1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wazuru eneo la ajali ya ndege

Admin.WagnerD25 Machi 2015

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Rais wa Ufaransa Francois Hollande na Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy wamewasili Seyne-les-Alpes kwenye kituo cha operesheni ya uokozi kuhusiana na ajali ya ndege ya Germanwings

https://p.dw.com/p/1ExU5
Rais Francois Hollande, Kansela Angela Merkel, na Waziri Mkuu Mariano Rajoy karibu na eneo la ajali
Rais Francois Hollande, Kansela Angela Merkel, na Waziri Mkuu Mariano Rajoy karibu na eneo la ajaliPicha: Getty Images/P. Macdiarmid

Kansela Angela Merkel na Rais Francois Hollande walisafiri pamoja katika helikopta kuelekea eneo hilo la ajali. Baadaye Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rahoy alijiunga nao kwenye kituo hilo kilichowekwa karibu na korongo ambamo ndege ya shirika la Germanwings ilianguka jana. Germanwings ni shirika tanzu la Lufthansa, shirika la ndege la Ujerumani.

Viongozi hao watatu wamewashukuru wafanyakazi wa uokozi, na wanatarajiwa kukutana na familia za watu waliokufa katika ajali hiyo, ambayo bado chanzo chake hakijabainishwa. Raia 72 wa Ujerumani ni miongoni mwa wahanga 150 wa ajali hiyo, ambayo pia iliuwa wahispania 49.

Akizungumza mjini Berlin hii leo, waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere amesema hakuna sababu yoyote kushuku kuwa ''hila chafu'' kuhusiana na ajali ya ndege hiyo ya Germanwings, na kuongeza lakini kwamba wachunguzi wataangalia kila sababu zozote zinazowezekana.

Uchunguzi wa kitaalamu utatoa jibu

Waziri wa usafirishaji wa Ujerumani wa Ujerumani Alexander Dobrindt ambaye pia yuko eneo la ajali amesema uchunguzi wa kitaalamu ndio utabainisha chanzo halisi cha ajali hiyo.

Visanduku vya kunakiri safari za ndege iliyoanguka
Visanduku vya kunakiri safari za ndege iliyoangukaPicha: Reuters/BEA

''Sasa kuhusiana na suala juu ya kisanduku cha kunakiri safari za ndege, wataalamu wetu wapo kwa ajili hiyo. Tunatumai kutokana nahabari zitakazopatikana katika kisanduku hicho, tutaweza kueleza bayana kilichosababisha ajali hiyo.'' Alisema waziri Dobrindt.

Jana, Ikulu ya Marekani pia ilisema hakuna dalili zozote za kuhusika kwa ugaidi katika ajali ya ndege hiyo.

Huzuni na simanzi kwa wafiwa

Wakati huo huo utaratibu wa kuwakumbuka watu waliokufa katika ajali hiyo unaendelea. Wafanyakazi wa shirika la Germanwings wamewasha mishumaa katika makao makuu ya shirika hilo kwenye uwanja wa ndege wa Cologne na Bonn, nao wenzao wa shirika mama la Lufthansa wamenyaza kimya kwa muda wa kuanzia saa nne na dakika 53 muda wa hapa Ujerumani, ambapo ndege iliyoanguka ilipoteza mawasiliano.

Ni huzuni kubwa kwa familia zilizopoteza ndugu katika ajali ya ndege ya Germanwings
Ni huzuni kubwa kwa familia zilizopoteza ndugu katika ajali ya ndege ya GermanwingsPicha: picture alliance/AP Photo/A. Dalmau

Katika mji mdogo wa Haltern am See watokako wanafunzi 16 wa sekondari, ambao walikufa katika ajali ya jana wakitoka Uhispania pamoja na walimu wao, huzuni na simanzi vimetanda. Mkuu wa shule hiyo Ulrich Wessel amesema safari iliyoanza kwa furaha imemalizika kwa majonzi, na kwamba msiba huo umeibadilisha milele shule yao.

Ndege iliyoanguka ni aina ya Airbus chapa A320, ambayo ilikuwa na umri wa miaka 24. Wamiliki wake wamesema ilikuwa katika hali nzuri kiufundi, na kwamba umri wake hauchukuliwi kama chanzo cha ajali.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/ape

Mhariri:Mohammed Khelef