1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kuiongezea Urusi vikwazo

Elizabeth Shoo6 Machi 2015

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wako mjini Riga, Latvia, kujadili mzozo wa Ukraine ambao bado haujapatiwa ufumbuzi kamili. Miongoni mwa mengine wamekubaliana kuongeza vikwazo kwa Urusi.

https://p.dw.com/p/1Emmp
Mawaziri Steinmeier na Mogherini
Picha: Reuters/I. Kalnins

Katika mkutano wao mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya waliashiria utayari wa kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi ambayo wanasema inaingilia kati mzozo wa Ukraine. Hata hivyo viongozi hao wamesisitiza kuwa wataelekeza juhudi nyingi zaidi katika kuhakikisha kuwa makubaliano ya amani yaliosainiwa mjini Minsk mapema mwaka huu yanaheshimiwa. Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, alisema: "Daima tumeshikamana na tutaendelea kushikamana. Sio rahisi lakini ndicho kinachohitajika. Sisi tunafahamu fika, na wanachama wetu wanafahamu fika, kwamba umoja ndio nguvu yetu na kuonyesha umoja ndio jambo sahihi la kufanya."

Mogherini alikazia umuhimu wa nchi zote mwanachama kusimama pamoja na kufanya maamuzi ya pamoja linapokuja suala la kuiwekea Urusi vikwazo zaidi. Aidha alisema licha ya kwamba mapigano yamesimamishwa kwenye maeneo mengi ya Ukraine ya Mashariki, vikwazo kwa Urusi havitalegezwa.

"Mamlaka ya Ukraine yaheshimiwe"

Umoja wa Ulaya umeungana na Marekani katika kuiwekea vikwazo Urusi lakini baadhi ya nchi mwanachama zinapata wakati mgumu kukubali viongezwe kwani nchi hizo zinaitegemea Urusi kwa nishati kama vile gesi. Urusi imekanusha madai kwamba imechochea mzozo wa Ukraine kwa kupeleka wanajeshi na silaha kwa nia ya kuwaunga mkono waasi wanaotaka Ukraine ya Mashariki ijitenge.

Wanajeshi na waasi wameanza kuondoa silaha nzito kwenye uwanja wa mapambano Ukraine
Wanajeshi na waasi wameanza kuondoa silaha nzito kwenye uwanja wa mapambano UkrainePicha: Reuters/G. Garanich

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, Alhamisi alizungumza na rais wa Ukraine Petro Poroshenko na walikubaliana kwamba juhudi zinazoendelea sasa, yakiwemo mazungumzo ya mara kwa mara na wawakilishi wa pande zote katika mzozo wa Ukraine, ndio uamuzi sahihi utakaoleta amani ya kudumu. "Ukraine inahitaji mamlaka yake yaheshimiwe na pia inahitaji kuwa na amani," alisema Mogherini. "Lazima tushirikiane katika masuala hayo mawili: Kuhakikisha kwamba mamlaka ya nchi yanaheshimiwa na kwamba tunapata suluhu ya kisiasa itakayoleta amani."

Mogherini alizungumzia pia hali ya kibinadamu Ukraine Mashariki na kusisitizia umuhimu wa amani kurejea haraka iwezekanavyo. Watu wapatao 5,000 wamekufa mpaka sasa kwa sababu ya mapigano yaliyoanza mwaka uliopita.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/reuters/ap

Mhariri: Josephat Charo