1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vurugu na mtafaruku nchini Libya

30 Julai 2014

Kambi muhimu ya kijeshi ya Benghazi imeangukia mikononi mwa Makundi ya itikadi kali na Viongozi wa Serikali wamezidiwa kutokana na Mapigano makali katika Mji mkuu Tripoli

https://p.dw.com/p/1CmGB
Mapigano yapamba moto BenghaziPicha: picture-alliance/dpa

Kutokana na mtafaruku huo,Ufaransa inajiandaa kuwahamisha kwa meli raia wake kutoka Libya baada ya uamuzi wa mataifa kadhaa ya magharibi ikiwemo Marekani,Uholanzi,Canada na Bulgaria kuwahamisha watumishi wa wakala zao za kidiplomasia.

Nchi nyingi zimewataka raia wao waihame nchi hiyo iliyozama katika bahari ya mapigano tangu Tripoli mpaka Benghazi. Baraza la wanamapinduzi wa Benghazi,muungano wa makundi ya itikadi kali limechapisha taarifa inayosema wanadhibiti makao makuu ya vikosi maalum vya jeshi.

Duru za kijeshi zimethibitisha kutekwa "kambi maalum ya kijeshi" na wanamgambo wakiwemo wale wa Ansar Asharia ,wanaotajwa na Washington kuwa ni "magaidi."

Katika mtandao wao wa kijamii Facebook,Ansar Asharia wamechapisha picha za silaha na masanduku kadhaa ya risasi walizoziteka katika kambi hiyo.

Mapigano yanayoendelea Benghazi yameshaangamiza maisha ya zaidi ya watu 60 tangu jumamosi iliyopita.

Ghala za Mafuta zafuka moto Tripoli

Mjini Tripoli,ghala kubwa ya mafuta inaendelea kufuka moto kwa siku ya nne mfululizo kufuatia mapigano ya makundi hasimu ya wanamgambo ya kuania kuudhibiti uwanja wa ndege wa kimataifa..

Libyen Tripolis Brand in Treibstoff Tanks Raketenbeschuss Rakete
Matangi ya mafuta yafuka moto baada ya kushambuliwa kwa makombora mjini TripoliPicha: Reuters

Serikali imeomba msaada kutoka nje,lakini nchi mfano wa Ufaransa na Italia zinashurutisha kwamba mapigano yasitishwe.

Juhudi zote za upatanishi za serikali kujaribu kumaliza mapigano zimeshindwa hadi sasa.Matumaini yanaelekezwa katika bunge jipya linalotokana na uchaguzi wa juni 25 ambalo huenda likalazimisha mapigano yakome.

Lakini wasi wasi umeenea kuhusu uwezekano wa wabunge hao kukutana mjini Benghazi kitovu cha mapigano yanayoendeklea takriban kila siku.

Hali ya vurugu ni faraja kwa wahamiaji

Wakiitumia hali ya vurugu na mtafaruku nchini humo pamoja na hali shuwari ya hewa,mamia ya wahamiaji wa chini kwa chini wamejazana ndani ya mashua,wakiyatia hatarini maisha yao kwa matumaini ya kufanikiwa kuingia barani Ulaya.

Flüchtlinge Lampedusa
Jeshi la wanamaji la Italia lawaokoa wahamiaji karibu na fukwe za Lampedusa nchini ItaliaPicha: picture alliance / ROPI

Wiki hii watu zaidi ya 20 walizama na dazeni kadhaa kutojulikana waliko mashua yao ilipozama katika fukwe za Libya.Msemaji wa jeshi la wanamaji la Libya amesema wahamiaji 22 wameokolewa wakiwa wahai pamoja na miili ya watu zaidi ya 20 waliokufa maji.Kwa mujibu wa waaliosalimika,mashua hiyo ilisheheni wahamiaji 150.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Josephat Charo