1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Madagascar wataka kumuondoa Rais Madarakani

27 Mei 2015

Rais wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina amepinga uhalali wa bunge kupiga kura ya kumuondoa madarakani kwa kutokuwa na imani naye kwa kusema kile nchi hiyo inachohitaji ni uthabiti kuepusha kurejea katika mzozo

https://p.dw.com/p/1FXL0
Picha: Reuters

Wabunge wa Madagascar hapo jana walipiga kura kumuondoa madarakani Rais Rajaonarimampianina kwa madai ya kukiuka katiba na kutomudu majukumu yake katika hatua ambayo inatishia kulirejesha taifa hilo katika mzozo wa kisiasa ulioshuhudiwa baada ya mapinduzi ya serikali mwaka 2009.

Mahakama ya katiba nchini humo sasa ndiyo liliyo na jukumu la kuamua iwapo kura hiyo ya kumuondoa madarakani Rais inaweza kuidhinishwa.

Rajaonarimampianina asisitiza bado ashikilia usukani

Katika hotuba kwa taifa Rais Rajaonarimampianina, amesema bado anasalia madarakani na viongozi wa nchi hiyo wanaendelea kulitumikia taifa na kuongeza kuwa maswali mengi yamezuka baada ya kura hiyo bungeni lakini kinachomtia wasiwasi ni iwapo mchakato unaostahili umefuatwa na uwazi umeheshimiwa katika hatua hiyo ya bunge.

Rais wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina
Rais wa Madagascar Hery RajaonarimampianinaPicha: Reuters

Rais huyo amesema nchi hiyo inastahili kuupa kipaumbele uthabiti na uungwaji mkono na jumuiya ya kimataifa ili kupiga hatua zaidi na sio kuzingatia mivutano ya kisiasa.

Rais anadai kuwa ingawa kura hiyo inasemekana kuungwa mkono na wabunge 121 ni wabunge 80 tu waliokuwepo katika kikao cha bunge cha hapo jana. Kura hiyo inamaanisha iliungwa mkono na thuluthi mbili ya wabunge wote 151 na hivyo inastahili kisheria kumuondoa madarakani.

Rajaonarimampianina amedai kuwa amekataa kuwapa wabunge zawadi wasizostahili kama magari ya kifahari na huenda ndicho kilichochea wabunge hao kumpinga.

Rais huyo aliingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2013 baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu na kuahidi kulikwamua taifa hilo kutoka kwa mzozo wa kisiasa baada ya mtangulizi wake Marc Ravalomanana kung'olewa madarakani katika mapinduzi mwaka 2009.

Aliahidi kuboresha maisha ya raia wake ambao kulingana na benki ya dunia asilimia 75 ya wamadagascar wameorodheshwa maskini lakini kupingwa kwa utawala wake kumeongezeka katika miezi ya hivi karibuni.

Rais akosolewa kwa kutoleta mageuzi

Wanaomkosoa wamesema ameshindwa kutimiza ahadi za kuimarisha uchumi, kukwamisha kuundwa kwa mahakama kuu, kufanyia mageuzi sekta alizoahidi kuziboresha na kuingiza siasa katika masuala ya dini.

Rais wa zamani wa Madagascar Andry Rajaoelina
Rais wa zamani wa Madagascar Andry RajaoelinaPicha: picture alliance/ landov

Hata washirika wake wa kisiasa wamemgeuzia mgongo. Andy Rajoelina aliyeingia madarakani baada ya mapinduzi ya serikali mwaka 2009 kama Rais wa mpito na aliyemsaidia Rajaonarimampianina kuchaguliwa miaka miwil iliyopita, ameungana na Ravalomanana kuwashawishi wabunge wa vyama vyao kupiga kura ya kumuondoa madarakani.

Maridhiano ya kitaifa yalikuwa mojawapo ya masuala makuu katika mchakato wa kumaliza mzozo wa kisiasa uliofikiwa na jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC na vyama vya kisiasa vya Madagascar mnamo mwaka 2011 na uchaguzi uliofutia uliazimia kukomesha msukosuko nchini humo ambao ulisababisha taifa hilo la visiwani kutengwa na jumuiya ya kimataifa na kuuathiri vibaya uchumi wake.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu