1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Ukraine zaafikiana mkataba wa gesi

3 Machi 2015

Umoja wa Ulaya umefaulu kuzishawishi Urusi na Ukraine kuufikia mkataba jana Jumatatu (02.03.2015) utakaohakikisha Ukraine inapata gesi hadi mwisho wa mwezi Machi baada ya Urusi kutishia kusitisha ugavi.

https://p.dw.com/p/1Ek8c
Symbolbild Russland Ukraine Gas Pipeline
Picha: Reuters

Mkataba hatimaye umefikiwa baada ya mazungumzo magumu mjini Brussels jana jioni ambayo yatahakikisha ugavi wa gesi nchini Ukraine na nchi za Umoja wa Ulaya unaendelea hadi mwisho wa msimu wa baridi.

Taarifa ya Halmashauri ya Ulaya imesema pande zote mbili zimethibitisha nia yao kutekeleza kikamilifu mkataba ulioafikiwa mwezi Oktoba mwaka uliopita. Katika mkataba huo Urusi iliahidi kuendelea kuipa Ukraine gesi hadi mwisho wa mwezi Machi, ili mradi malipo ya awali yanafanywa.

Akizungumza baada ya kuwa mpatanishi katika mazungumzo ya dharura kati ya waziri wa nishati wa Urusi Alexander Novak na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Demchyshyn, kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na masuala ya nishati Maros Sefcovic amesema ameridhika kwamba wamefaulu kuhakikisha ugavi kamili wa msimu wa baridi wa gesi unafanyika kwa mahitaji ya Ukraine.

Sefcovic aidha amesema ana imani ugavi wa gesi katika masoko ya Umoja wa Ulaya unabakia kuwa wa uhakika, huku kampuni ya gesi ya Ukraine Naftogaz na kampuni ya gesi ya Urusi Gazprom zikiafikiana makubaliano kuhusu malipo.

EU Kommissar Maros Sefcovic
Maros SefcovicPicha: AFP/Getty Images/E. Dunand

Waziri wa nishati wa Urusi Alexander Novak amesema, "Suala kuhusu msimu wa joto na masuala yanayohusiana na kuhifadhi gesi chini ya ardhi, yatajadiliwa mwisho wa mwezi huu. Mazungumzo yataendelea lakini kwa ujumla ili kutekeleza makubaliano ya Minsk tutakuwa na mashauriano zaidi kuhusu kufanya mazungumzo tofauti."

Pande hizo mbili zimekubaliana kuliacha suala la ugavi wa gesi katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi ya Luhansk na Donetsk nje ya mazungumzo hayo. Umoja wa Ulaya hupokea takriban theluthi moja ya gesi yake kutoka kwa Urisi, nyingi ikipitia Ukraine.

Poroshenko ataka tume ya kulinda amani

Hapo awali rais wa Urusi Vladimir Putin alizungumza kwa njia ya simu kuhusu mzozo wa Ukraine na utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano na mwenzake wa Ukraine Petro Poroshenko, kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa, Francois Hollande.

Weißrussland Minsk Ukraine Konferenz Poroschenko Merkel
Petro Poroshenko (kushoto) na kansela Angela MerkelPicha: Reuters/K. Kudryavtsev/Pool

Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya rais wa Ufaransa, viongozi hao walikubaliana ufanisi umepatikana, lakini jitihada zaidi zinahitajika kuboresha zaidi hali ilivyo hivi sasa. Viongozi hao pia wamekubaliana kuliomba Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, OSCE, kuwa na jukumu kubwa zaidi katika kuhakikisha mkataba wa usitishwaji mapigano unatekelezwa.

Ofisi ya rais Poroshenko imeandika barua kwa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya kuomba wanajeshi wa kulinda amani watumwe mashariki ya Ukraine ambako wanajeshi wa serikali wanapambana na waasi wanaoiunga mkono Urusi. Ofisi ya rais Poroshenko hata hivyo haikutoa maelezo ya kina kuhusu tume hiyo na lini inapotakiwa kuanza.

Urusi imelipinga vikali wazo hilo huku waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa nchi hiyo, Sergei Lavrov, akitaka mkataba wa amani wa Minsk uendelee kutekelezwa. Nchi za magharibi pia hazioni uwezekano wa tume ya kulinda amani kupelekwa Ukraine.

Mwandishi: Josephat Charo/AFP, AP, DPA, Reuters

Mhariri: Grace Patricia Kabogo