1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushiriki wa Iran mkutano wa Syria bado kitendawili

21 Desemba 2013

Umoja wa Mataifa umeamua juu ya washiriki wa mazungumzo juu ya mgogoro wa Syria, lakini maafisa wamesema Ijumaa kuwa Marekani inajaribu kuizuwia Iran kushiriki katika mkutano huo uliopangwa kufanyika Januari 22.

https://p.dw.com/p/1AeQX
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya mataifa ya Kiarabu katika mgogoro wa Syria, Lakhdar Brahimi.
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya mataifa ya Kiarabu katika mgogoro wa Syria, Lakhdar Brahimi.Picha: Reuters

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu anaesuluhisha katika mgogoro wa Syria Lakdhar Brahimi, alisema karibu mataifa 30 yataalikwa katika mkutano huo mjini Montreux, na kuongeza kuwa ushiriki wa Iran ndiyo jambo pekee linalosababisha magawanyiko, lakini bado upo uwezekano wa taifa hilo kushiriki mazungumzo hayo. Wapinzani wa Syria pia wamepinga kuishirikisha Iran katika mazungumzo hayo.

Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Wendy Sherman akisalimiana na mwenzake kutoka Urusi Mikhail Bogdanov kabla ya kuanza kwa mikutano kujadili ya maandalizi ya Mkutano wa Geneva II.
Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Wendy Sherman akisalimiana na mwenzake kutoka Urusi Mikhail Bogdanov kabla ya kuanza kwa mikutano kujadili ya maandalizi ya Mkutano wa Geneva II.Picha: Getty Images

Siyo jambo sahihi
"Washirika wetu nchini Marekani bado hawajaridhishwa kwamba kuishirikisha Iran litakuwa jambo sahihi," Brahimi aliuambia mkutano wa waandishi wa habari na kuongeza kuwa "tumekubaliana kwamba tutazidi kuzungumza tuone kama tunaweza kufikia muafaka juu ya suala hili."

Matamshi yake yalifuatia siku ya mikutano na wawakilishi wa mataifa matano wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa - Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Marekani -pamoja na majirani wa Syria, Uturuki, Jordan, Lebanon na Iraq.

Pamoja na mataifa hayo, waalikwa wengine ni pamoja na Algeria, Brazil, Misri, Kuwait, Oman, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu. Mazungumzo halisi kati ya serikali ya rais Bashar Al-Assad na wawakilishi wa upande wa upinzani yataanza tarehe 24 Januari, katika makao ya Umoja wa Mataifa barani Ulaya, mjini Geneva.

Wajumbe wa majadiliano katika mkutano mjini Geneva.
Wajumbe wa majadiliano katika mkutano mjini Geneva.Picha: Getty Images

Sababu za Marekani kuizuwia Iran
Afisa mwandamizi wa serikali ya Marekani aliwaambia waandishi wa habari kwa sharti la kutotajwa jina, kwamba Marekani ilipinga kuishirikisha Iran kwa sababu nchi hiyo haijaridhia wazi kanuni za mkutano wa kwanza wa Geneva kuhusu amani ya Syria, uliyofanyika Juni 2012, na kwamba imeendelea kutoa msaada wa kijeshi kwa wanamgambo, wakiwemo washirika wa Iran kundi la Hezbollah kutoka Lebanon, ambalo linayasaidia majeshi ya Assad.

Kikosi cha kulinda mapinduzi cha Iran kimesema kina washauri wa ngazi za juu nchini Syria, lakini kinakanusha kuwapo na wapiganaji.

Mikutano ya siku ya Ijumaa iliwahusisha naibu mawaziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Mikhail Bogdanov na Gennady Gatilov, ambao nchi yao ndiyo mshirika mkubwa zaidi wa Syria, naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani anaehusika na masuala ya kisiasa Wendy Sherman, na majirani wa Syria, ambao wamekuwa wakikabiliana na mgogoro wa nchi hiyo pamoja na kuwapokea wakimbizi zaidi ya milioni 2.3 kutoka Syria.

Mji wa Aleppo unavyoonekana baada ya kushambuliwa.
Mji wa Aleppo unavyoonekana baada ya kushambuliwa.Picha: Reuters

Bogdanov akutana na wpinzani
Migogoro juu ya nani auwakilishe upinzani wa Syria na serikali, na iwapo Iran, Saudi Arabia na mataifa mengine ya kanda hiyo yashirikishwe au la, vimekwamisha majaribio ya awali kuzileta pamoja pande za Syria zinazopingana.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi ilisema katika taarifa kuwa Bogdanov, ambaye ndiye mjumbe maalumu wa rais wa Urusi katika mashariki ya kati, alikutana siku ya Alhamisi na katibu mkuu wa muungano wa upinzani wa Syria unaoungwa mkono na mataifa ya magharibi Badr Jamous, pamoja na maafisa wengine wa muungano huo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape
Mhariri: Abdu Mtullya