1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakusanyika mjini Riga

22 Mei 2015

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amewaambia washirika wa Umoja wa Ulaya katika Ulaya ya Mashariki kutotarajia mambo mengi sana kutoka kwa umoja huo. Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanahudhuria mkutano wa kilele mjini Riga

https://p.dw.com/p/1FU95
EU Gipfel Riga Merkel mit Tsipras
Picha: Getty Images/AFP/A. Jocard

Aidha ameionya Urusi kuzirekebisha mbinu zake kuhusu Ukraine ikiwa ingetaka kujiunga tena katika kundi la mataifa tajiri ulimwenguni la G7. Kansela Merkel, ambaye ametekeleza jukumu muhimu katika juhudi za amani kuhusu mzozo wa Ukraine, amesema Urusi haina sababu ya kuogopa mahusiano ya karibu baina ya kundi hilo lenye nchi wanachama 28 na mataifa sita yaliyokuwa sehemu ya muungano wa kisovieti.

Katika mazungumzo hayo ya Riga, viongozi wa Umoja wa Ulaya watasisitiza nia yao ya kuyajenga mahusiano ya kisiasa na kiuchumi na Armenia, Azerbaijan, Belarus, Georgia, Moldova na Ukraine.

Mapema leo, Umoja wa Ulaya na Ukraine zimesaini mkataba wa mkopo wa kiasi cha euro bilioni 1.8 katika juhudi za kusaidia kuufufua uchumi wa nchi hiyo ulio na matatizo ya fedha.

Mpango huo unaiihitaji Ukraine kuidhinisha msururu wa mageuzi zikiwemo hatua za kupambana na rushwa ili kuyatatua matatizo ya kimuundo katika uchumi wake.

Katika mkutano huo wa Riga, Umoja wa Ulaya pia umeahidi ruzuku ya euro milioni 200 ili kusaidia biashara ndogondogo na za wastani katika nchi za Ukraine, Georgia na Moldova.

EU Gipfel Riga Merkel mit Tsipras
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiwa mjini RigaPicha: Reuters/I. Kalnins

Merkel pia ameionya Urusi kuwa isifikirie kurejea tena katika Kundi la nchi saba zilizostawi kiviwanda ikiwa itaendelea kukiuka sheria ya kimataifa nchini Ukraine – kutokana na kitendo cha kulinyakua jimbo la Crimea. Uwanachama wa Urusi ulilifanya kundi la G7 kuwa G8 lakini washirika wake wakasitisha uwanachama wake mwaka jana huku wakisusia kuhudhuria mkutano wa kilele ulioandaliwa mjini Sochi na Rais wa Urusi Vladmir Putin kulalamikia hatua ya serikali ya Urusi kuwaunga mkono waasi wa mashariki mwa Ukraine.

Mgogoro wa Ukraine, hata hivyo, ulifichua migawanyiko mikubwa ndani ya umoja huo kuhusu namna ya kushirikiana Urusi. Chini ya Mikataba yao ya Ushirikiano na Umoja wa Ulaya, Georgia, Moldova na Ukraine zinaahidi kufanya mageuzi ya kisiasa na mashirika ya kijamii yanayolenga kuzifanya nchi hizo kuwa na mifumo ya kisasa na kuweka misingi ya kidemokrasia.

Matokeo yake ni kuwa nchi hizo zitaweza kupata nafasi za kiuchumi katika Umoja wa Ulaya, ambao ni mojawapo ya masoko makubwa kabisa ulimwenguni, na ushirikiano mkubwa wa kisiasa. Moldova ilisaini mkataba na Umoja wa Ulaya wa raia wake kusafiri katika nchi za umoja huo bila visa, lakini Umoja wa Ulaya unasema Ukraine na Georgia bado zina kazi ya kufanya kabla ya kufikia kiwango kinachostahiki, hata ingawa zimepiga hatua kubwa.

Mkutano huo wa kilele pia unalenga kutatua masuala ya ndani katika Umoja wa Ulaya. Waziri Mkuu aliyechaguliwa upya wa Uingereza David Cameron, atawasilisha suala lake la kutathminiwa upya masharti ya uwanachama wa nchi yake katika umoja huo, kabla ya kura ya maoni ya “kuwauliza wananchi ikiwa wanataka kubakia au kjiondoa, aliyoahidi kuandaa mwaka wa 2017.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef