini nchini Kenya. Mkurugenzi mkuu wa WADA David Howman amesema katika taarifa kuwa wanatarajia kuwa mashirika husika yatachunguza visa hivyo na kuchukua hatua. Amesema shirika hilo litaijadili makala hiyo ya televisheni ya Citizen na mamlaka, wakati maafisa wake watakapozuru Kenya wiki ijayo.

40. Berlin-Marathon Wilson Kipsang Kiprotich 29.09.2013
Mwanariadha wa mbio za Marathon Mkenya Wilson Kipsang KiprotichPicha: picture-alliance/dpa

Maafisa wa Kenya kila mara wanawalaumu mawakala wa kigeni kwa kusababisha hali hiyo na mapema wiki hii Shirikisho la Riadha la Kenya, liliyapokonya leseni makampuni mawili ya kigeni dhidi ya kuhudumu nchini Kenya kwa miezi sita.

Kampuni ya Rosa & Associati na Volare Sports ya Uholanzi yamepigwa marufuku ili kufanyiwa uchunguzi kuhusiana na ongezeko la karibuni la visa vya kutumia madawa ya kusisimua damu.

Hatua hiyo haijapokelewa vyema na wanariadha mahiri nchini humo ambao wakisema kuwa imeyavuruga maandalizi yao ya mashindano ya ubingwa wa ulimwengu na mashindano mengine makuu msimu huu.

Kundi la wanariadha wakiongozwa na anayeshikilia rekodi ya ulimwengu katika mbio za marathon Wilson Kipsang, wametoa taarifa wakisema hatua ya AK imesababisha mtarafuku siyo tu nchini Kenya bali pia kimataifa

Zaidi ya wanariadha 30 wa Kenya wamegunduliwa kutumia madawa yaliyopigwa marufuku michezoni katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, huku nyota wa marathon kwa upande wa wanawake Rita Jeptoo anayewakilishwa na kampuni iliyopigwa marufuku ya Rossa & Associati akiwa mmoja wa walioadhibiwa kwa kupigwa marufuku kwa miaka miwili.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu