1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Unaijua Facebook 'Zero'?

24 Machi 2014

Je, unajua kuwa unaweza kuupata mtandao wa kijamii wa Facebook kwa gharama ndogo kabisa kwenye simu yako ya mkononi au pengine hata bila ya gharama yoyote ukitumia teknolojia mpya iliyopewa jina la Facebook 'Zero'?

https://p.dw.com/p/1BV8b
Mtandao wa Facebook kwenye simu za mkononi.
Mtandao wa Facebook kwenye simu za mkononi.Picha: picture alliance/AP Photo

Kwa kuwa upatikanaji na utumiaji wa Intaneti kwenye mataifa yanayoendelea ni changamoto kubwa kwa watoaji wa huduma hiyo, mitandao ya Facebook na Google ambayo inaongoza kwa kuwa na watumiaji wengi duniani, imekuja na suluhisho lao wenyewe kwa matumaini kwamba kutakuwa na kiwango kikubwa zaidi cha watumiaji kwenye maeneo hayo ya dunia na hivyo kuchochea ukuwaji.

Kama ilivyo, kwa Google Zero, Facebook Zero nayo ni huduma ya kupokea taarifa za maneno tu bila ya picha na ambazo ni bure kwa watumiaji wake. Huduma hiyo inayopatikana kwenye kiungo cha 0.facebook.com inatafautiana kidogo na ile inayopatikana kwenye m.facebook.com ambayo kwa hakika ni kwa ajili ya watumiaji wa simu za mikononi pia.

Kwa mujibu wa msemaji wa Facebook, Brandee Barker, huduma hiyo "huondosha kiwango chochote cha taarifa ambazo huchukua nafasi kubwa kama vile picha". Nambari 0 imetumika kumaanisha kuwa aina hii ya huduma inaingizwa kwenye kiwango cha sifuri katika kampuni za simu za mkononi, na hivyo aina maalum za taarifa haziingizwi kwenye malipo ya mwezi au ya kifurushi.

Hivyo, mtumiaji anaweza kutumia mtandao wa intaneti kwa zile kurasa ambazo zimeingizwa kwenye orodha hiyo ya 0 kama huu wa 0.facebook.com, lakini tu kwa sharti la kuwa kwenye nchi ambayo inaruhusu huduma hiyo na simu yenye mfumo wa WAP.

DW Kiswahili kwenye Facebook Zero

Kilicho muhimu ni kwamba kwa Facebook Zero, unapata kila kitu kwenye simu yako ya mkononi kikiwa kimerahisishwa na bila ya picha au vidio. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2010, huduma hii ya Facebook Zero, imeuongezea mtandao wa Facebook wateja maradufu.

Ipate Idhaa ya Kiswahili ya DW kupitia Facebook Zero.
Ipate Idhaa ya Kiswahili ya DW kupitia Facebook Zero.Picha: DW/D. Visevic

Ndani ya kipindi cha miezi 18 tu tangu kuanzishwa kwake, watumiaji waliongezeka kwa asilimia 114 barani humo, na kufikia Disemba 2011, watumiaji wa Facebook barani Afrika walikuwa zaidi ya milioni 37.

Ukiichukulia takwimu hii kieneo na kinchi, utakuta kuwa nchini Nigeria peke yake, idadi ya watumiaji Facebook ilichupa hadi asilimia 154, Ghana asilimia 85 na Kenya kwa asilimia 50.

Ukiwa nawe na simu yako ya mkononi na unataka kuwa mchangiaji wa moja kwa moja kwenye matangazo yetu ya Idhaa ya Kiswahili ya DW kupitia Facebook, basi ingia kwenye 0.facebook.com halafu itafute DW Kiswahili. Kwa urahisi wa fedha na wakati, utaweza kuungana nasi moja kwa moja na kuchangia maoni yako kupitia ukurasa wetu wa Facebook.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Google/Facebook
Mhariri: Saumu Yusuf