1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waiwekea vikwazo Sudan Kusini

Anuary Mkama/DPAE, AFPE 11 Julai 2014

Umoja wa Ulaya umetangaza majina ya wakuu wa kijeshi wa Sudan Kusini iliowaekea vikwazo vya kusafiri pamoja na kuzuia mali zao kutokana na kufanya ukatili dhidi ya raia wasio na hatia.

https://p.dw.com/p/1Cb1Q
Rais Salva Kiir wa Sudan ya Kusini (kulia) na aliyekuwa makamu wake na mpinzani wake mkuu wa sasa, Riek Machar, kabla ya wawili hao kutafautiana.
Rais Salva Kiir wa Sudan ya Kusini (kulia) na aliyekuwa makamu wake na mpinzani wake mkuu wa sasa, Riek Machar, kabla ya wawili hao kutafautiana.Picha: Ashraf Shalzy/AFP/Getty Images

Taarifa ya Umoja wa Ulaya iliyotolewa mapema Ijumaa, imetangaza kumuwekea vikwazo Peter Gadet ambaye ni kiongozi wa jeshi la waasi kutoka kabila la Nuer, ambaye pamoja na mengine inamtaja kuwa kikwazo cha kupatikana amani ya kudumu katika nchi hiyo ambayo imekuwa ikikabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tokea ipate uhuru wake miaka mitatu iliyopita.

Inasemekana Gadet, aliyewekewa vikwazo pia na Marekani mwezi Mei mwaka huu, alipanga na kuongoza mashambulizi katika mji wa Bentiu ambayo yalisababisha watu wapatao 200 kuuwawa.

"Peter Gadet anahusika katika kuchochea machafuko, kuzuia mchakato wa kisiasa Sudan Kusini pamoja na matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu," ilisema ripoti hiyo ya Umoja wa Ulaya.

Vikwazo vya matumizi ya silaha

Kwa upande wa jeshi la serikali, taarifa hiyo ya Umoja huo imesema imemuwekea vikwazo Santino Deng ambaye alikiuka makubaliano ya kusitisha vita yaliyosainiwa Januari 23 mwaka huu.

Watoto waliopoteana na wazazi wao kutokana na mapigano ya Sudan ya Kusini.
Watoto waliopoteana na wazazi wao kutokana na mapigano ya Sudan ya Kusini.Picha: Reuters

Katika taarifa yake nyingine iliyotoka mapema Ijumaa, Umoja wa Ulaya umesema kikwazo juu ya matumizi ya silaha kipo pale pale licha ya kwamba Umoja huo umebaini kuwa jeshi la serikali na waasi wameendelea kupokea silaha ambazo wamekuwa wakizitumia katika mapigano kati yao.

Umoja huo wa Ulaya umesema endapo pande hizo mbili zinazohasimiana hazitoheshimu mkataba wa kusitisha mapigano uliotiwa saini tarehe 23 Januari na kurudiwa tena tarehe 9 Mei, itatoa vikwazo zaidi kwa kila upande.

Zaidi ya watu millioni 1.5 hawajulikani walipo huku takribani watu 10,000 wameuwawa tokea kuanza kwa mapigano ya kugombania madaraka kati ya jeshi la serikali ya Sudan Kusini inayoongozwa na Salva Kiir dhidi ya waasi wanaoongozwa na aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar.